1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Miaka 50 ya "I have a dream"

Elizabeth Shoo28 Agosti 2013

Imetimia miaka 50 tangu Martin Luther King alipotoa hotuba yake ya kihistoria. King aliyekuwa mwanaharakati wa kupigania haki za watu weusi Marekani, alizungumzia ndoto yake ya kuwa na nchi yenye usawa kwa wote.

https://p.dw.com/p/19Xpc
Martin Luther King
Martin Luther KingPicha: ullstein bild - AP

"Nina ndoto kwamba siku moja watoto wangu wanne wataishi kwenye nchi ambapo hawatatathminiwa kulingana na rangi ya ngozi yao bali kulingana na tabia yao." Ilikuwa tarehe 28 Agosti mwaka 1963, pale ambapo Martin Luther King na maelfu ya Wamarekani weusi waliandamana mjini Washington kudai uhuru na haki sawa ya kupata ajira kwa watu weusi. King alikuwa miongoni mwa waandalizi wa maandamano hayo na mmoja wa watu waliotoa hutoba siku hiyo. Hotuba yake ya I have a dream - yaani nina ndoto - inaelezea mustakabali anaoutamani kwa nchi yake. Alitaka Marekani iwe na umoja na watu wasibaguliwe kwa sababu ya rangi ya ngozi yao.

"Hatuwezi kuridhika iwapo mtu mweusi kutoka Mississippi hana haki ya kupiga kura na mtu mweusi anayeishi New York haoni sababu ya kupiga kura," alisema King katika hotuba yake. Miaka hamsini baadaye, sehemu fulani ya ndoto ya Martin Luther King imetimia. Kwa mara ya kwanza Marekani inaongozwa na rais mweusi.

Ubaguzi bado tatizo sugu

Barack Obama leo ataongoza maadhimisho ya miaka 50 ya hotuba ya King. Atatoa hotuba kwenye jengo la kumbukumbu ya Lincoln mjini Washington - mahali pale pale ambapo King alielezea ndoto yake miaka 50 iliyopita.

Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa Marekani
Barack Obama ni rais wa kwanza mweusi wa MarekaniPicha: Reuters

Obama ameeleza kuwa mafanikio yake kama mwanasiasa mwenye mamlaka makubwa zaidi Marekani, yamejengwa juu ya misingi ya juhudi za Martin Luther King na wenzake. Anaamini kwamba asingekuwa rais wa Marekani leo, kama wanaharakati wa kupinga ubaguzi wa rangi wasingekuwa tayari kuvumilia vitisho, mateso na hata kufungwa jela.

Hata hivyo, ubaguzi wa rangi bado ni tatizo sugu kwenye baadhi ya maeneo ya Marekani. Kisa cha kijana Trayvon Martin aliyepigwa risasi na Mmarekani mwenye ngozi nyeupe aliyehisi kuwa Treyvon ni kibaka kiliweka wazi kwamba bado yapo maoni potofu juu ya watu weusi. Suala lililozusha mjadala mkubwa zaidi ni kwamba aliyempiga risasi kijana huyo hakupewa hukumu yoyote mahakamani.

Sherehe za leo za mjini Washington zitahudhuriwa pia na marais wa zamani wa Marekani. Bill Clinton na Jimmy Carter ni miongoni mwa wale watakaotoa hotuba.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/Reuters/ap

Mhariri: Josephat Charo