1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo wa saa 24 waanza Ugiriki

Thelma Mwadzaya10 Desemba 2008

Nchini Ugiriki huduma zote za usafiri na afya zimekwama kufuatia mgomo wa jumla kote nchini humo.Mabenki,shule,viwanja vya ndege pamoja na hospitali vyote vimeathiriwa na hali hiyo.

https://p.dw.com/p/GCue
Waziri Mkuu wa Ugiriki Costas CaramanlisPicha: AP Photo

Hali hiyo inatokea baada ya maandamano kutokea kwenye miji ya Ugiriki baada ya kijana mmoja kuuawa na polisi juma lililopita.Uongozi nchini humo umetoa wito wa ushirikiano lakini vyama vya upinzani vinashikilia kuwa uchaguzi mpya ndio suluhu.

Wafanyikazi wanaoandamana katikati ya mji wa Athens walisikika wakipiga mayowe ya kuipinga serikali kwasababu ya sera mbaya za kiuchumi.

Ni siku tano tangu ghasia kuzuka nchini humo kufuatia mauaji ya kijana mmoja wa umri wa miaka 15.Kijana huyo Alexandros Grigoropoulos alipigwa risasi na polisi hadi kufa jumamosi iliyopita.Kwa mujibu wa Stathis Anestis msemaji wa shirikisho la wafanyikazi katika sekta binafsi GSEE mgomo huo unajumuisha sekta zote na shughuli zote zimekwama.

Makundi ya vijana walipambana na polisi hapo jana wakati wa maziko ya kijana huyo aliyeuawa wiki iliyopita.Mauaji hayo yamesababisha ghadhabu nchini humo wakati ambapo serikali inashtumiwa kwa kuhusika na kashfa,ukosefu wa nafasi za kazi pamoja na hali mbaya ya kiuchumi.


Waziri Mkuu wa Ugiriki Costas Karamanlis ametoa wito wa ushirikiano vilevile maandamano hayo kuvunjwa.''Sharti tuwe na msimamo wa pamoja kadhalika tulaani ghasia,wizi na uhalifu.Ni wajibu wetu kushirikiana ili kupambana na vitendo vya aina hii.''


Serikali imeahidi kuwalipa fidia wauza maduka wote iwapo mali zao ziliharibiwa wakati wa ghasia hizo.

Wanachama wa vyama vya upinzani kwa upande wao wamependekeza kufanyika kwa uchaguzi mpya kwani raia wa nchi hiyo hawana imani na uongozi uliopo.Giorgios Papandreou ni kiongozi wa chama cha upinzani cha Kisoshalisti na anasisitiza kuwa ''Hali ni mbaya na sote tuna wasiwasi kuhusu hatma ya nchi yetu.Hatujafurahishwa na kinachoendelea ila kuna tatizo kubwa zaidi linalokumba taifa hili.Tatizo lenyewe liko katika uongozi ambao haujatilia maanani masuala ya rushwa na uwazi.Serikali hii haijatatua matatizo ya kijamii ya nchi hii katika kipindi cha miaka mitano iliyopita.Kuna tatizo kubwa ndiposa nikatoa wito wa uchaguzi kufanyika.''

Kwa mujibu wa kura za maoni Chama tawala cha New Demokratik kilicho na wingi wa kura bungeni kimepoteza umaarufu wake.Afisa mmoja wa polisi tayari ameshtakiwa kwa mauaji ya kijana huyo Alexander Grigoropoulos ila amejitetea na kueleza kuwa risasi iliyosababisha kifo cha kijana huyo haikumlenga yeye.Maelezo kamili kuhusu kitendo hichi yanasubiriwa kutangazwa hii leo kadhalika afisa wa polisi mhusika na mwenzake wanatarajiwa kufikishwa mbele ya wachunguzi.

Maandamano hayo ambayo yamedumu kwa siku tano sasa yamesambaa katika yapata miji 10 nchini humo vikiwemo visiwa vilivyo maarufu kwenye sekta ya utalii vya Crete na Corfu.

Mgomo huo wa leo umeandaliwa na mashirika ya wafanyakazi nwa serikali ya GSEE na shirikisho la wafanyikazi katika sekta binafsi ADEDY.Maduka mengi yanaripotiwa kufungwa kwasababu ya kuhofia ghasia.Maandamano hayo ya tangu wiki iliyopita yamesababisha hasara ya mamilioni ya euro baada ya magari,maduka na mabenki kuteketezwa.