1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgomo kuendelea Ufaransa

Kabogo Grace Patricia18 Oktoba 2010

Hatua hiyo inatokana na vyama vya wafanyakazi wa reli kutangaza mgomo mpya hii leo.

https://p.dw.com/p/PgRR
Waandamanaji wakiwa katika mitaa ya Paris.Picha: AP

Nchini Ufaransa vyama vya wafanyakazi wa reli vimetangaza mgomo mpya hii leo na madereva wa malori wamesema walipanga kuzuia barabara kuu kuanzia jana jioni. Mgomo huo ni katika kuweka shinikizo jipya kwa Rais Nicolas Sarkozy kuachana na mpango wake wa mageuzi kuhusu pensheni ambao unapingwa.

Maandamano mapya kupinga mipango hiyo ya kuongeza umri wa chini wa kustaafu kufikia miaka 62 na umri kabisa wa kustaafu kuwa 67, yamepangwa kufanyika hapo kesho.

Maandamano hayo yataifanya wiki hii kuwa ya maamuzi kwa Rais Sarkozy kuendelea au kuachana na mpango huo. Bunge la nchi hiyo linatarajia kupigia kura mageuzi hayo ya pensheni siku ya Jumatano.

Wakati huo huo, hofu ya kwamba uwanja wa ndege wa kimataifa wa Charles de Gaulle wa mjini Paris huenda ukaishiwa mafuta katika muda wa saa 48 zijazo, imeondolewa na Waziri wa Usafiri, Dominique Bussereau.

Waziri huyo amekiambia kituo cha redio cha Europe 1 kwamba huduma za ugavi katika bomba la kupitisha mafuta kwenda kwenye uwanja huo wa ndege ambazo zilikuwa zimevurugika, sasa zimeanza tena.