Mgogoro wa Ukraine wapamba moto. | Matukio ya Kisiasa | DW | 23.04.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Mgogoro wa Ukraine wapamba moto.

Majeshi ya Ukraine yameanza hujuma mpya dhidi ya waasi wanaoipendelea Urusi, huku wanajeshi wa Marekani wakielekea katika eneo hilo la Mashariki ya Ulaya katika kile kinachoonekana kuwa ni kuonyesha mshikamano.

Marekani imesema inapanga kutuma wanajeshi 600 nchini Poland na mataifa ya baltic, ili kuwahakikishia uungaji mkono washirika wake, baada ya kutishia kuiwekea vikwazo zaidi Urusi. Wanajeshi 150 watawasili Poland leo na wengine 540 wanatarajiwa kuwasili Estonia,Latvia na Lithuania mnamo siku zinazokuja.

Mjini Kiev , kaimu rais wa Ukraine Oleksandr Turchynov ameamuru operesheni mpya ya kupambana na kile alichokiita kuwa ni " ugaidi," dhidi ya wanaotaka kujitenga na ambao wanaishikilia miji kadhaa.Hatua hiyo inafuatia kugunduliwa maiti za watu wawili , zikiwa zimeteswa vibaya , akiwemo mwanasiasa mmoja kutoka chama cha kiongozi huyo.

Mwanasiasa huyo alitekwa nyara wiki mbili zilizopita katika mji wa mashariki wa Slavyansk na Turchynov amewalaumu waasi kwa tukio hilo. Kwa upande mwengine mashambulizi mapya dhidi ya waasi sasa yanatishia kuyavuruga kabisa makubaliano yaliofikiwa wiki iliopita mjini Geneva baina ya Ukraine, Urusi na nchi za magharibi, kuutuliza mgogoro huo, ambao baadhi wanahofia unaweza ukazusha vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini humo.

Ukraine Interim Präsident Alexander Turtschinow 23.02.2014 2013

Rais wa mpito wa Ukraine Oleksandr Turchynov

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani John Kerry amekuwa na mazungumzo na mwenzake wa Urusi Sergei Lavrov, huku akielezea wasiwasi wake mkubwa juu ya ukosefu wa hatua za kupunguza uwezekano wa kupamba moto kwa mgogoro huo. pia Kerry ameonya kwamba kutokuweko kwa maendeleo yoyote baada ya makubaliano yaliofikiwa Geneva wiki iliopita, kutasababisha kuwekwa vikwazo zaidi dhidi ya Urusi.Marekani na serikali mpya ya Ukraine, zinaamini kwamba rais Vladimir Putin wa Urusi yuko nyuma ya uasi unaoendelea Mashariki mwa Ukraine.

Wakati huo huo, leo Urusi nayo imeishutumu Marekani ikisema ndiyo inayodhibiti na kuratibu vitendo vya serikali inayoungwa mkono na nchi za magharibi mjini Kiev.Jumuiya ya usalama na ushirikiano barani ulaya OSCE ambayo lina waangalizi 150 ndani ya Ukraine imeelezea wasiwasi wake kuhusu kupamba moto kwa mvutano nchini humo.

Mwandishi: Mohammed Abdul-Rahman, AFP

Mhariri: Saumu Yusuf

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com