1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgogoro wa kisiwa cha Comoro cha Anjouan

Abdulrahman, Mohamed13 Machi 2008

Kiongozi wa Anjouan asema yuko tayari kuzungumza lakini pia yuko tayari kupigana hadi kufa ikiwa atavamiwa.

https://p.dw.com/p/DNoo
Baadhi ya wakaazi wa Anjouan..Picha: picture-alliance / dpa/epa

Kiongozi huyo muasi alikua akizungumza na shirika la habari la Ufaransa na kituo cha matangazo ya televsisheni France 24 leo, siku moja baada ya wanajeshi wa umoja wa Afrika kuanza kukusanyika katika kisiwa kikuu cha Ngazija jana,wakiitikia wito wa serikali ya umoja wa Comoro ya Rais Ahmed Abdullah Sambi kuisaidia kukirejesha kisiwa cha Nzuwani katika mamlaka yake.

Bacar ambaye mara kadhaa ameukataa wito wa kumtaka aondoke madarakani na hata kupewa nafasi ya kwenda kuishi uhamishoni na hivyo kuondoa nafasi yoyote ya ufumbuzi kwa njia ya mazungumzo, anasema" wakati wote wamekua tayari kujadiliana na kuuliza kwanini leo pasisitizwe suluhisho la kijeshi ?"

Pamoja na hayo kiongozi huyo wa Anjouan ambaye matamshi yake yalionekana kuwa ni mchanganyiko wa upatanishi na ukaidi, akaonya kuwa ana silaha na wapiganaji wa kutosha kupambana na jeshi hilo la umoja wa Afrika, akiongeza " niko tayari kufa kulinda demokrasia na kupambana na wavamizi akatika Anjouan."

Akizumgumza na redio Deutsche juu ya msimamo wa serikali ya comoro kuhusiana na amatamshi ya Kanali Bacar kwamba yuko tayari kuzungumza, msemaji wa serikali ya Comoro Waziri wa elimu Abdulrahim Said Bacar aliitaja kauli hiyo kuwa ni kujaribu kupoteza wakati akisema kwamba,"Kauli yake imechelewa. hatuna muda wa kufanya mazungumzo naye. Tumefanya vikao vingi kutokana na juhudi nyingi za Umoja wa Afrika lakini hajaridhia. Alikataa kushirikiana na jamii ya kimataifa, hivyo sasa awe tayari kukubali yatakyomfika."

Akiulizwa kwanini serikali inakataa kumpa nafasi nyengine Kanali Bacar, wakati akiwa ameeleza kuwa tayari kuzungumza na hivyo kunusuru maisha ya watu wa kawaida wasiokua na hatia, msemaji huyo wa serikali ya Comoro Abdulrahim Said Bacar alisisitiza tena kuwa,"Hakutaka kuokoa maisha ya wakaazi wa Anjouan. Anafanya nini Anjouan kama anataka kuokoa maisha ya wakaazi wake ? Unajua kuna watu 2.500 wamelazimika kukimbia. Anawatesa watu. Kama alitaka kuokoa maisha angekubali juhudi za jamii ya kimataifa kusaka suluhu. Alikataa kwa hivyo hakuna njia jengine."

Umoja wa Afrika uliamua kuipa msaada wa kijeshi serikali ya umoja wa Comoro ambayo inavijumuisha visiwa vya Anjouan, Moheli na Ngazija, ili kumn´goa madarakani Kanali Bacar.

Kiongozi muasi wa Anjouan amekanusha kwamba kuna ukiukaji wa haki za binaadamu kisiwani Anjouan na kusema madai ya mteso ni ni njama iliopangwa na Rais Sambi. Matamshi yake hata hivyo yanasemekana kupingana na yale ya Wanzuwani waliokimbilia visiwa vya jirani.

Kanali Bacar anakitawala kisiwa cha Nzuwani tangu 2002, lakini akajitangaza tena mwenyewe kuwa mshindi wa uchaguzi Juni mwaka jana, uchanguzi ambao haukutambuliwa na serikali kuu ya Comoro wala na Umoja wa Afrika.

Hofu imetanda kisiwani humo , kukiwa na shauku katika visiwa vyengine, ni lini hasa uavamizi huo wa utafanyika. Maafisa wa umoja wa Afrika mjini Moroni wanasema wakati hauko mbali.