Mgodi waporomoka, zaidi ya watu 200 wafariki Kongo
2 Februari 2026
Ifahamike kuwa asilimia 15 ya madini ya coltan ulimwenguni yanatokea Rubaya na ni kiungo muhimu cha kutengezea simu za kisasa za mkononi na bidhaa nyeninge za kielektroniki.
Kwa mujibu wa Gavana wa Kivu ya Kaskazini aliyeteuliwa na waasi Bahati Musanga, watu zaidi ya 200 walipoteza maisha yao kwenye mkasa huo wa migodi ya Rubaya.
Gavana Bahati Musanga aliizuru Rubaya siku moja baada ya maporomoko ya ardhi kutokea na kuwataka wakaazi kuwa waangalifu.
"Nimefahamishwa kuwa mwaka 2017 zaidi ya watu alfu 2 waliuawa baada ya maporomoko ya ardhi kutokea, ukizingatia kilichotokea hapa nawaomba tuwe waangalifu. Ni sawa kusaka hela ila huwezi kuwa nazo ukiwa huko hai.”
Kulingana na mshauri wa gavana wa Kivu ya Kaskazini,idadi ya vifo imethibitika kuwa 227 ila hakutaka jina lake lifahamike.
Eliya Harerimana ni miongoni mwa manusura anasema waliwahi kuokolewa ndio maana hawakupata madhara makubwa.
"Nilikuwa kibarazani….nikauona mlima unaporomoka na tope zikatusomba.Tuliokolewa,,,ndio mana niko hapa.”
Hali ya mgodi wa Rubaya chini ya AFC/M23
Mgodi huo wa Rubaya umekuwa ukisimamiwa na kundi la AFC/M23 tanu mwaka 2024 na wahudumu wake wanachimba madini kwa mikono.
Kulingana na Umoja wa Mataifa,kundi la AFC/M23 limekuwa likipora rasilmali ya madini ili kufadhili shughuli zake ikiungwa mkono na nchi jirani ya Rwanda, kauli ambayo Kigali inaikanusha kwa nguvu zake zote.
Duru zinaeleza kuwa dhamira ya kundi hilo lililojihami kwa silaha nzito,ni kuipindua serikali ya Kinshasa na kuyalinda maslahi ya wa Tutsi wa Kongo walio wachache.
Mwaka uliopita lilipanua wigo wa operesheni zake hadi maeneo yaliyo na utajiri mkubwa wa madini ya mashariki mwa Kongo.Kulingana na shirika la habari la AFP, mkasa huo ulianza katikati ya wiki iliyopita.
Huduma za mawasiliano zimeathirika pakubwa
Rubaya ni eneo lililo na mabonde na makorongo na barabara zisopitika hasa wakati wa msimu wa mvua.
Kufikia sasa, huduma za simu za mkononi zimeathiriwa kwa siku kadhaa na makundi ya kiraia na serikali yamekimbilia sehemu salama zaidi.T
aarifa zinasambaa kupitia madereva wa pikipiki ambao ndio walio na uwezo wa kufika kwenye milima hiyo ya Rubaya isiyopitika.Kupitia mtandao wa X,ubalozi wa Ubelgiji mjini Kinshasa umeelezea mshikamano wake kufuatia mkasa huo.
Eneo la mashariki ya Kongo linalipakana na Rwanda na Burundi lililo na utajiri mkubwa wa madini limezongwa na mapigano yaliyodumu zaidi ya miaka 30.
Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa,M23 inasimamia operesheni za jimbo la Kivu ya Kaskazini sanjari na serikali kuu ya Kinshasa ili kudhibiti mgodi wa Rubaya.
Siku ya Jumapili,serikali kuu ya Kongo imeitolea wito jamii ya kimataifa kutathmini uzito wa mkasa huo mkono wa uasi na mfumo wa uporaji unaolaumiwa.
Kimsingi,uchimbaji rasmi wa madini na biashara hiyo imepigwa marufuku Rubaya tangu mwezi huu kuanza ila duru zinaeleza kuwa kati ya tani 112 na 125 za madini zinachimbwa kila mwezi na kusafirishwa hadi nchi jirani.