1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mgao wa maji Tanzania wazidisha adha kwa wananchi

11 Novemba 2021

Kumekuwa na mgao wa maji katika maeneo mengi ya nchini Tanzania hali ambayo imeibua hali ya wasiwasi kwa wananchi wengi. Mgao huo umezidisha adha kwa wakaazi ambao kwa miaka mingi wanaisumbukia huduma hiyo.

https://p.dw.com/p/42rJE
Menschen holen Wasser mit Eimern, weil es bei ihnen zuhause kein fließendes Wasser gibt
Picha: DW/E. Boniphace

Kihoro na wasiwasi kimeendelea kuwakumba wananchi ambao wanaona huenda wakajikuta wakiingia katika wakati mgumu hasa wakati huu kunakoshuhudiwa mabadiliko ya hali ya hewa kutokana na joto kali linalojitokeza katika maeneo mengi.

Ingawa baadhi ya mamlaka kama serikali kuu kujaribu kutoa maelezo ya kutia faraja kuhusiana na uhakika wa upatikanaji wa huduma hiyo muhimu ya maji, lakini ukweli wa mambo ni kuwa bado haijafamika mgao huo utafikia tamati wakati gani. Jijini Dar es salaam pekee, upatikanaji wa maji umekuwa wa shida, na tayari mamlaka ya majisafi na mazingira(Dawasa) imetahadharisha juu ya kuendelea kushuka kina cha maji katika mtu Ruvu.

Menschen holen Wasser mit Eimern, weil es bei ihnen zuhause kein fließendes Wasser gibt
Wanawake ndio wamekuwa wahanga wakubwa wa shida ya majiPicha: DW/E. Boniphace

Mkurugenzi mtendaji wa mamlaka hiyo,  Cyprian Luhemeje, anasema mgao huo ambao unayakumba maeneo yote ya jiji unafanywa kwa awamu na kila eneo linaweza kukosa huduma hiyo siyo chini ya saa 12. Kilio cha ukosefu wa maji ni cha miaka nenda rudi na waathirika wakubwa ni wanawake ambao siyo tu kwamba wanatumia muda mwingi kuyasaka lakini wakati mwingine wanakwenda umbali mrefu kuitafuta huduma hii.

Mama huyu kwa mfano hivi karibuni alifichua adha kubwa inayowaandama wanawake wengi ambao ndiyo wanaochukua jukumu la kutunza familia. Ripoti zinaonyesha kwamba, mgao wa  maji umetapakaa karibu maeneo mengi ya nchi huku sababu zikitajwa kama vile kuchakaa kwa mitambo, kupungua kwa kina cha maji na maelezo mengine ya hapa na pale.

Bungeni jambo hilo limejitokeza wakati ambapo mbunge mmoja aliamua kuibana serikali akihoji kulikoni jiji kama Dodoma kuendelea kuwa na mgawo wa kimya kimya kwa siku kadhaa sasa. Mgao wa maji pia umetipotiwa katika mikoa mingine kadhaa na kulingana na Kaimu Mkuregenzi wa majisafi na usafi wa mazingira mkoani Tanga, mhandisi Rashid Shabaani uwepo wa mgao wa maji katika eneo hilo kumetokana na kushuka kiwango cha uzalishaji maji katika mitambo yake.  Kama ilivyo kwa bawabu na mlango wote wakitegemeana ndivyo ilivyo kwa maji na uhai lakini hapa kikubwa zaidi ni kwamba pakosenekapo maji, uhai nao pia unatishiwa.