Mfungwa wa kigaidi aruhusiwa kuwasiliana na jamaa zake | Matukio ya Afrika | DW | 19.06.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mfungwa wa kigaidi aruhusiwa kuwasiliana na jamaa zake

Mahakama moja nchini Marekani imetoa uamuzi kwamba Mtanzania aliyefungwa kifungo cha maisha kwa mashambulizi dhidi ya ubalozi wa Marekani jijini Dar es Salaam, ana haki ya kuwasiliana na ndugu zake.

Jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Agosti 1998 yaliyofanywa na mtandao wa al-Qaida.

Jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Agosti 1998 yaliyofanywa na mtandao wa al-Qaida.

Akisoma uamuzi wa kesi hiyo, Jaji Marcia Krieger amesema marufuku ya mawasiliano aliyowekewa Khalfan Khamis Mohammed, mwenye umri wa miaka 40, "haikuwa na mashiko ya kisheria na yalikosa ushahidi wa kuithibitisha.

Katika hukumu yake ya kurasa 45, Jaji Krieger amesema hakuridhishwa na ushahidi kutoka afisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) kwamba Khalfan amekuwa akigoma kula, kutoa kauli mbaya dhidi ya Marekani na kuwazulia uongo wafanyakazi wa jela.

Jaji huyo ameliamuru shirika la upelelezi la FBI na maafisa wa jela kupitia upya orodha ya majina ya watu ambao wanaweza kuwasiliana na Khalfan.

Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya DW muda mchache uliopita akiwa mjini Zanzibar, Rubea Khamis, kaka yake Khalfan, amesema hukumu hii ina maana kubwa kwa familia yao kwani sasa ndugu yake "ataweza kuzungumza na watoto wao na jamaa zao wengine, ambao wamakuwa wakimjua kupitia hadithi tu."

Mfungwa hatari

Jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Agosti 1998 yaliyofanywa na mtandao wa al-Qaida.

Jengo la Ubalozi wa Marekani jijini Nairobi, Kenya, baada ya mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 7 Agosti 1998 yaliyofanywa na mtandao wa al-Qaida.

Khalfan alikuwa amelishitaki Shirika la FBI na Idara ya Magereza ya nchi hiyo kwa kumzuia kuwasiliana na ndugu na marafiki zake kadhaa, akiwamo mmoja wa kaka zake, akihoji kwamba marufuku hiyo ni kinyume cha Katiba ya Marekani.

Mfungwa huyo aliyetiwa hatiani kwa kuwa sehemu ya mtandao wa kigaidi wa al-Qaida amefungwa kwenye jela inayofahamika kama Supermax, jimbo la Colorado, inayotambuliwa kuwa kituo cha kuwazuilia wafungwa wanaoaminika kuwa hatari sana.

Dada yake waliyezaliwa pacha, Fatma Khamis, ameiambia DW kwa njia ya simu kutokea Zanzibar, kwamba licha ya pacha mwenzake kutumikia kifungo cha maisha, bado ana matumaini ya kuonana naye japo uzeeni.

"Vile kuonana tu hata kama tumekuwa wazee, tukaambiwa hawa ni mapacha, ni jambo kubwa sana kwetu."

Lawama kwa serikali ya Tanzania

Hadi muda mchache kabla ya uamuzi huu kutolewa, alikuwa anaruhusika tu kuwasiliana na watu maalum waliomo kwenye orodha ya serikali ya Marekani.

Upande wa serikali kwenye kesi hiyo ulikuwa unahoji kwamba bado Khalfan ni kitisho kwa usalama wa Marekani, licha ya kwamba anatumikia kifungo cha maisha jela.

Licha ya Tanzania kuwa nchi anayotokea mfungwa huyo, baadhi ya ndugu zake wameikosoa serikali ya nchi hiyo kwa kutokujihusisha kabisa na raia wao huyo tangu alipokamatwa nchini Afrika ya Kusini mwaka 1999 na kupelekwa Marekani.

"Serikali ya Tanzania haipaswi kumchukulia kuwa huyu (Khalfan) ni mkosa tu, bali ni raia wake." Msellem ameiambia DW kwa njia simu akiwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Miongoni mwa wafungwa walio kwenye jela hiyo ya Supermax ni mpangaji wa mashambulizi ya jengo la Shirika la Biashara Duniani ya mwaka 1993, Ramzi Yousef.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Josephat Charo