1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfumo wa afya DRC dhidi ya Ebola haukuwasaidia raia

Saleh Mwanamilongo
17 Septemba 2020

Taasisi ya utafiti  kuhusu Congo ya chuo kikuu cha NewYork, imesema mfumo wa kiafya wa kupambana na ugonjwa wa Ebola nchini humo haukuwasaidia raia bali kuwatajirisha maafisa wa serikali na mashirika ya misaada

https://p.dw.com/p/3idEX
Kongo: Erneuter Ausbruch von Ebola
Picha: Reuters/G. Tomasevic

Taasisi hiyo ya utafiti kuhusu Congo imeonyesha kwamba wizara ya afya na wadau wake wa kimataifa waliweka mfumo mbadala wa kiafya katika kupambana na Ebola.

Taasisi ya GEC ( Groupe de recherche sur le Congo) inasema mfumo huo mbadala wa kiafya uliwekeza fedha, lakini kwa bahati mabaya hazikuwanufaisha raia wa kawaida.

Ripoti ya taasisi ya GEC inaelezea kasoro chungu nzima zilizopelekea ugonjwa wa Ebola kudumu zaidi ya mwaka mmoja jimboni Kivu ya kaskazini. Miongoni mwa kasoro hizo ni pamoja na chanjo dhidi ya Ebola ambayo haikufanyiwa mchakato wa wazi kabla ya kuidhinishwa kwake. Kasoro nyingine ni kupelekwa kwa wahudumu wa afya wasiokuwa na ufahamu wa kutosha wa mila na desturi za watu wa Kivu. Hali hiyo ilisabisha raia wa huko kutokubali chanjo dhidi ya Ebola.

Kongo Mbandaka Ebola
Mfanyakazi wa afya akitoa chanjo ya Ebola Picha: picture-alliance/AP Photo/S. Mednick

Ripoti hiyo ya GEC inaeleza pia kwamba mfumo uliowekwa wa kupambana na Ebola huko kwenye majimbo ya Kivu na Ituri,haukuzingatia pia ujenzi wa miundo mbinu ya kudumu ya afya.

Tresor Kibangula amependekeza kwa serikali ya Congo kuwashawishi wadau wake wa kiafya kuwekeza kwenye mfumo wa kiafya wa kudumu.

Ripoti hiyo imetolewa wakati ambapo kuna kashfa ya ubadhirifu wa fedha zilizotengwa na serikali katika kupambana na janga la COVID-19 na ugonjwa wa Ebola nchini Kongo. Mwezi uliopita Rais Felix Tshisekedi aliagiza wizara ya afya ifanyiwe uchunguzi kuhusu matumizi ya dola milioni 11 za kupambana na COVID-19 na Ebola. Hatua hiyo ilifuatia tuhuma za naibu waziri wa afya dhidi ya waziri wake kwamba kumekuwa na ubadhirifu wa fedha hizo.

DR Kongo yaripoti maambukizi mapya ya Ebola

Kwenye ripoti yake mkaguzi mkuu wa hesabu nchini Kongo amesema kwamba fedha za serikali zilifujwa na wizara ya afya. Waziri wa Afya, Eteni Longondo amesema kwamba yuko tayari kutoa ushahidi wote kuhusu matumizi ya fedha hizo. Mjini Kinshasa na jimboni Equateur wahudumu wa afya wamegoma kwa wiki ya pili sasa wakidai nyongeza ya mshahara na kuboreshewa kwa mazingira ya kufanyia kazi.

Congo imejitahidi kupambana na ugonjwa wa ebola mara kadhaa ulipozuka hata bila kuweko na chanjo.