Mfanyabiashara haramu ya kusafirisha binadamu Libya auawa
2 Septemba 2024Mfanyabiashara haramu ya kusafirisha binadamu nchini Libya ameuliwa katika mji mkuu Tripoli jana Jumapili na kuchochea wasiwasi eneo la magharibi la nchi hiyo ya Afrika Kaskazini.
Maafisa wamesema Abdel-Rahman Milad, ambaye alikuwa akiongoza kikosi cha ulinzi wa pwani katika mji wa magharibi wa Zawiya, alipigwa risasi na kuuwawa na washambuliaji wasiojulikana.
Mazingira ya kifo chake hayakufahamika mara moja, na hakuna kundi lolote lililodai kuhusika na mauaji yake. Vyombo vya habari vya Libya vimeripoti kwamba Abdel-Rahman Milad, ambaye aliwekewa vikwazo na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa, alipigwa risasi alipokuwa ndani ya gari lake katika eneo la Sayyad, eneo la magharibi la mji mkuu Tripoli.
Hakuna kauli yoyote iliyotolewa na serikali yenye makao yake Tripoli ya waziri mkuu Abdul Hamid Dbeibah.