1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfalme Thailand amkatalia dada yake kugombea uwaziri mkuu

Iddi Ssessanga
9 Februari 2019

Mfalme wa Thailand amezuia jaribio la dada yake la kuwania nafasi ya waziri mkuu. Siku moja tu baada ya kuwasilisha jina la binti mfalme kuwa mgombea wake, chama cha Thai Raksa Chart kimesema kitatii amri ya mfalme.

https://p.dw.com/p/3D309
Maha Vajiralongkorn König  Thailand
Picha: Getty Images/P. Changchai

Chama cha upinzani nchini Thailand cha Thai Raksa Chart kilisema katika taarifa yake siku ya Jumamosi kwamba kitaheshimu na kutii amri ya mfalme inayobatilisha ugombea wa binti mfalme Ubolratana kwa nafasi ya waziri mkuu.

Chama hicho kimemshukuru binti Mfalme mwenye umri wa miaka 67 kwa juhudi zake, na kimesema kitaheshimu kanuni za uchaguzi na "mila za kitamaduni za kifalme" chini ya ufalme wa kikatiba wa Thailand.

Chama cha Raksa Chart kiliishitua nchi kilipomtangaza Ubolratana kama mgombea wake asubuhi ya Ijumaa. Baadae siku hiyo hiyo, mfalme Maha Vajiralongkorn, 66, alikosoa hatua hiyo kuwa isiyo ya kikatiba na "isiyofaa."

Katika taarifa yenye matamshi makali, mfalme alisema wanachama wa juu wa familia ya kifalme wanapaswa kubakia juu ya siasa na kutoegemea upande wowote wa kisiasa.

Thailand Prinzessin Ubolratana Rajakanya
Binti Mfalme Ubolratana Rajakanya.Picha: Reuters/C. Hartmann

Tume ya uchaguzi, ambayo inasimamia uchaguzi wa Machi, ilisema itatoa uamuzi wake kuhusu suala hilo siku ya Jumatatu. Wakati chombo hicho kina usemi wa mwisho kuhusu orodha ya wagombea, haina uwezekano wa kupuuza msimamo wa mfalme katika kuchukua uamuzi wake.

Vita katiya jeshi na wafuasi wa Thaksin

Uchaguzi mkuu ujao -- wa kwanza tangu mapinduzi ya mwaka 2014 -- unatazamwa na wnegi kama shindano kati ya jeshi la wale, kikiwemo chama cha Thai Raksa Chart, ambao ni watiifu kwa waziri mkuu wa zamani Thaksin Shinawatra.

Ugombea wa Ubolratana ungempambanisha na waziri mkuu Prayuth Chan-ocha, alieongoza mapinduzi ya 2014 dhidi ya serikali inayomuunga mkono Thaksin.

Binti Mfalme hakujibu moja kwa moja juhudi za kaka yake kufuta azma yake. Hata hivyo aliwashukuru wafuasi wake mapema Jumamosi na kusema alitaka Thailand "isonge mbele."

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dw

Mhariri: Zainab Aziz