Mfalme Qaboos wa Oman atimiza miaka 45 ya utawala | Matukio ya Kisiasa | DW | 18.11.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mfalme Qaboos wa Oman atimiza miaka 45 ya utawala

Mfalme Qaboos bin Said al Said amekuwa akiitawala Oman kwa miaka 45 baada ya kumpindua baba yake. Je, mfalme huyo ni mtu wa aina gani, ameibadili vipi nchi yake na ataachia lini madaraka?

Mansoor Al Shabibi anafunga funga vitu vyake, mtaalamu huyo wa fani ya maktaba mwenye ndevu zilizojaa mvi na uso wa tabasamu anataka kwenda zake nyumbani, kwa mkewe na watoto wake sita. Anahitaji nusu saa ikiwa atapita katika njia kuu ya Express. Al Shabibi anaithamini sana njia hiyo ya haraka. Alipokuwa mtoto safari yake hiyo ingedumu siku nzima. Wakati ule hakujakuwa na njia wala nyumba pembezoni mwa mji mkuu wa Oman Muscat. Na Oman ilikuwa miongoni mwa nchi ambazo hazikuendekea ulimwenguni.

"Tulikuwa tukilala juu ya mchanga," anakumbuka Mansoor, mwenye umri wa miaka 47. Umri wake wa kweli haujui. "Nyumba yetu ilijengwa kwa makuti. Kulikuwa na chumba kimoja na hakujakuwa na chochote ndani ya chumba hicho. Mamaangu alikuwa akipikia nje jangwani," anasimulia.

Mwana ampindua baba

Kasri la Mfalme wa Oman katika mji mkuu Muscat

Kasri la Mfalme wa Oman katika mji mkuu Muscat

Yalikuwa maisha ya shida yaliyowafanya waoman wengi kuihama nchi yao na kwenda kutafuta kazi katika nchi jirani. Sultan Said bin Taimur aliyeitawala nchi hiyo kuanazia mwaka 1932 hadi 1970 alikuwa akiangalia maendeleo kwa jicho la hofu. Hata radio na miwani watu hawakuwa wakiruhusiwa kuwa navyo.

Hali hiyo ilibadilika pale Qaboos bin Said al-Said alipoingia madarakani nchini Oman. Kwa msaada wa waingereza, Qaboos akampindua babaake madarakani na kuanzisha miradi ya maendeleo. Mapato ya shughuli za kutafuta mafuta zilizoanza katika miaka ya 60 nchini Oman yakasaidia kuigeuza nchi hiyo ya kifalme kuwa ya kimambo leo.

Hii leo nchi hiyo iliyoko mashariki ya bara arabu ina njia inayoifikia kila pembe ya nchi hiyo,ina shule na hospitali.Yote hayo kutokna na juhudi za mfalme Qaboos anasema Jürgen Werner, msomi katika chuo kikuu cha teknolojia cha Ujerumani mjini Muscat. "Mfalme amefanikiwa kuutumia ipasavyo utajiri wa nchi hiyo kwa masilahi ya nchi hiyo. Daima amekuwa akihakikisha kwamba kila mmoja anafaidika kwa njia moja au nyengine."

Uchumi wategemea mafuta

Hakuna umaskini nchini Oman. Hata hivyo wimbi la vuguvugu la mageuzi katika nchi za kiarabu liliitikisha kidogo nchi hiyo. Watu walipoteremka majiani mwaka 2011 nchini Tunisia, Misri na Syria, kulalamika dhidi ya serikali, maelefu pia waliteremka majiani nchini Oman. Waliandamana lakini sio dhidi ya mfalme, bali dhidi ya kuenea rushwa na kudai hali bora zaidi ya maisha.

Uchumi wa Oman wategemea mafuta kwa sehemu kubwa

Uchumi wa Oman wategemea uchimbaji na uuzaji wa mafuta kwa sehemu kubwa

Kwasababu kila mwaka maelfu ya vijana walikuwa wakimiminika katika soko la ajira, wengi wao wana shahada za vyuo vikuu. Lakini sio wasomi wote wenye kupata kazi. Idadi ya wasiokua na kazi ni kubwa na hasa miongoni mwa vijana-anasema mjasiria mali Murtadha Hassan Ali. "Zamani serikali ilikuwa ikiwaingiza katika idara za serikali vijana wengi kama ilivyowezekana. Lakini hilo sasa haliwezekani."

Zaidi ya hayo ajira nyingi inakutikana katika sekta ya kibinafsi na wengi wanaofanya kazi katika sekta hiyo ni wasomi kutoka nje kwasababu wana ujuzi mkubwa zaidi kuliko wenzao wa Oman, anasema Murtadha Hassan Ali.

Tatizo jengine kubwa linatokana na kupungua mapato ya shughuli za kuchimba mafuta kunakotokana na kupungua bei ya mafuta. Hata hivyo mfalme aliahidi miaka minne iliyopita, ili kutuliza hasira za waandamanaji, kubuni nafasi 50,000 za kazi katika sekta za serikali pamoja na kuwapatia Euro 300 kwa mwezi wanafunzi na watu wanaotafuta kazi. Wimbi la malalamiko likatulia lakini bajeti ya serikali ikapanda tangu wakati huo. Ingawa hakuna anaeyatia doa maendeleo yaliyopatikana, miaka 45 tangu mfalme Qaboos alipiingia madarakani, hata hivyo wadadisi wanajiuliza nani atakaekamata nafasi yake? Hadi hii leo hajulikani.

Mwandishi: Allmeling, Anne/Hamidou Oummilkheir

Mhariri: Josephat Charo

Sauti na Vidio Kuhusu Mada

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com