1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Abdullah azikwa makaburi ya watu wa kawaida

Admin.WagnerD23 Januari 2015

Mfalme Abdullah ibn Abdul-Azizi, moja wa watu matajiri zaidi katika historia ya dunia, amezikwa katika kaburi la kawaida ambalo halikuanishwa mjini Riyadh, katika mwendelezo wa utamaduni wa kujinyima anasa za mwili.

https://p.dw.com/p/1EPl3
Jeneza la marehemu Abdullah bin Abdul-Aziz likibebwa na wanafamilia kwenda kuzikwa.
Jeneza la marehemu Abdullah bin Abdul-Aziz likibebwa na wanafamilia kwenda kuzikwa.Picha: Reuters/Faisal Al Nasser

Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan, waziri mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif na viongozi wa Sudan na Ethiopia, waliungana na watawala wa mataifa ya Ghuba katika swala ya Janaaza iliyofanyika katika msikiti wa Imam Turki bin Abdullah. Walisali sambamba na mrithi wa Abdullah ambaye pia ni mdogo wake wa baba mmoja, mfalme Salman bin Abdul-Azizi.

Picha za video ziliuonyesha mwili wa Abdullah uliyofunikwa kwa nguo nyeupe, ukiwa kwenye jeneza iliyobebwa na wana wa familia ya Kifalme waliovalia mavazi ya asili ya Shamagh, baada ya swala ya Janaaza au sala ya kumuombea maiti. Mwanamfalme Miteb bin Abdullah, waziri wa ulinzi wa taifa na mtoto wa marehemu mfalme, alikuwa miongoni mwa waliobeba jeneza la Abdullah.

Marehemu Abdullah ibn Abdul-Aziz enzi za uhai wake.
Marehemu Abdullah ibn Abdul-Aziz enzi za uhai wake.Picha: Reuters/Z. Abd Halim

Uharamu wa maombolezo ya majivuno

Kulingana na mafundisho ya Wasunni wa Wahabi ambayo ndiyo yanafuata rasmi nchini Saudi Arabia, kuonyesha huzuni kwa majivuno au kuomboleza ni jambo lisilokubalika, linalofananishwa na kumshirikisha Mwenyezi Mungu.

Hakukuwa na kipindi rasmi cha maombolezo nchini Saudi Arabia na bendera zote nchini humo zilipepea mlingoti kamili. Na licha ya umaarufu wake miongoni mwa raia, hakukuwa na mikusanyiko ya mitaani kuashiria kifo chake. Ofisi za serikali zilifungwa kwa siku za mwisho wa wiki wa mashariki ya kati, ambazo ni Ijumaa na Jumamosi, na zitafungua siku ya Jumapili kama kawaida.

Wakati sala ya Ijumaa iliyotangulia mazishi yake ilihudhuriwa na viongozi wa Kiislamu, wanamfalme wa Saudia, na matajiri wa Kiarabu na wafanyabiashara, mwili wake ulisafirishwa msikitini kwa gari la wagonjwa la jiji.

Mfalme mpya wa Saudi Arabia Sulaiman bin Abdul-Aziz. akilihutubia taifa baada ya kutawazwa.
Mfalme mpya wa Saudi Arabia Sulaiman bin Abdul-Aziz. akilihutubia taifa baada ya kutawazwa.Picha: Reuters/Saudi Press Agency

Tofauti na Falme za Ulaya

Hayo yalikuwa ni mabadiliko kwa Mfalme, ambaye wakati wa uhai wake alisafiria katika anasa inayotarajiwa kwa mtawala wa juu kabisaa wa taifa linaloongoza kwa mauzo ya mafuta duniani. Watangulizi wa Abdullah na ndugu zake wengine, pia walizikwa katika makaburi yasiyoainishwa.

Familia ya Al-Saud imekuwa ikijatahidi kujitofautisha na falme za Ulaya, ikipendelea kurejea kwenye misingi ya kikabila ya uongozi wake ambamo Wasaudi wa kawaida wanakuwa na uwezo kinadharia kuwalalamikia wafalme.

Abdullah na mrithi wake Salman wanajitanabaisha kama wafalme na walinzi wa misikiti miwili mitakatifu - ishara ya wazi ya namna wanavyochukulia kwa umuhimu imani yao ya dini katika kutegemeza uhalali wao.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre, afp

Mhariri: Saumu Yusuf