1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu Mzee Kassim Mapili

Christopher Buke1 Juni 2007

Ni mmoja wa wanamziki wakongwe nchini Tanzania

https://p.dw.com/p/CHc4

Kwa kweli jina la Kassim Mapilli lilikuwa geni makikioni mwangu lakini yule binti alizidi kunisisitiza nimtafute mkongwe huyo katika fani ya muziki Tanzania.

“ Huyo ndio atakupa kila kitu, ana majina ya wanamuziki wote nchini walio hai na waliokufa mimi sijui anaishi wapi lakini mpigie namba yake ya simu si nimekupa?”

Dada Vicky mwandishi wa habari wa michezo wa gazeti la Mwananchi alinielekeza.

“Mi naitwa Kassim Mapilli, nani mwenzangu”?, mkongwe huyo alihoji baadaa ya kumpigia simu mikiomba miadi naye.

Kwanza alifurahi, akawa hata anasita kuzungumza nami anaelekeza simu yake karibu na radio iliyokuwa ikiimba wimbo wa zamani, “ si unasikia ndugu mwandishi hizi ndio zangu”, kikafuata kicheko.

Kweli kwa waswahili mtu wa namna hii humuita mzungu maana kesho yake muda tuliokubaliana alikuwepo.

Ndipo tukaanza moja kwa moja kazi. Alianza kujitambulisha “Mimi naitwa Ndugu Kassim Saidi Mapilli. Nilizaliwa mwaka 1937 katika kijiji cha Lipuyu, tarafa ya Lionya wilaya ya Nachingwea Mkoani Lindi.”

Ni mtoto wa mzee Saidi Amri Mkolela na mama yake ni Ajena Binti Mussa Mtikita. Alipata elimu yake ya msingi katika shule ya msingi Lionja baadae akahamia Wilayani Lindi katika kitongoji cha Mtama.

Ni kwenye kitongoji hiki alipopata mlipuko wa kipaji chake cha muziki. Akiwa huko aliingia maddrasa (shule iliyokuwa inafundisha lugha ya kiarabu na mafunzo ya dini ya kiislamu) kwa sheikh Abduli Kahali, kama ilivyo kwa watoto wa kiislamu.

Kwanza upigaji wake wa dufu ulikuwa sio wa kawaida. Dufu ni kifaa mithili ya matari, au mgoma iliyoachwa wazi sehemu moja ambayo mara nyingi hupigwa kwa viganja likitoa mlio mtamu kwenye nyimbo zenye maadhi ya kiislamu au kaswida ukitaka, na mara nyingi wasikilizaji au waimbaji wakiitikia kwa kuyumba kutoka upande mmoja kwenda mwingine.

Kutokana na kuwa na hamu ya kujiendeleza kimaisha Bwana Kassimu aliachana na mafunzo hayo na kwenda mjini Lindi mwaka 1958 ambapo alianzisha biashara ndogo ndogo.

Licha ya hivyo wazimu wa mirindimo ya dufu wakaendelea kumwandama. hakuwa na jinsi ispokuwa kuwapunga kwa kuanza kujifunza muziki.

“ Ndipo niaanza kujifunza muziki na kuwa hasa mwanamuziki chini ya uongozi wa Bwana Hamisi Seif Mayocha kwenye bendi ya White Jazz ya mjini Lindi,” anasisitiza mzee Mapili.

Lakini kama ilivyo ada ya wanamuziki mwaka 1959 alihama kutoka kwenye bendi hiyo ambayo ilimpatia ujuzi wa muziki na kwenda mkoani Mtwara. Huko akajiunga na bendi iliyojulikana kama Mtwara jazz akiwa kama mwimbaji.

Mwanamuziki huyu chipikizi akaanza kuimba kwenye bendi hiyo akishirikiana na mwanadada mmoja aliyejulikana kwa jina la Mwajuma Chitumbili.

Mwaka 1962 aliihama Mtwara jazz bendi na kujiunga na Honolulu jaz ya hapo hapo Mtwara.

Huko nyuma akapata habari kuwa mwalimu wake na mshirika wake wa zamani wa kule Lindi Bwana Hamisi, Seif Mayocha ameunda bendi nyingine, kwa hiyo mwaka 1963 akarudi tena Lindi na kujiunga tena na Bwana Mayocha.

Lakini bendi nayo ikaja kubadilisha tena jina na kuitwa Tanu Youth League band ingawa mara hii chini ya uongozi wa Mapili.

Kwa hatua hii kwa hiyo akawa mtu mzima katika ulimwengu wa muziki.

Maendeleo na mafanikio haya mapya yakamtia mori mwanamuziki huyo lakini ambaye mwezi Desemba 1964 akahamia Tunduru mkoani Ruvuma na kuanzisha bendi iliyojulikana kama TYL.

Hata kwenye bendi hiyo hajatulia sana maana kama ujuavyo katika muziki ni kuhama hama. Mara hii alifuatwa na uongozi wa bendi ya Kilwa jazz iliyokuwa ikiongozwa na Hamad Kipande ambaye sasa ni Marehemu.

Baadhi ya nyimbo ambazo Bwana Kassim alizitunga kipindi hiki ni pamoja na Ewe Mola tunakuomba ubariki Afrika, Dunia kukaa wawili wawili, Dolie mimi nakwambia, sikutegemea na Yatanikabili.

“ Nilikaa na bendi hiyo mpaka mwezi Desemba 1965 nikaihama kilwa na kwenda Mgulani ambako nilianzisha bendi ya JKT baada ya kununuliwa vyombo vipya vya muziki.

Tulianzisha bendi ambayo ilikuwa inaitwa JKT Kimbunga jazz pamoja na wanamuziki wenzangu kama vile Athumani Omari, Msenda Saidi, Vinyama Kiss Rajabu” anasema Mapili ingawa hata kwenye bendi hii hajakaa sana kwani alitimkia bendi ya polisi ambayo alikaa muda mrefu.

Haikuchukua muda mrefu kama ilivyo utaratibu wa jeshi hili Mapili naye akaajiriwa kama askari polisi na kupewa namba ya kazi B 3710.

Akiwa katika bendi hii akishirikiana na wanamuziki wenzake ambao ni pamoja na ali Omari Kayanda, Kassim Mponda, Manzi Matumla, Abdu Ali Mwalugembe, Plimo Gandam, Bosco Mfundiri, Juma Ubao na Kitwana Majaliwa.

Ni katika bendi hii alikuja kukutana na mwanamuziki ambaye baadaye alikuja kuvuma na kuwa mashuhuri sana nchini Tanzania Moshi William (sasa ni Marehemu).

Ngekewa yake ikazidi kupanda maana akiwa katika bendi hii ya polisi aliteuliwa kuifundisha bendi ya akina mama wa Tanu Youth League.

Bendi hii anasema ikafanya vizuri kiasi ikawa miongoni mwa bendi zilizokaribishwa kwenda nchini Kenya katika miji ya Naibrobi na Mombasa ambapo ilipiga wakati wa sikukuu za Kenyatta Day.

Bila shaka ni sifa hizi na nyingine zilizomsaidia kupandishwa cheo na kuwa Koplo mwaka 1973 . miaka miwili baadae alikwenda Msumbiji na bendi hii ya polisi kwenye sherehe ya uhuru wa wanchi hiyo.

Anadai nyimbo alizotunga akiwa katika bendi ya polisi ni pamoja na Dunia ni watu, kashinagali ugupina, lijelalwa ngwamba, Ashijajani mweshimajani mwe pamoja na Nataka uoe mke uwe mume wa nyumbani.

Mwaka 1980 Mapilli akafanya jaribio lake la kwanza la kuacha kazi analodai lilimletea shida sana kazini ingwa anakuwa na ukakasi kutaja ilikuwa shida gani lakini anasisitiza kuwa baadae 1981 akakubaliwa kuacha kazi.

Ni tangia wakati huu alipoanza kujiunga na kuongoza vyama mbalimbali vya muziki nchini. Kwa mfano baada ya kuhudhuria semina ya Baraza la Muziki Tanzania BAMUTA mwaka 1982 alichaguliwa kuwa mwenyekiti wa mpito wa chama kipya kilichoanzishwa yaani Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania CHAMUDATA.

Katika mwaka huo wa 1984 Mapilli akawa mwenyekiti wa kwanza wa CHAMUDATA. Mojawapo ya kazi zilizofanwa na chama hiki ni pamoja na kuwaleta pamoja jumla ya wanamuziki 57 mwaka 1986 ambao walitunda nyimbo zilizokuwa na mafanikio ya kisiasa sio tu Tanzania bali hata Afrika kwa ujumla.

Nyimbo hizo ni pamoja na ule wa kutoa rambi-rambi kwa ajiri ya kifo cha rais wa kwanza wa msumbiji Hayati Samora Machel, wimbo wa miaka 20 ya kuzaliwa Azimio la Arusha na wimbo uliokuja kujulikana nchini Tanzania kama fagio la chuma.