1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mfahamu mfalme Haile Selassie wa Ethiopia

Amina Mjahid
30 Mei 2018

Jua historia ya Haile Selassie Mwanamfalme kijana RasTafari Makonnen aliyevikwa taji la mfalme Haile Selassie mwaka 1930.

https://p.dw.com/p/2yfJD

Mfalme Haile Selassie, ‘Simba wa Yuda anayeshinda’, anawakilisha ukoo wa kifalme wa karne nyingi. Alikuwa kiongozi wa kiimla lakini pia wa kisasa ambaye alianzisha mabadiliko ambayo yalichangia kuanguka kwake. 

Haile Selassie aliishi wakati gani? Haile Selassie alizaliwa kama Tafari Makonnen Julai 23, 1892, karibu na Harar, Ethiopia. Babake alikuwa binamu na mshirika wa karibu wa mfalme mkuu Menelik II. Aliitwa katika mahakama, iliyoko Addis Ababa wakati babake alipoaga dunia mwaka 1906. 

Mwaka 1916 alibadili jina na kuwa Ras Tafari, mrithi mdhaniwa na mtawala mshikiliaji wa mfalme wa kike Zauditu, binti yake Menelik II, na mwaka 1928 yeye na wafuasi wake walimfanya Zauditu amtawaze mfalme.

Mwaka 1930, kufuatia kifo cha Zauditu, Tafari alitawazwa kuwa mfalme mkuu Haile Selassie – "Nguvu ya Utatu". Aliangushwa katika mapinduzi ya utawala wa kikomunisti wa Derg mwaka 1974 na akafa chini ya mwaka mmoja badaye, Agosti 26, 1975, mjini Addis Ababa.

Haile Selassie
Picha: Comic Republic

Ni misingi ipi aliyoweka Haile Selassie kwa taifa lake? Kwa mara ya kwanza alianzisha katiba iliyoandikwa kwa taifa lake mwaka 1931; katiba hiyo ilitoa nafasi ya mabunge mawili na utaratibu wa sheria na kutangaza kuwa watu wote Ethiopia ni sawa. Hata hivyo katiba hiyo ya kwanza na ya pili iliyoidhinishwa mwaka 1955 zilikosolewa kwa kumpa mamlaka makubwa zaidi mfalme mkuu -alibakisha haki ya kufutilia mbalia uamuzi wowote wa bunge na kwa kutoweka vipengele vya kuruhusu vyama vya siasa. 

Je, Haile Selassie hakosolewi? Kuanzia miaka yake ya mwanzo, Tafari Makonnen anachukuliwa kuwa mpanga mikakati mzuri. Huenda alihusika katika njama ya kumuondoa mfalme mkuu mteule Lij Iyasu, mtangulizi wa Zauditu, aliyetawala kwa miaka mitatu. Akiwa mfalme mkuu, Haile Selassie aliwapa fursa maelfu ya wanafunzi kusomea nje. Ni wanafunzi hao hao ambao baadaye walioanzisha harakati za kumpindua wakisema wanataka mabadiliko. Kuchoshwa na utawala wake kulisababisha jaribio la mapinduzi mwaka 1960, ambalo lilikuwa kitisho kikubwa zaidi kwa utawala wake hadi alipopinduliwa na Derg.

Nifahamishe kuhusu shauku ya Haile Selassie juu ya ushirikiano wa kimataifa. Kama mtawala, Ras Tafari aliileta Ethiopia katika Ligi ya Mataifa mwaka 1923, moja ya mataifa huru machache wakati huo na moja lililopatiwa uanachama.

Mwaka 1963, mfalme huyo aliandaa mkutano wa kwanza wa Shirika la Umoja wa Afrika (OAU), na baadaye ikawa Umoja wa Afrika. Alisaidia kuchapisha sheria za kwanza za Umoja huo na kuwa mwenyekiti wake wa kwanza. Makao yake makuu yalianzishwa Addis Ababa.

Asili ya Afrika: Haile Selassie

Haile Selassie alitazamwa vipi Ujerumani? Katika kutilia mkazo shauku yake katika ushirikiano wa kimataifa, Haile Selassie alisafiri sana. Mwaka 1954, alikuwa kiongozi wa kwanza wa taifa kuizuru Jamhuri mpya ya shirikisho la Ujerumani, akipokea kile ambacho kingripotiwa kuw amapokezi makubwa kuwahi kupewa kwa mgeni yeyote tangu kumalizika kwa vita. Alikaribishwa kama kiongozi sawa na juu ya yote aliwa anataka kujifunza kuhusu maendeleo ya kiufundi - kiafya, kilimo na kiviwanda -- ambavyo angerejea nayo nyumbani. Ethiopia ilisalia kuwa mshirika wa karibu wa Ujerumani na Haile Selassie aliandaliwa tena mapokezi muruwa mjini  Bonn mwaka 1973, mwaka mmoja kabla ya kupinduliwa.

Nukuu za Haile Selassie:

"Mbali na Ufalme wa Bwana, hakuna taifa hapa ulimwenguni ambalo liko juu ya lingine..Leo ni sisi. Kesho ni wewe."

             — Hotuba katika Ligi ya Mataifa, 1936, akiomba msaada wa kuyaondoa majeshi ya ukaliaji ya Kitaliano.

"Historia inatufunza kuwa umoja ni nguvu na inatutahadharisha kuzika na kuzishinda tofauti zetu kwasababu ya malengo sawa, kujitahidi kwa nguvu zetu zote kwa njia ya kweli, umoja na udugu wa Afrika."
                —Hotuba ya kukubali uenyekiti, alipochaguliwa kuwa kiongozi wa kwanza wa Shirika la Umoja wa Afrika,1963

Urithi wa Haile Selassie ni upi? Haile Selassie aliipatia Ethiopia chuo chake kikuu cha kwanza, shule, hospitali na serikali kuu. Mageuzi aliyotekeleza yalimaanisha kuwa Ethiopia ilifungua milango kwa ulimwengu wa nje na mfalme huyo mkuu alitambuliwa kimataifa kuwa kiongozi mwenye shupavu na mwenye haiba-nafasi aliyotumia kwa maslahi mema ya Afrika kwa ujumla, akipigia debe juhudi za bara hilo. Viongozi wa Afrika baada ya uhuru walimuona kama mtetezi wa maadili ya Afrika na uhuru. Viongozi wa Ulaya walimuona kama mpinga ufashisti na kule Jamaica, marasta walimuabudu kama Mesaya.  

Jackie Wilson na Yilma Haile Michael wamechangia katika makala hii. Ni sehemu ya makala maalum za  mfululizo wa "Asili ya Afrika", ushirikiano kati ya shirika la DW na taasisi ya Gerda Henkel.

Mwandishi: Jackie Wilson and Yilma Haile Michael 
Imetafsiriwa na: Shisia Wasilwa
Mhariri: Iddi Ssessanga