1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meya mpya wa London amshutumu Cameron

8 Mei 2016

Meya mpya wa jiji la London Sadiq Khan amemshutumu Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron kwa kutumia mbinu alizoziita za "Donald Trump" kujaribu kuigawa jamii katika juhudi za kumzuwia kupata ushindi katika uchaguzi.

https://p.dw.com/p/1IjnO
Sadiq Khan London Großbritannien Vereidigung
Sadiq Khan katika sherehe za kuapishwa katika kanisa la Southwark mjini LondonPicha: Reuters/Y.Mok

Siku moja baada ya kuapishwa akitoa ahadi kwamba "atakuwa meya wa wakaazi wote wa London" mbunge huyo wa chama cha Labour amekishutumu chama cha Cameron cha kihafidhina kwa kujaribu kumhusisha na watu wenye itikadi kali ya Kiislamu wakati wa kampeni za uchaguzi.

"Walitumia hofu na maneno ya kejeli kujaribu kuyabadilisha makundi ya kikabila na kidini kupambana wao kwa wao kitu ambacho moja kwa moja ni mbinu za Donald Trump, " Khan aliandika katika gazeti la Observer.

Sadiq Khan London Großbritannien Vereidigung
Sadiq Khan(kulia) akipongezwa baada ya kuapishwaPicha: Reuters/Y.Mok

"Watu wa London walistahili kitu bora na nina matumaini ni kitu ambacho chama cha kihafidhina hakitajaribu kurudia tena."

Khan alishinda kwa asilimia 57 ya kura siku ya Alhamis katika uchaguzi wa Meya, akipata kura milioni 1.3 na kumshinda tajiri mkubwa kutoka chama cha kihafidhina Zac Goldsmith na kuweka historia kuwa Muislamu wa kwanza kuwa meya wa mji mkuu katika mataifa ya magharibi.

Mtoto wa mhamiaji

Khan mwenye umri wa miaka 45 , mtoto wa mhamiaji kutoka Pakistan ambaye alikuwa dereva wa basi , alisifu ushindi wake kama ushindi wa "Umoja dhidi ya mtengano" baada ya wiki za ukosoaji kutoka chama cha kinafidhina kuhusiana na kujitokeza kwake hapo zamani katika matukio ya wazi pamoja na Waislamu wenye imani kali.

Großbritannien Cameron und Johnson in London
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron (kulia)pamoja na Boris Johnson meya wa zamaniPicha: picture alliance/empics/Y. Mok

Idadi kadhaa ya wanasiasa wa chama cha kihafidhina wameshutumu matamshi hayo katika kampeni, lakini waziri wa ulinzi Michael Fallon amesema maswali yaliyojitokeza yalikuwa ni halali.

Khan amekiri kuwakilisha "baadhi ya watu ambao hawastahili" katika wakati wa kazi zake zilizopita kama mwanasheria wa haki za binadamu lakini amesema mawazo yao yalikuwa yanachukiza.

"Wagombea wote waliulizwa maswali juu ya maisha yao ya nyuma, walivyo, maamuzi yao, watu waliokuwa wakijihusisha nao," Fallon ameiambia redio ya BBC.

Sadiq Khan London Großbritannien Vereidigung
Sadiq Khan akipongezwa baada ya kuapishwa kuwa meya wa LondonPicha: Reuters/Y.Mok

"Hii ndio hali ya demokrasia yetu na mapambano ya kuzuka na kuanguka kisiasa."

Meya wa wakaazi wote wa London

Khan aliapishwa kuwa meya katika sherehe kubwa iliyohudhuriwa na watu wa imani mbali mbali katika kanisa kuu la Southwark , akiahidi kuwakilisha,"kila jamii " na kila sehemu ya jiji hilo, kama Meya wa wakaazi wote wa London".

Hillary Clinton, ambae anaelekea kupata uteuzi wa chama chake kuwa mgombea wa kiti cha urais kupitia chama cha Democratic atakabiliana na mgombea anayeonekana kupata uteuzi wa chama cha Republican Donald Trump , ameongoza pongezi za kimataifa zinazomiminika kwa Khan.

Großbritannien Sadiq Khan & Zac Goldsmith in Sikh Tempel
Sadiq Khan na Zac Goldsmith katika nyumba ya ibada ya Singasinga mjini LondonPicha: Imago/i Images

Meya wa jiji la New York Bill de Blasio amesema anatarajia kufanyakazi pamoja na , "mwanaharakati mwenzake anayepigania watu kupata nyumba rahisi" wakati meya wa mjini Paris Anne Hidalgo ameandika katika ukurasa wa Tweetter kwamba "ubinadamu na upenda maendeleo wa Khan utawafaidia watu wa jiji la London."

Nchini Pakistan , Bilawal Bhuto , kiongozi wa chama cha upinzani cha Pakistan People's Party na mtoto wa kiume wa waziri mkuu wa zamani Benazir Bhutto , na kiongozi hasimu wa upinzani Imran Khan pia wameandika pongezi zao katika ukurasa wa Tweeter.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe

Mhariri: Caro Robi