Merz asema hakati tamaa kufanya kazi na Trump
4 Mei 2026
Kansela wa Ujerumani Friedrich Merz amesema hatakata tamaa kufanya kazi na Rais wa Marekani Donald Trump licha ya mzozo kati ya viongozi hao kuhusu vita nchini Iran.
Akizungumza jana kwenye mahojiano na kituo cha utangazaji cha umma ARD Merz alijaribu kupunguza mvutano wowote na Trump akisema kwa mfano kwamba tangazo la ghafla la hadharani kuwa Marekani itawaondoa wanajeshi 5,000 kutoka kambi za kijeshi nchini Ujerumani halikushangaza na halipaswi kuonekana kama kulipiza kisasi.
Merz alisema uamuzi wa Marekani kuhusu wanajeshi si jambo jipya na haukuwa na uhusiano wowote na kutokubaliana hivi karibuni.
Kansela huyo pia alionekana kuthibitisha kwamba kuletwa nchini Ujerumani kwa makombora ya masafa marefu ya Marekani chapa Tomahawk, kulikotangazwa na rais wa zamani wa Marekani Joe Biden, kunafutwa angalau kwa sasa.
Merz alisema uamuzi huo unatokana na silaha hizo kupungua kwa sababu ya vita nchini Iran na Ukraine.