1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na karata zake za wakimbizi

7 Septemba 2015

Wahariri wa magazeti ya Ujerumani wanazingatia mgogoro wa wakimbizi, azma ya waziri Steinmeier kugombea urais na kujiimairsha kijeshi kwa Urusi nchini Syria.

https://p.dw.com/p/1GS6W
Ungarn Budapest Flüchtlinge mit Merkel Plakaten
Picha: Getty Images/AFP/C. Stache

Mhariri wa gazeti la General Anzieger anazungumzia mkakati wa kansela Angela Merkel kuhusu wakimbizi, akisema kwa sera yake ya kiutu kuelekea wakimbizi, Merkel amefanikiwa kuepusha mkwamo wa kisiasa.

Kwa upande mmoja amesema Ujerumani itaweza kumudu mtiririko wa wakimbizi wanaoingia Ujerumani, lakini kwa upande wa pili ametoa wito wa kuwepo na mgawanyo wa haki wa wakimbizi katika mataifa ya Umoja wa Ulaya.

Kwa upande mmoja anaruhusu kukikukwa kwa mkataba wa Dublin linapokuja suwala la wakimbizi wa Syria, lakini kwa upande anayaulumu mataifa mengine kwa kutoheshimu makubaliano. Hayo ni mambo ambayo hayaendi sawia, anasema mahariri huyo.

Je, hii ndiyo Ulaya tunayojivunia?

Ulaya ya zamani inaitazama Ulaya mpya ya Mashariki kwa kirahi. Hungary haijajaribu hata mara moja kuonyesha utu katika namna inavyowashughulikia wakimbizi wanaoingia katika mipaka yake. Hapo ndipo mhariri wa gazeti Hannoversche Allgemeine anauliza je, hii ndiyo Ulaya inayojivunia mustakabali mwema?

Mhariri anajibu swali lake akisema hali haipaswi kuwa na kamwe isiwe hivyo. Lilikuwa ni jambo la kiutu kufungua mipaka. Ujumbe wa mamia ya Wajerumani waliojitokeza kwenye vituo vya treni mjini Munich, Dortmund au Hamburg wakipiga makofi ulikuwa zaidi ya kuwakaribisha watu waliokuwa na safari ndefu na iliyojaa vizingiti.

Wameonyesha taswira inayokinzana kabisaa na matukio ya kutisha yaliyoyashuhudiwa katika vituo vya treni mjini Budapest. Ujumbe wa wasamaria wema hao ulikuwa bayana, kwamba sisi ndiyo tunaamua aina ya Ulaya tunayoitaka.

Mhariri wa gazeti la Frankfurter Allgemeine, anasema Ujerumani inavutia na iko imara ikilinganishwa na mataifa mengine, lakini peke yake haiwezi kuumudu mtiririko wa wakimbizi kwa kuwa unahitaji fedha nyingi na mifumo ya umma inayofanya kazi vizuri kuweza kuwahudumia mamia kwa maelfu ya wakimbizi ipasavyo. Mhariri huyo anasema raia hawapaswi kubebeshwa mzigo wa kuwahudumia wakimbizi.

Putin ataka kuipiga kumbo Marekani Mashariki ya Kati

Mhariri wa Kölner Stadt-Anzeiger anazungumzia hatua ya rais Vladimir Putin wa Urusi kuimarisha uwepo wa majeshi yake nchini Syria. Anasema rais Putin anatuma majeshi yake katika nchi iliyoharibiwa vibaya na iliyoko kwenye kingo za kufilisika kwa malengo ya kimkakati.

Mpango huo unaungwa mkono pia na kipenzi cha Putini, rais wa Misri Abdul-Fatah Al-Sisi. Wote hao wana ndoto ya kuwa na Mashariki ya Kati inayoelemea upande wa Urusi na ambayo mwishowe inaweza kujiondoa katika ushawishi wa Marekani na Ulaya.

Steinmeier autaka urais wa shirkisho

Mhariri wa gazeti la Badische Neueste Nachrichten anazungumzia azma ya waziri wa mambo ya kigeni wa Ujerumani Frank-Walter Steinmeier kuchaguliwa kuwa rais wa shirikisho la Ujerumani akisema:

Bila shaka Frank-Walter Steinmeier anaweza kuwa rais mzuri - upole wake na diplomasia vimemjengea waziri huyo wa mambo ya nje heshima inayovuka nje ya mipaka ya chama chake cha SPD.

Lakini kwa njia ya kuelekea kasri la rais la Bellevue, vikwazo bado ni vile vile vilivyomfanya ashindwe katika azma yake ya kuwa Kansela mwaka 2009. Kuchukuwa wadhifa kama huo siyo kikwazo kwa mtu wa aina yake, kikwazo ni kuupata.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Saumu Yusuf