1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Hollande wazuru Ukraine

5 Februari 2015

Katika juhudi mpya za kutafuta amani mashariki mwa Ukraine viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wametangaza Alhamisi (05.02.2015) wanakwenda Kiev na Ijumaa Moscow na pendekezo la kukomesha mapigano.

https://p.dw.com/p/1EWDJ
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: picture-alliance/epa/O. Hoslet

Katika juhudi mpya za kutafuta amani mashariki mwa Ukraine viongozi wa Ujerumani na Ufaransa wametangaza leo hii kwamba watakwenda Kiev na Moscow na pendekezo la kukomesha mapigano hayo.

Juhudi hizo za kidiplomasia za ngazi ya juu zina lengo la kukomesha kuzuka upya kwa mapigano mashariki ya Ukraine ambayo yanatishia usalama barani Ulaya. Ujerumani na Ufaransa zinataraji safari hii zinaweza kufanikiwa kupatikana kwa makubaliano ya amani ambayo yanaweza kukubaliwa na Ukraine halikadhalika Urusi.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa amesema yeye na Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wataelekea katika mji huo mkuu wa Ukraine Kiev leo hii na hapo kesho watakwenda Moscow na pendekezo lenye kuzingatia kuheshimiwa kwa mipaka ya ardhi ya Ukraine.Uamuzi huo wa ziara ya ghafla umekuja wakati Marekani ikielekea kuipa Ukraine msaada wa silaha za kijeshi jambo ambalo nchi nyingi za Ulaya inalipinga

Kama ishara ya umuhimu wa juhudi hizo hii itakuwa ziara ya kwanza ya Merkel mjini Moscow tokea kuzuka kwa mzozo huo wa Ukraine mwaka mmoja uliopita.

Hollande amekaririwa akisema isingelifaa kusemwa kwamba Ufaransa na Ujerumani kwa pamoja hazikujaribu kufanya juhudi zozote zile na kuchukuwa hatua yoyote ile kudumisha amani.

Marekani haikujulishwa

Afisa mwandamizi wa serikali ya Ufaransa amesema viongozi hao wawili waliamuwa jana usiku juu ya safari hiyo na hawakushauriana na maafisa wa serikali ya Marekani kuhusu mpango wao huo.Afisa aliyesema hayo alikuwa haruhusiwi kutaja jina lake.

Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: Reuters/P. Wojazer

Msemaji wa Merkel Steffen Siebert amesema kutokana na kupamba moto kwa mapambano kulikoshuhudiwa siku chache zilizopita ,Kansela na Rais Hollande wanaimarisha juhudi zao walizokuwa wakiziendeleza kwa miezi kadhaa ili kuweza kufikia suluhisho la amani kwa mzozo huo.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraine akimkaribisha Waziri wa mambo ya nje wa Marekani mjini Kiev leo hii ameuita wakati huu kuwa muhimu sana kwa historia yao.

Marekani yatafakari kuipa silaha Ukraine

Baada ya kukutana na Rais Poroshenko mjini Kiev Waziri wa mambo ya nje wa Marekani John Kerry ameitaka Urusi kujitolea kuutatua mzozo huo kwa njia ya amani ya kidiplomasia.

Rais Petro Poroshenko wa Ukraina akimkaribisha Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry katika Kasri la Rais mjini Kiev.(05.02.2015)
Rais Petro Poroshenko wa Ukraina akimkaribisha Waziri wa Mambo ya nje wa Marekani John Kerry katika Kasri la Rais mjini Kiev.(05.02.2015)Picha: picture-alliance/TASS/Ukrainian presidential press service

Kerry yuko Ukraine kuonyesha uungaji mkono wa serikali ya nchi hiyo inayopigwa vita wakati utawala wa Rais Barack Obama wa Marekani ukitafakari kupeleka silaha Ukraine kuisaidia nchi hiyo kupambana na waasi wanaoegemea upande wa Urusi.

Mwanadiplomasia huyo wa Marekani anaipelekea nchi hiyo msaada mpya wa kibinaadamu wa dola milioni 16.4 lakini serikali ya Ukraine ina shauku ya kusisitiza ombi lake la kupatiwa msaada wa silaha.

Rais Obama alikuwa amepinga fikra ya kupeleka silaha Ukraine lakini duru zinasema msimamo huo unaweza kubadilika kutokana na mapigano yaliyozuka karibuni.

Putin yuko tayari kwa mazungumzo

Mjini Moscow mshauri wa masuala ya kigeni wa kingozi wa Urusi Yuri Ushakov amesema Rais Vladimir Putin yuko tayari kuwa na mazungumzo ya tija na Rais Hollande wa Ufaransa na Kansela Merkel wa Ujerumani.

Rais Vladimir Putin wa Urusi.
Rais Vladimir Putin wa Urusi.Picha: picture-alliance/TASS/Russian presidential press service

Amesema mkutano huo ni hatua muhimu na kwamba anataraji mpnago wao huo utazingatia hatua zilizopendekezwa na Putin mapema wakati wa kuanza kwa mzozo huo.

Urusi imekuwa ikanusha vikali kwamba madai ya kuwasaidia waasi huko Ukraine wakati ikikiri kwamba wapiganaji wa kujitolea wa Urusi wanapambana upande wa waasi.Wataalamu wa mataifa ya magharibi wanasema kuwepo kwa idadi kubwa ya silaha mikononi mwa waasi kunaonyesha jinsi dai hilo lisivyokuwa na ukweli.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/Reuters

Mhariri :Josephat Charo