1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Hollande wataka kukomeshwa mapigano Ukraine

Mohamed Dahman6 Februari 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa wamesema watatumia nguvu zote katika ziara zao mjini Kiev na Moscow kukomesha umwagaji damu Ukraine na kuyapa uhai makubaliano ya Minsk.

https://p.dw.com/p/1EXQR
Kansela Angela Merkel mara baada ya kuwasili Moscow.(06.02.2015)
Kansela Angela Merkel mara baada ya kuwasili Moscow.(06.02.2015)Picha: Reuters/Sergei Karpukhin

Akizungumza mjini Berlin Ijumaa (06.02.2015) kabla ya kuondoka kuelekea Moscow mjii mkuu wa Urusi kukutana na Rais Vladimir Putin,Merkel amekanusha kwamba yeye na Rais Hollande katika mazungmzo yao hayo ya pamoja na Putin wako tayari kuwapa ardhi zaidi waasi wa Ukraine na kuongeza kusema kwamba kamwe hatoshughulikia masuala ya ardhi yanayohusiana na nchi nyengine.

Juhudi hizo za kidiplomasia zinakuja kutokana na kupamba moto kwa mapambano mashariki mwa Ukraine kulikoipelekea Marekani kufikiria kulipatia jeshi la Ukraine silaha uamuzi ambao Ujerumani na mataifa mengine ya Ulaya yanaupinga.

Hakuna ufumbuzi wa kijeshi

Merkel haamini kwamba mzozo huo wa Ukraine unaweza kutatuliwa kijeshi.Amesema "Tuna imani kwamba hakutakuwa na ufumbuzi wa kijeshi kwa mzozo huu.Lakini pia tunajuwa kwamba masuala bado yako wazi kabisa iwapo tutafanikiwa kusitisha mapigano kwa kupitia mazungmzo haya. Hatujuwi iwapo tutafanikiwa leo au pengine itabidi kufanyike zaidi.Hatujuwi iwapo mazungumzo hayo ya leo mjini Moscow yatachukuwa muda mrefu au yatakuwa mafupi au iwapo pengine yatakuwa mazungumzo ya mwisho."

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi katika mkutano na waandishi wa habari Berlin kabla ya kuondoka kwenda Moscow.(06.02.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani akiwa na Waziri Mkuu wa Iraq Haider al-Abadi katika mkutano na waandishi wa habari Berlin kabla ya kuondoka kwenda Moscow.(06.02.2015)Picha: Reuters/H. Hanschke

Kwa mujibu wa Merkel hali ni tete na watajaribu kuchangia kila wanachoweza kupata ufumbuzi wa mzozo huu na hususan kukomesha umwagaji damu.

Naye Rais Hollande akizungumza mjini Paris leo, kabla ya kuelekea uwanja wa ndege kwa safari ya kwenda kukutana na Putin mjini Moscow amesema kwamba kila mtu anatambuwa kuwa hatua ya kwanza lazima iwe kusitisha mapigano na iwapo hilo halitofanikiwa hapo itabidi lazima watafute ufumbuzi wa dunia.Hata hivyo amesema wanapaswa kuwa na matumaini kwa juhudi hizo zao mpya.

Msimamo wa Merkel ni ishara nzito kwa Obama

Hapo jana Merkel na Hollande walikutana na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine mjini Kiev na hapo kesho kiongozi huyo wa Ujerumani na Rais wa Ukraine watauhutubia Mkutano wa Usalama mjini Munich Ujerumani ambao pia utahudhuriwa na Makamo wa Rais wa Marekani John Biden na Waziri wa mambo ya nje wa Urusi Sergei Lavrov.

Hapo Jumatatu Merkel atakuwa na mazungumzo muhimu na Rais Barack Obama wa Marekani mjini Washington ambapo msemaji wa Ikulu ya Marekani amesema msimamo wa Merkel wa kupinga kupatiwa silaha kwa Ukraine unatowa ishara nzito kwa Obama.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa mjini Kiev. (06.02.2015)
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa mjini Kiev. (06.02.2015)Picha: picture-alliance/dpa/N. Maxim

Makamo wa Rais wa Marekani Joe Biden akizungumza mjini Brussels leo hii amesema kwamba Umoja wa Ulaya na Marekani lazima ziwe kitu kimoja kuisaidia Ukraine wakati Urusi ikiendelea kuupalilia mzozo huo. Amesema Ukraine kwa hivi sasa inapigania uhai wake.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AP/dpa

Mhariri :Josephat Charo