1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel na Hollande wajadili mzozo wa wahamiaji

Admin.WagnerD24 Agosti 2015

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani Jumatatu (24.08.2015) anakutana na Rais Francois Hollande wa Ufaransa mjini Berlin kutowa msukumo mpya kwa Ulaya kukabiliana na mzozo mkubwa wa uhamiaji kuwahi kushuhudiwa kwa miaka 50.

https://p.dw.com/p/1GKWn
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.
Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na Rais Francois Hollande wa Ufaransa.Picha: AP

Mkutano wao huo pia utazungumzia kuibuka upya kwa matumizi ya nguvu Ukraine na utahudhuriwa na Rais Petro Poroshenko wa Ukraine ambapo baada ya viongozi hao kukutana na waandishi wa habari watakuwa na majadiliano wakati wa chakula cha usiku.

Merkel na Hollande wamejitwika wajibu mkubwa wa kisiasa kuupatia ufumbuzi wa uasi wa miezi 16 wa wanaharakati wanaoungwa mkono na Urusi nchini Ukraine na kurudisha amani katika nchi hiyo ilioko kwenye mpaka wa mashariki na Umoja wa Ulaya.

Duru za Ukraine zinasema kwamba kutojumuishwa kwa Rais Vladimir Putin wa Urusi katika mkutano huo kunaonyesha kwamba Ujerumani na Ufaransa wako upande mmoja na Ukraine lakini duru za Ufaransa zimezima mara moja tafsiri kwamba kuna vita vya kidiplomasia dhidi ya Urusi.

Shinikizo la uhamiaji

Wakati huo huo shinikizo la kidiplomasia kuhusu wahamiaji linakuja wakati Umoja wa Ulaya ukikabiliana na miminiko mkubwa wa wahamiaji usio na kifani wanaokimbia vita, ukandamizaji na umaskini. Umoja wa Ulaya umeulezea mzozo huo wa wakimbizi kubwa mbaya kabisa kuwahi kushuhudiwa tokea Vita Vikuu vya Pili vya Dunia.

Hii ndio hali inayowakabili wahamiaji wanaokimbilia Ulaya.
Hii ndio hali inayowakabili wahamiaji wanaokimbilia Ulaya.Picha: Reuters/O. Teofilovski

Takwimu rasmi zinaonyesha wahamiaji 107,500 wamevuka kuingia Umoja wa Ulaya mwezi uliopita na wito umekuwa ukiongezeka kwa umoja huo kuchukuwa msimamo wa pamoja zaidi kukabiliana na miminiko huo wa wahamiaji.

Wakati Ulaya ikikabiliana na hali hiyo wanasiasa wa Ujerumani wana wasi wasi wa athari za kifedha na kisiasa kwa nchi yao ambayo ndio nchi yenye kupokea idadi kubwa ya wakimbizi miongoni mwa nchi za Umoja wa Ulaya.

Vurugu dhidi ya wahamiaji

Polisi imepambana na wafuasi wa sera kali za mrengo wa shoto kwa siku mbili mfululizo nje ya kituo cha kuwahifadhi kwa muda wahamiaji katika mji wa Heidenau karibu na Dresden mashariki mwa Ujerumani.

Vurugu dhidi ya wahamiaji Heidenau.
Vurugu dhidi ya wahamiaji Heidenau.Picha: picture-alliance/dpa/A. Burgi

Waziri Mkuu wa jimbo la Saxony Stanislaus Tillich alilitembelea eneo hilo hapo Jumapili na kulaani vurugu za wafuasi hao wanaopinga kupewa hifadhi kwa wakimbizi.

Tillich amekaririwa akisema "Haikubaliki kwamba watu wanaotafuta hifadhi, wafanyakazi au polisi wanashambuliwa kwa sababu ya chuki isiokuwa na msingi.Jambo hilo haliwezi kuvumiliwa."

Ujerumani ambayo ina sheria za wastani kuhusu watu wanaotafuta hifadhi inataraji idadi ya wakimbizi kuongezeka mara tatu zaidi mwaka huu na kufikia 800,000.Kansela Angela Merkel amesema ni tatizo kubwa kabisa linaoikabili Umoja wa Ulaya kuliko hata mzozo wa madeni wa Ugiriki.

Hata hivyo Rais wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya Jean Claude Juncker amepuuza wito wa kuitishwa kwa mkutano mpya wa kilele wa Umoja wa Ulaya kuhusu uhamiaji kwa kusema kwamba nchi wanachama ziache kuburuza miguu na kutekeleza makubaliano yalioko juu ya suala hilo.

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri :Mohammed Abdul-Rahman