Merkel kugombania tena uongozi | Matukio ya Kisiasa | DW | 01.08.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel kugombania tena uongozi

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani ambaye ameiongoza Ujerumani tokea mwaka 2005 kuwania muhula wa nne na ameanza kupanga kampeni yake ya kuwania kuchaguliwa tena hapo mwaka 2017 kwa mujibu wa jarida la Der Spiegel.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Msemaji wa chama cha Merkel cha Christian Demokratic (CDU ) amekataa kuzungumzia repoti hiyo ya Jumamosi (01.08.2015) ambayo jaridha hilo mashuhuri la Der Spiegel halikutaja chanzo chake. Merkel ambaye mara nyingi amekuwa akiitwa kuwa ni mwanamke mwenye nguvu kubwa kabisa duniani yuko mapumzikoni kwenye milima ya Alps.

Kansela huyo wa Ujerumani ambaye ametimiza umri wa miaka 61 hapo Julai 17 hakuwahi kutowa tamko lolote hadharani iwapo atagombea muhula wa nne au la juu ya kwamba aliwahi kudokeza kwenye hotuba mjini Cologne mwaka jana kwamba angeligombea tena.

Merkel ambaye aliingoza Ujerumani taifa lenye nguvu kubwa za kiuchumi barani Ulawa wakati wa msukosuko wa kifedha hapo mwaka 2008 na wakati wa machafuko ya kanda ya sarafu ya euro amekuwa akihesabika wakati wote kuwa mmojawapo wa viongozi mashuhuri kabisa wa Ujerumani jambo ambalo sio kawaida kwa kansela anayeendelea kuwa madarakani.

Hakuna ukomo wa ukansela

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani.

Nchini Ujerumani hakuna ukomo wa muhula wa uongozi madarakani na kansela wa mwisho kutoka chama cha CDU Helmut Kohl aliongoza kwa miaka 16 kabla ya kupoteza jaribio lake la kuwania muhula wa tano hapo mwaka 1998 baada ya kushindwa na Gerhard Schroeder wa chama cha Social Demokratik (SPD).Makansela hao wote wawili hawakuwahi mashuhuri miongoni mwa wapiga kura kama vile alivyo Merkel.

Katika nchi ambayo inathamini utulivu baada ya machafuko ya jamhuri ya Weimar kuchangia kuibuka kwa utawala wa Hitler Merkel ni kansela wa nne wa baada ya kipindi cha vita nchini Ujerumani.Chama chake cha CDU hadi sasa hakina mrithi wake anayetambulikana dhahir.

Kijarida hicho cha kila wiki cha Der Spiegel kinachoaminika nchini Ujerumani kimeandika kwamba imedhihirika kwamba Merkel ameamuwa kuwania tena muhula mwengine madarakani hapo mwaka 2017 habari ambazo zitakifurahisha chama chake cha kihafidhina ambacho kinategemea umashuhuri wake kuendelea kushikilia ukansela baada ya kushindwa mara kadhaa katika chaguzi za majimbo.

Mikutano ya mkakati

Katibu Mkuu wa chama cha CDU Peter Tauber .

Katibu Mkuu wa chama cha CDU Peter Tauber .

Der Spiegel limesema amekuwa na mkutano wa kupanga makakati hivi karibuni na katibu mkuu wa chama cha CDU Peter Tauber,meneja wake wa kampeni na meneja wa chama chake Klaus Schueler kujadili kampeni.

Kijarida hicho kimesema operesheni za kampeni zinapaswa kufanyika makao makuu ya chama hiki cha CDU na kwamba ikiwa kama ni matokeo ya mkutano huo wafanyakazi tayari wameanza kuandikishwa.

Der Spiegel vile vile limesema Merkel pia alijadili hivi karibuni mkakati huo wa uchaguzi na Horst Seehofer kiongozi wa chama cha (CSU) cha jimbo la Bavaria ambacho ni chama ndugu na chama cha CDU.Baada ya mkutano huo Seehofer ametowa wito wa vyama hivyo kuweka lengo la kujipatia ushindi wa viti vingi kuiwezesha kuunda serikali bila ya kushirikikisha vyama vyengine hapo mwaka 2017.

Umashuhuri wa Merkel

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakati wa mikutano ya mzozo wa Ugiriki.

Kansela Angela Merkel wa Ujerumani wakati wa mikutano ya mzozo wa Ugiriki.

Merkel ni mashuhuri sana nchini Ujerumani kiasi kwamba kiongozi mmoja wa SPD Torsten Albig waziri mkuu wa jimbo la Schleswig -Holstein amesema hivi karibuni kwamba chama chao cha SPD kisihangaike kumuweka mgombea kushindana na Merkel hapo mwaka 2017.Albig amekiambia kituo cha NDR TV kwamba mama huyo anafanya kazi nzuri kabisa.

Kulikuwa na tetesi miaka miwili iliopita kwamba Merkel atajiuzulu katikati ya muhula wake wa sasa lakini jambo hilo lilikanushwa na msemaji wake Steffen Seibert aliyesema Merkel ataamuwa juu ya muhula wa nne karinu na wakati wa uchaguzi unaotazamiwa kufanyika mwishoni mwa mwaka 2017.

Merkel alishinda muhula wake wa tatu hapo mwaka 2013 na baada ya mazungumzo yaliochukuwa wiki kadhaa aliunda serikali ya mseto na chama cha SPD.Katika muhula uliotangulia huo Merkel aliongoza serikali kwa ushirikano kati ya chama chake cha CDU;CSU na Freedom Demokratik (FDP).

Mwandishi : Mohamed Dahman/Reuters/AFP

Mhariri : Isaac Gamba

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com