1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel awaongoza viongozi wa nchi katika mkutano wa COP23

Caro Robi
15 Novemba 2017

Viongozi kadhaa wa dunia Jumatano (15.11.2017) wanawasili, mjini Bonn kuhudhuria mkutano wa kimataifa wa mazingira ili kuyapiga jeki mazungumzo kuhusu mabadiliko ya tabia nchi yatakayomalizika Ijumaa wiki hii.

https://p.dw.com/p/2nejy
Deutschland | Fortsetzung Sondierungsgespräche | Ankunft Angela Merkel
Picha: picture-alliance/dpa/M. Kappeler

Darubini sasa inamulikwa kwa Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayekabiliwa na shinikiko la kutangaza muda wa mwisho ambao nchi yake itakomesha matumizi ya nishati ya makaa ya mawe. Wanaharakati wa mazingira na nchi masikini zinamtaka Merkel kutumia mkutano huu wa kimataifa wa mazingira ujulikanao COP23 kutangaza kuwa Ujerumani itaondolea mbali nishati inayochafua vibaya mazingira ifikapo mwaka 2030.

Lakini huenda hilo lisiwe jambo rahisi kwa Merkel, kwani punde tu baada ya kuhutubia hapa Bonn kwa dakika 11 baadaye leo mchana, atarejea Berlin kwa ajili ya mazungumzo ya kuunda serikali mpya ya mseto yanayovijumuisha vyama vya kihafidhina Christian Democratic Union CDU na Christian Social Union CSU kwa upande mmoja na chama cha walinda mazingira cha kijani pamoja na chama cha kutetea mazingira rafiki ya kibiashara cha Free Domocrats FDP ambacho kinapinga kutolewa muda wa mwisho wa kuondolewa mbali matumizi ya makaa ya mawe.

Makaa ya mawe suala tete Ujerumani

Makaa ya mawe yanachangia asilimia 40 ya umeme Ujerumani na nchi hiyo haijaweza kupunguza gesi chafu ya Carbon kwa kipindi cha miaka nane iliyopita. Ujerumani imeahidi kupunguza gesi chafu inayotoka viwandani kwa asilimia 40 ifikapo mwaka 2020.

Niederaußem Kohlekraftwerk und Solarpanele
Kiwanda cha makaa ya mawe UjerumaniPicha: Getty Images/L. Schulze

Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron wanaonekana kuwa manahodha wa mchakato wa kuyalinda mazingira kuambatana na makubaliano yaliyofikiwa Paris mwaka 2015 yanayokusudia kupunguza viwango vya joto duniani hadi chini ya nyuzi mbili.

Viongozi hao wametwishwa jukumu hilo la kuuongoza ulimwengu kuhusu suala hilo la mazingira baada ya Rais wa Marekani Donald Trump mwezi Juni mwaka huu kutangaza kuwa nchi yake inajiondoa kutoka makubaliano hayo ya Paris.

Merkel na Macron manahodha wa mazingira

Armelle le Comte wa shirika la kimataifa la kutoa misaada ya kiutu la Oxfam amesema wanatarajia Merkel na Macron watakuwa mfano wa kuigwa kuhusu masuala ya kuyalinda na kuyahifadhi mazingira. Mtizamo unaoungwa mkono na Pierre Cannet mkuu wa mazingira na nishati wa shirika la ulinzi wa wanyama pori duniani WWF.

Belgien Brüssel EU-Gipfel
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais wa Ufaransa Emmanuel MacronPicha: Reuters/F. Lenoir

Wajumbe wa mkutano huo wa COP23 kwa siku tisa wamekuwa wakijadili ni namna gani makubaliano hayo ya Paris yatakavyotekelezwa na sasa mawaziri wa mazingira na nishati wa nchi takriban 196 watajaribu kuwianisha masuala tete kabla ya siku ya Ijumma kutoa msimamo wa pamoja kuhusu ni hatua zipi zimefikiwa na ni masuala gani bado yanahitaji kufanyiwa kazi.

Miongoni mwa masuala ambayo mawaziri wa mazingira watayashughulikia leo ni matakwa ya nchi masikini kupewa msaada wa kifedha kuweza kujiandaa kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabia nchi.

Mohamed Adow wa shirika lisilo la serikali la Action Aid linalowakilisha maslahi ya nchi maskini katika mazungumzo hayo ya COP23, amesema mkutano huo haujaweza kupiga hatua za tija kuhusu masuala makuu akiongeza anahisi wajumbe wanauchukulia mkutano huu wa mazingira kama fursa ya kuja likizo.

Viongozi wengine watakaohutubia leo katika mkutano huo wa COP23 ni Rais wa Ujerumani Frank Walter Steinmeier, Waziri mkuu wa Fiji Frank Binarimana na Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres.

Mwandishi: Caro Robi/afp/ap

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman