Merkel awaomba wanasiasa kuweka pembeni tofauti zao | Matukio ya Kisiasa | DW | 04.10.2021
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel awaomba wanasiasa kuweka pembeni tofauti zao

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel anayemaliza muda wake amewatolea mwito wanasiasa kumaliza tofauti zao wakati mazungumzo baina ya vyama ya kumsaka mrithi wake yakiendelea.

Tayari vyama vinne vikubwa vimefanya mazungumzo jana Jumapili, kujadili nafasi ya kila chama kabla ya kuamua hatua zaidi kuelekea kuunda serikali ya muungano. 

Soma Zaidi: FDP, Kijani wakutana kwa mazungumzo ya serikali ya mseto Ujerumani

Kansela Merkel akizungumza mbele ya viongozi wa vyama wakati wa kumbukumbu ya Ujerumani kuungana tena mnamo mwaka 1990 mjini Halle kwamba kwa mara nyingine taifa lilikuwa na fursa ya kuutengeneza mustakabali wake ujao.

"Ni kweli, lazima tuendelee kuitengeneza nchi yetu. Tunaweza kubishana juu ya namna gani siku za usoni zitakavyokuwa lakini tunajua kuwa jibu liko mikononi mwetu, kwamba ni lazima tusikilizane na kuzungumza na kila mmoja kwamba tuna tofauti, lakini pamoja na yote tuzingatie kwanza masuala ya msingi. " alisema Merkel.

Kommunalwahlkampf Nordrhein-Westfalen - Podiumsdiskussion

Olaf Scholz na chama chake cha SPD wanakabiliwa na kibarua kigumu cha mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano.

Chama cha siasa za wastani za mrengo wa kushoto cha Social Democrats, SPD kikiongozwa na mgombea wake Olaf Scholz kilishinda kwenye uchaguzi huo huku muungano wa kihafidhina wa CDU/CSU kuanguka vibaya wakati Kansela Merkel akijiandaa kuondoka madarakani baada ya miaka 16.

Soma Zaidi: Wajerumani wamtaka Laschet akae pembeni

Juhudi za kuunda serikali mpya zinaendelea, wakati chama kilichobeba turufu ya kuunda serikali cha kiliberali cha FDP kikisema ni lazima kishirikiane kwa karibu na chama cha Kijani, cha watetezi wa mazingira ili kuzuia kurejea kwa muungano huo wa kihafidhina na SPD.

Vyama vinne vikubwa pia tayari vimefanya mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano jana Jumapili huku kila kimoja kikijadiliana na mwenzake kabla ya kuchukua hatua zaidi. SPD hapo jana kilikutana kwanza na FDP kilichoshika nafasi ya nne kabla ya kuzungumza na chama cha Kijani, waliopata nafasi ya tatu.

Mazungumzo hayo ya Jumapili mjini Berlin, yanayoelezewa na baadhi ya wafuatiliaji ni kama ya kuharakisha makubaliano, yalihitimishwa na mkutano kati ya muungano FDP na muungano wa kihafidhina wa kansela Merkel. Pande zote zilisisitiza kwamba zilikuwa na mazungumzo mazuri lakini zikikataa kuzungumzia kwa kina ili kuepuka kuhujumu makubaliano hayo.

Hata hivyo, katibu mkuu wa chama cha FDP Volker Wissing alielezea umuhimu wa serikali kuundwa haraka na kuongeza kuwa kwa sasa wanasubiri matokeo ya mazungumzo kati ya chama cha Kijani na CDU/CSU kisha watatoa tathmini yao ya ndani.

Mashirika: APE/RTRE