1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel atafakari kuchukulia Uturuki hatua kali

Sekione Kitojo
2 Septemba 2017

Kansela  wa  Ujerumani Angela  Merkel ametoa  wito wa kutafakari upya mtazamo  wa serikali  ya Ujerumani  kuelekea  Uturuki baada ya nchi  hiyo kuwakamata raia  wawili  zaidi  wa  Ujerumani.

https://p.dw.com/p/2jFHS
Merkel MIT Business Treffen
Picha: Getty Images/J. Koch

 Uhusiano kati  ya  nchi  hizo  mbili umeporomoka tangu jaribio lililoshindwa  la mapinduzi mwaka 2016.

Hakuna "msingi wa  kisheria" wa kukamatwa  katika matukio  mengi, Merkel amesema , akielezea  kuhusu Wajerumani wawili waliokamatwa  siku  ya  Alhamis nchini  Uturuki, na  kufikisha  jumla ya idadi  ya  raia  wa Ujerumani  waliokamatwa  nchini  humo  kwa sababu  za  kisiasa  kuwa 12.

"Hii  ndio  sababu  tunahitaji kuchukua  hatua  muhimu  hapa," amesema , na  kuongeza  kwamba  serikali "huenda inapaswa kutafakari  upya" uhusiano  wake na  Uturuki.

Deutschland Peter Steudtner und Deniz Yücel
Deniz Yucel (kushoto) mwandishi habari raia wa Ujerumani mwenye asili ya UturukiPicha: picture-alliance/privat/K. Schindler

Merkel  amesema  Ujerumani  tayari, "imeendeleza  kwa  kiasi kikubwa " uhusiano wake  na  Uturuki, lakini  hatua   hii  mpya  ina maana "huenda  ni  muhimu  kutafakari  upya zaidi," na  kuongeza kwamba  kunaweza  kuwa  na  mazungumzo  zaidi  juu  ya  ushiriki wa  Ankara katika  Umoja  wa  forodha  wa  Umoja  wa  Ulaya  hadi pale  hali  ya  hivi  sasa  itakapotatuliwa.

"Madai yetu kwa  Uturuki yako  wazi  kabisa," msemaji  wa  serikali ya  Ujerumani  Steffen Seibert amesema. "Tunatarajia Uturuki itawaachia  huru  raia  wa  Ujerumani  ambao  wamekamatwa  kwa misingi isiyokuwa ya  kisheria."

Mahusiano baina  ya  washirika  hao  wa  NATO yamevurugika tangu  pale  serikali  ya  Ujerumani  ilipoikosoa  Uturuki  kuhusiana na  ukandamizaji  uliofuatia  jaribio la  mwaka  jana  lililoshindwa  la mapinduzi.

Kukamatwa Wajerumani

Kukamatwa  kwa  Wajerumani  wawili siku  ya  Alhamis  kunafikisha idadi  ya  watu  55, Wajerumani  waliokamatwa  nchini  Uturuki, 12 kati  yao  wanashikiliwa  kwa  sababu  za  kisiasa  na  wengine wanne wana uraia  pacha  wa  Ujerumani  na  Uturuki , ikiwa  ni pamoja  na  mwandishi  habari  mwenye  uraia  wa  Uturuki  na Ujerumani  Deniz Yucel, ambaye  yuko  kizuwizini  sasa  kwa  siku 200, imesema  wizara  ya  mambo  ya  kigeni  ya  Ujerumani.

Shirika  la  habari  la  Uturuki  linaloendeshwa  na  serikali Anadolu limeripoti  kwamba  raia  wawili  wa  Ujerumani  wenye  asili  ya Uturuki  wamekamatwa  katika  uwanja  wa  ndege  wa  Antalia kwa madai  ya  kuwa  na  uhusiano  na mtandao wa  imamu  anayeishi uhamishoni  nchini  Marekani Fethullah Gulen , ambaye  Ankara inamshutumu kwa  kutayarisha  jaribio  la  mapinduzi  lililoshindwa mwaka  jana.

Türkei | Erdogan am Atatürk-Mausoleum anlässlich der Feierlichkeiten zum 95. Jahrestag des großen Sieges
Kiongozi wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan Picha: Reuters/U. Bektas

Ujerumani  haijafahamishwa  rasmi kuhusiana  na  kukamatwa  kwa watu  hao  wawili, ambako  kulitokea katika  uwanja  wa  ndege  wa Antalia siku ya  Alhamis.

Ubalozi  mdogo wa  Ujerumani   katika  mji  wa  pwani  wa  Izmir ulifahamishwa  kuhusu kukamatwa  huko "na vyanzo  ambavyo  si vya  serikali," msemaji  wa  wizara  ya  mambo  ya  kigeni Maria Adebahr  aliwaambia  waandishi  habari.

"Tunajaribu  kujua  wanashitakiwa  kwa  madai  gani,"  amesema Adebahr. "Tunapaswa  kufikiria  kwamba  ni  madai  ya  kisiasa, shaka ya  ugaidi, kama  ilivyo  kwa  wengine."

Wanadiplomasia hawajaweza  kuwa na  mawasiliano  nao , ameongeza, sikukuu  ya  Ijumaa  ya  Kiislamu  ya  Eid al-Adha  ikiwa ni  sababu  mojawapo ya uchelewesho  wa  mawasiliano  na maafisa.

Mwandishi: Sekione Kitojo / rtre,ap,afp,dpa

Mhariri: Sudi Mnette