1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asikitishwa na mzozo kuhusu Maassen

Isaac Gamba
24 Septemba 2018

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema anasikitishwa na mzozo wa wiki iliyopita kuhusu mkuu wa shirika la ujasusi Hans Georg Maassen ambao umesababisha mivutano miongoni mwa washirika wa serikali ya mseto.

https://p.dw.com/p/35OAh
Deutschland Gremiensitzungen der Bundesparteien | Angela Merkel, Bundeskanzlerin
Picha: picture-alliance/dpa/B.v. Jutrczenka

Merkel amesema ni wakati sasa wa serikali yake kuachana na mivutano na kuangazia matatizo ya watu. Hapo jana viongozi walifikiana kuwa mkuu huyo wa zamani wa shirika la ujasusi Hans Georg Maassen atakuwa mshauri maalum katika wizara ya ndani.

Masuala ambayo Wajerumani wanataka kuiona serikali ni pamoja na kuongezeka kwa kodi za nyumba, malipo ya pensheni na sakata la magari yanayotumia mafuta ya Diesel.

Chama cha  siasa za wastani  za mrengo wa  kushoto Social Democratic-SPD kilikuwa  kikisisitiza kwamba  Maassen afutwe kazi kwa kushindwa kuwajibika  kuhusiana na  machafuko ya hivi  karibuni dhidi ya wahamiaji.

Sakata hilo lilipamba moto baada ya Waziri wa ndani na kiongozi wa chama cha Christian Social union-CSU Horst Seehofer kusimama kidete kumuunga mkono na kumtetea Maassen.

Mnamo wiki iliopita , Serikali hiyo inayoongozwa na Kansela Angela Merkel kutoka chama cha Christian Democratic Union-CDU, ilikubaliana  kumuondoa  Maassen katika wadhifa wake na  kuteuliwa kuwa waziri mdogo wa ndani,  hatua ambayo ilikuwa ni kumpandisha cheo na mshahara zaidi.

 Hatua hiyo ilizusha  mtafaruku ndani ya chama cha SPD na kumlazimisha kiongozi wa chama hicho Andreas Nahles  kutaka maafikiano hayo yajadiliwe upya.

Kutokana na mgogoro huo mpya, hatimaye pande hizo tatu CDU-CSU na SPD zikakubaliana kuwa Maassen apewe wadhifa mwengine na akateuliwa kuwa mshauri katika wizara ya ndani akiwa na jukumu la kushughulikia  masuala ya Ulaya na kimataifa, huku Waziri wa ndani Seehofer akisema afisa huyo atabakia  na mshahara wake  ule ule  wa zamani.

Kutokana na maridhiano hayo, waziri mdogo wa  ndani  Gunther Adler kutoka chama cha SPD atabakia katika wadhifa wake huo. Hivi sasa kiongozi wa chama hicho Nahles  atalazimika  kuwasilisha maridhiano hayo mapya mbele ya chama chake  ili  yaidhinishwe.

SPD wasema ni suluhisho muafaka

Naibu mkuu  wa SPD Ralf Stegner  alisema  uamuzi uliofikiwa ni " suluhisho muwafaka.”

CDU na chama ndugu CSU, vimekuwa vikivutana hivi karibuni kuhusiana na  suala la wahamiaji huku seehofer aliyeacha uongozi wa chama chake CSU ili kuwa waziri wa ndani akiwa na msimamo mkali kuhusu suala hilo.

Hans-Georg Maaßen
Hans-Georg Maassen , Aliyekuwa mkuu wa shirika la ujasusi wa ndani nchini Ujerumani.Picha: Getty Images/S. Gallup

Kisa cha Maassen kilianzia  pale aliposema idara yake haikuwa na ushahidi wa kutosha kuwa wageni walikuwa wakiandamwa mitaani mjini Chemnitz baada ya  mjerumani mmoja kuchomwa kisu na kuuwawa na  mtu anayetuhumiwa kuwa ni mhamiaji, wakati  ukanda wa video uliochapishwa kwenye mitandao ulionesha wazi wafuasi wa siasa kali za mrengo wa kulia wakiwaandama na kuwashambulia wageni mjini humo.

Mgogoro huo umegeuka mtihani kwa  mustakbali wa serikali ya muungano ya Kansela Merkel katika wakati ambao  vyama hivyo vitatu vinavyounda serikali hiyo, vikikabiliwa na changamoto mpya kuelekea uchaguzi wa jimbo la Bavaria wa Waziri wa ndani Seehofer Oktoba 14 na katika jimbo jirani la Hesse Oktoba 28.

Mivutano ya ndani inaelekea kudhoofisha uungaji mkono wa vyama hivyo, tokea uchaguzi mkuu wa Ujerumani mwaka mmoja uliopita , ambapo chama cha siasa kali za kizalendo za mrengo wa kulia AFD kilifanikiwa kuingia bungeni na kugeuka kuwa  changamoto kubwa kwa vyama hivyo asilia.

Kuna wasiwasi mkubwa kwamba matokeo mabaya kwa CSU jimboni Bavaria katika uchaguzi huo mwezi ujao yanaweza kuwa kitisho kwa mustakabali wa serikali hiyo ya muungano.

Mwandishi. Isaac Gamba/ AP, Reuters

Mhariri: Caro Robi