Merkel asema EU hainuii kuibana Urusi | Matukio ya Kisiasa | DW | 21.05.2015
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel asema EU hainuii kuibana Urusi

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema ushirikiano kati ya Umoja wa Ulaya na nchi za Ulaya Mashariki ambazo awali zilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti, sio mpango wa sera ya kuupanua Umoja wa Ulaya.

Bi Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani

Bi Angela Merkel, Kansela wa Ujerumani

Katika hotuba yake kwenye bunge la Ujerumani mjini Berlin leo kabla ya mkutano wa Umoja wa Ulaya na nchi hizo za Ulaya Mashariki, Bi Merkel amesema Ulaya haipaswi kuweka matumaini ya uongo ambayo haiwezi kuyatekeleza.

Hotuba hiyo ya Kansela Angela Merkel imetolewa muda mfupi kabla ya kuanza kwa mkutano kati ya Umoja wa Ulaya wenye nchi 28 wanachama, na nchi sita za Ulaya ya Mashariki ambazo zilikuwa katika Umoja wa Jamhuri za Kisovieti, ambazo ni Ukraine, Belarus, Georgia, Armenia, Azerbaijan na Moldova. Mkutano huo unaanza leo katika mji mkuu wa Latvia, Riga.

Katika hotuba yake bungeni Bi Merkel amezungumza kuhusu mkutano wa kundi la nchi 7 zilizoendelea zaidi kiviwanda au G-7, ambalo kabla ya kupanuka kwa mzozo wa kisiasa na kivita nchini Ukraine lilikuwa likijumuisha Urusi.

Urusi kubaki nje ya G-7

Hatua ya Urusi kulichukua eneo la Ukraine la Crimea lilifuatia mvutano kuhusu ushirika kati ya EU nchi za Ulaya Mashariki

Hatua ya Urusi kulichukua eneo la Ukraine la Crimea lilifuatia mvutano kuhusu ushirika kati ya EU nchi za Ulaya Mashariki

Merkel amesema haifikiriki kwamba Urusi itakaribishwa katika kundi hilo, wakati wote nchi hiyo itakapokaidi kuheshimu misingi ya demokrasia na utawala wa sheria. Urusi ilifukuzwa katika kundi hilo baada ya kulitwaa eneo la Crimea kutoka Ukraine, hatua ambayo bi Merkel amesema ni kinyume cha maadili ya kundi hilo.

''Tunalichukulia kundi la G-7 kama jumuiya ya kimaadili, ambayo inashirikiana kuendeleza uhuru, demokrasia na utawala wa sheria. Maana yake ni kuheshimu sheria na mipaka ya nchi nyingine. Hatua ya Urusi kuhusu Ukraine ni kinyume cha maadili hayo.'' Amesema Merkel.

Hata hivyo, katika mkutano unaoanza leo kati ya Umoja wa Ulaya na nchi zilikuwa sehemu ya Umoja wa Kisovieti, Ulaya itakuwa makini kutoikasirisha Urusi. Katika mkutano uliopita wa aina hiyo mwaka mmoja na nusu uliopita, aliyekuwa rais wa Ukraine Viktor Yanukovich alikataa kusaini makubaliano ya ushirikiano kati ya nchi yake na Umoja wa Ulaya, hali iliyoibua mvutano mkali kati ya viongozi wa Ulaya na rais wa Urusi, Vladimir Putin.

Shari ya kuipuuza Urusi

Mawazizi wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya mjini Riga

Mawazizi wa mambo ya nchi za nje wa Umoja wa Ulaya mjini Riga

Viongozi wa Ulaya, wakiwemo Kansela Angela Merkel wa Ujerumani na rais wa Ufaransa Francois Hollande watafanya majadiliano na nchi sita za Ulaya ya mashariki. Ingawa rais Putin hatakuwepo katika mkutano huo, anatarajiwa kuwa mada kubwa ya mazungumzo.

Na tayari, kabla ya mkutano huo wa mjini Riga, Urusi imekwisha bainisha msimamo wake. Waziri wa mambo ya nchi za nje wa nchi hiyo, Sergei Lavrov ameliambia baraza la seneti mjini Moscow, kwamba, ''Hatuchukulii hatua ya majirani zetu kuimarisha ushirikiano na Umoja wa Ulaya kuwa jambo la hatari, lakini kuufanya mchakato huo uwe wenye tija, wanapaswa kuepuka kuyahujumu maslahi ya Urusi''.

Na tangu mkutano ule wa mwaka mmoja na nusu uliopita, nchi za Ulaya ya Mashariki zinazoegemea upande wa Umoja wa Ulaya, zimekwishaonja shari inyotokana na kuipa kisogo Urusi.

Mwandishi:Daniel Gakuba/ape/rtre/afpe

Mhariri: Iddi Ssessanga

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com