Merkel apata upinzani mashariki mwa Ujerumani | Uchaguzi wa Ujerumani 2017 | DW | 13.09.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

UJERUMANI YAAMUA

Merkel apata upinzani mashariki mwa Ujerumani

Ikiwa ni chini ya wiki mbili tu hadi tarehe ya uchaguzi mkuu wa Ujerumani unaofanyika tarehe 24 Septemba, Kansela Angela Merkel anaonekana kupata upinzani mkali kwenye upande anaotokea mwenyewe - mashariki.

Njiani kuelekea Köthen tukitoka mji mkuu Berlin kupitia Bitterfeld, ilikuwa dhahiri kwamba tofauti na maeneo ya magharibi mwa Ujerumani, mabango yanayomuonesha Kansela Angela Merkel anayepigiwa upatu kushinda uchaguzi huu, ni nadra sana kuyaona.

Hapa mashariki mwa Ujerumani, ambako ndiko anakotoka kansela huyo, umaarufu wake ulishuka sana mnamo miaka miwili iliyopita, kutokana na sera yake ya kufungua milango kwa wakimbizi.

Pigo kubwa alilolipata lilikuwa katika mji wa Bitterfeld katika eneo hili, ambako chama cha Christian Democratic (CDU) kilipigwa kikumbo na chama chenye misimamo mikali ya kizalendo kijiitacho Mbadala kwa Ujerumani (AfD) katika uchaguzi wa bunge mapema mwaka huu.

Lakini sasa, kulingana na maoni ya watu ambao tumewakuta katika hadhara hii ya chama cha Die Linke, ambayo ilihutubiwa na kiongozi wake maarufu, Gregor Gysi, ni kwamba chama cha AfD mara hii hakitafua dafu.

Mecklenburg-Vorpommern Strasburg Angela Merkel Wahlkampf (Reuters/F. Bensch)

Merkel analenga kuongoza kwa muhula wa nne.

Gysi mwenyewe, ambaye ni mbunge katika bunge la shirikisho, alisema katika mkutano huo, kwamba inachopaswa kukifanya Ujerumani katika kupambana na tatizo la wakimbizi, ni kupinga mizozo inayosababisha watu kukimbia.

"Mtazamo wangu ni kwamba ni bora kuzuia mizozo inayosababisha vita. Kwa mfano, katika vita vinavyoongozwa na Saudi Arabia nchini Yemen, wakimbizi watakuja hapa Ujerumani. Ujerumani ni miongoni mwa wasambazaji wa silaha zinazotumika katika vita hivyo. Je, baada ya mzozo wa wakimbizi wa mwaka 2015, isingekuwa uamuzi mzuri kusitisha mauzo ya silaha kwa nchi hizo?"

Gysi ambaye anafahamika kwa misiamamo yake ya kupinga vikwazo dhidi ya Urusi, alisema serikali ijayo ya Ujerumani inapaswa kujikita katika kuepusha mizozo duniani badala ya kuhusika kuisababisha.

Wazee wengi wanampinga Merkel

Wengi katika mkutano huu walikuwa watu wa makamo ambao bila shaka ni wafuasi wa chama hiki tangu wakati sehemu iliyokuwa Ujerumani Mashariki ilipokuwa chini ya ushawishi wa iliyokuwa Umoja wa Kisovieti. Lakini pia walikuwepo vijana, ambao waliiambia DW, kwamba bado wanaamini kuwa chama hiki ndicho bora kwa maslahi ya wafanyakazi.

Deutschland Wahlplakat der Partei Die Linke in Bonn (DW/I. Sheiko)

Die Linke wana umaarufu mkubwa mashariki mwa Ujerumani.

Mmoja wa watu waliozungumza na DW, Jürgen Gewinner, mbunge wa chama cha Die Linke kutoka eneo hilo, alisema madai ya chama cha AfD ya kuwachukulia wakimbizi kama kisingizio hayana mashiko tena, akisema kwa maoni yake, sera za chama hicho ndio tatizo.

"Tatizo katika uchaguzi huu, au kinachokasirisha, sio wakimbizi, ni siasa kali za kizalendo, za mrengo wa kulia, wanaotaka kurudisha siasa za kinazi za mwaka 1993. Sio jambo zuri. Wakimbizi? Tafadhali sana. Sisi watu wa mashariki tuliwahi pia kuwa wakimbizi, na tunapaswa kupinga chuki dhidi ya wakimbizi".

Licha ya msimamo wake huo, lakini wakaazi wengi wa maeneo haya ya mashariki mwa Ujerumani, wana malalamiko ya hali ya kiuchumi, ambayo imedorora ikilinganishwa na ya sehemu za magharibi mwa nchi.

Kutokana na uhaba wa ajira, vijana wengi wanayahama maeneo haya, wakitafuta neema katika miji mikubwa yenye makampuni makubwa na ajira za viwandani.

Adha hii inatosha kuwafanya baadhi ya watu kuwa na dhana kuwa wakimbizi na wahamiaji, watakuwa washindani kwenye soko la ajira.

Mwandishi: Daniel Gakuba
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Sikiliza Matangazo Yetu

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com