Merkel alegeza msimamo kuhusu ndoa za jinsia moja | Matukio ya Kisiasa | DW | 27.06.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Merkel alegeza msimamo kuhusu ndoa za jinsia moja

Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel sasa anaonekana kulegeza msimamo wake dhidi ya ndoa ya watu wa jinsia moja  ambayo imeruhusiwa katika takriban nchi 20 duniani kote, 13 miongoni mwao zikiwa Barani Ulaya

Mnamo mwezi Aprili mwaka 2001, Uholanzi  lilikuwa taifa la kwanza duniani kuruhusu ndoa za wapenzi wa jinsia moja. Nchi 12 za Ulaya zilifuatia ambazo ni Ubelgiji, Uingereza, ukiiondoa Ireland ya Kaskazini, Denmark, Ufaransa, Iceland, Ireland, Luxembourg, Norway, Ureno, Hispania na Sweden.  

Kansela Angela Merkel ameulegeza msimamo wake huo wa kupinga ndoa za jinsia moja na hivyo kuyapa makundi ya mashoga na wasagaji sababu ya kusherehekea wakati akivinyima vyama vya upinzani suala muhimu la kufanyia kampeni ikiwa imesalia miezi mitatu kabla ya uchaguzi.

Merkel amesema anakaribisha kura kuhusu suala hilo ambapo wabunge wataruhusiwa kuweka kando msimamo wa chama, na kuamua kibinafsi mageuzi ambayo yanaonekana yatapitishwa bila ya shaka.

Hapo kabla kiongozi huyo wa chama cha sera za wastani za mrengo wa kulia christian Democratic Union-CDU mara kwa mara alieleza maoni yake binafsi kuhusu haki za ndoa za mashoga, ikiwa ni pamoja na suala la kuasili watoto kwa wapenzi wa jinsia moja, akihoji  hasa juu ya  mustakbali na  matunzo bora ya watoto hao.

Merkel akabiliwa na shinikizo kubwa kuhusu sheria itakayoruhusu ndoa za jinsia moja.

Hatua ya kubadili msimamo ya  Merkel inakuja wakati ambapo utafiti wqa maoni unaonesha kuwepo kwa idadi kubwa ya wapiga kura wa Ujerumani na katika  vyama vingine vikuu wakiunga mkono kuruhusiwa kwa ndoa za jinsia moja. 

EU-Parlamentspräsident Martin Schulz in der Knesset (picture-alliance/AP)

Mpinzani mkuu wa Merkel, Martin Schulz wa SPD anayesema ataingilia kati iwapo CDU na CSU watashindwa kuandaa sheria

Mpinzani mkuu wa Merkel katika uchaguzi wa mwezi Septemba Martin Schulz leo hii amesema chama chake kitashinikiza  kupigwa kwa kura ya bunge kuhusu suala hilo.

Mgombea huyo kupitia chama cha Social Democrats, SPD hata hivyo hakusema wazi ni lini chama chake kitawasilisha muswada wa sheria kuhusu usawa katika ndoa katika bunge la Ujerumani, Bundestag. Hii ni wiki ya mwisho kwa vikao vya bunge lililopo sasa.

Schulz amesema, ana imani chama cha Merkel cha CDU na chama ndugu cha Christian Social Union, CSU chenye makao yake jimbo la Bavaria, vitashirikiana katika kutengeneza sheria, la sivyo SPD kitaingilia kati na kujadili nini cha kufanya katika mkutano utakaofanyika jumanne mchana.

Hata hivyo, CSU bado kinapinga kukubaliwa kwa ndoa za jinsia moja, ingawa kiongozi wa chama hicho amesema wabunge wake watakuwa huru kupiga kura, iwapo suala hilo litafikishwa bungeni.

Mbunge wa CDU Stefan Kaufmann ameandika kupitia ukurasa wake wa twitter akisema "asante Angela Merkel! ni uhuru mkubwa. Kama ingekuwa ni juu yangu, tungepiga kura wiki hii!. Mkuu wa taasisi ya serikali ya kupinga ubaguzi, Christina Lueders naye amesema, wapenzi wa jinsia moja hawafai kuendelea kusubiri kwa muda mrefu kabla ya kufikiwa maamuzi.

CDU na CSU mara kwa mara wamezuia harakati za kuanzishwa kwa usawa kamili wa ndoa kwa wapenzi wa jinsia moja nchini Ujerumani. Kulingana na takwimu za taasisi hiyo ya serikali ya kupinga ubaguzi, asilimia 83 ya Wajerumani wanaunga mkono ndoa za jinsia moja.

Mwandishi: Lilian Mtono/afpe/dpae
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com