Merkel akutana na Sarkozy mjini Paris | Matukio ya Kisiasa | DW | 09.01.2009
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Kisiasa

Merkel akutana na Sarkozy mjini Paris

Wajadili kuyumba kwa uchumi na hatima ya ubepari

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy (kulia) na kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy (kulia) na kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy wamekubaliana kushirikiana kukabiliana na kuondokana na mzozo mkubwa wa kiuchumi. Viongozi hao walikutana jana kwenye mkutano wa kimataifa uliojadili njia za kufanya mageuzi katika masoko ya fedha uliofanyika jana mjini Paris nchini Ufaransa.

Ulikuwa mkutano wa mara mbili kwa kansela wa Ujerumani Angela Merkel huko mjini Paris. Asubuhi ulikuwa wakati wa kuwasilisha mawazo na mchana kujadiliana kuhusu siasa za kila siku na rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy. Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair alihudhuria pia mkutano huo.

Viongozi hao watatu walitoa hotuba kwenye ufunguzi wa mkutano huo na walikuwa na msimamo mmoja kwamba miungano kama jumuiya ya nchi saba zilizoendelea kiviwanda duniani, G7, zimenusurika kutokana na mzozo wa kiuchumi. Ndio maana kansela wa Ujerumani Angela Merkel anapendekeza kuundwe baraza la uchumi la Umoja wa Mataifa.

''Tumeamua mbali na baraza la usalama la Umoja wa Mataifa kuundwe baraza la kiuchumi la Umoja wa Mataifa.''

Rais wa Ufaransa Nicholas Sarkozy aliukosoa ubepari, mabenki na walanguzi lakini hata hivyo muda mfupi baadaye akautetea ubepari akipendekeza kuundwe sheria mpya. Pendekezo hili pia limetolewa na waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ambaye mara kwa mara kwenye mkutano huo alihutubia kwa lugha ya kiingereza na kifaransa.

''Kitu ambacho bado kinadhihirishwa wazi na kuyumba huku kwa uchumi ni kwamba ni muhimu kuwa na uadilifu ili uchumi uendelee bila matatizo.''

Mapendekezo haya yatafuatiliwa na Ujerumani na Ufaransa ili kuandaa mkutano wa kilele wa nchi 20 zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia haraka kiuchumi duniani. Mkutano wa viongozi wa serikali utakaojadili hatua za kuchukua kuhakikisha uchumi hautumbukii kwenye matatizo kama sasa unapangwa kufanyika mjini Berlin hapa Ujerumani.

Mbali na swala la uchumi kansela Merkel na rais Sarkozy walijadiliana juu ya mzozo wa Mashariki ya Kati ambapo viongozi hao wawili wanataka kuisadia Misri kuulinda mpaka kati yake na Ukanda wa Gaza ili kuzuia uingizwaji silaha.

Viongozi hao pia walikuwa na msimamo mmoja kuhusu kumalizwa kwa mzozo wa gesi kati ya Urusi na Ukraine. Bi Merkel na rais Sarkozy wamependekeza kuwe na ushirikiano katika utafiti kati ya Ujerumani na Ufaransa.

Mtizamo kwamba serikali ya Ujerumani ndiyo yenye jukumu la kusuka mipango na kisha kansela Merkel aende Paris kumfahamisha rais Sarkozy ulijitokeza kwenye mkutano uliofanyika mwaka jana kati ya viongozi hao wawili. Rais Sarkozy alisema wakati huo, ''Angela Merkel analishughulikia. Nitalifikiria.''

Lakini kwenye mkutano wa jana rais Sarkozy alimuomba radhi kansela Merkel akiyaeleza matamshi kuwa yasiyo ya kidiplomasia. Wakati huu rais Sarkozy amempongeza kansela Merkel hususan kuhusu wazo la Ujerumani kutoa mikopo kwa kampuni.

''Naliona kuwa wazo zuri kabisa. Tulikuwa tayari tunalifikiria. Sasa tutaharakisha na baadaye tufanye kama Ujerumani.''

Rais Sarkozy akiuongoza mkutano huo wa siku mbili mjini Paris kuhusu hatma ya ubepari amesema hakuna nchi inayoweza kuunda sera ya kiuchumi bila kushirikisha nchi nyingine.

 • Tarehe 09.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/ Johannes Duchrow
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GV2K
 • Tarehe 09.01.2009
 • Mwandishi Charo Josephat/ Johannes Duchrow
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/GV2K
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com