1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aionya Urusi

Admin.WagnerD13 Machi 2014

Ujerumani imesema ikiwa Urusi itaendelea na msimamo wake katika mgogoro wa Ukraine, kutakuwa na janga kubwa sio tu kwa taifa hilo bali hata kwa Umoja wa Ulaya na Urusi yenyewe.

https://p.dw.com/p/1BOyx
Angela Merkel Regierungserklärung zur Ukraine 13.03.2014
Picha: Odd Andersen/AFP/Getty Images

Hii inaelezwa kuwa ni kauli kali kabisa kutolewa na kiongozi huyo tangu kuanza kwa mgogoro wa Ukraine. Sudi Mnette anaarufu zaidi.

Kansela Angela Merkel ameyasema wakati akilihutubia bunge la Ujerumani. Akielezea zaidi amesema Urusi haisaidii katika kuleta utulivu Ukraine, taifa ambalo linamuingiliano wa karibu wa kiuchumi na kiutamadanuni badala yake inaonekana kupata faida kutokana na udhaifu wa Ukraine. Hali ilivyo sasa inaonekana kama mchezo wa mwenye nguvu kuwa mwenywe haki.

Maslahi ya Urusi kwa Ukraine

Markel alisema Urusi inaweka mbele faida zake za kisiasa kuliko kujenga ushirikiano mzuri katika maridhiano. Aidha amesema kuendelea na mipango yake ya kuihodhi Crimea, taifa hilo litajiweka katika athari za kiuchumi na kisiasa. Alisema Urusi inaendelea na mikakati yake kwa kutumia mbinu za karne ya 19 na 20 ambapo kwa kufanya hivyo inavunja sheria za kimataifa.

Ukraine Russland Krim-Krise 06.03.2014
Eneo la mgogoro la Crimea 06.03.2014Picha: Getty Images

Kufuatia mtazamo huo Kansela alisema haikubaliki, na ikibidi umoja wa Ulaya utatumia kiwango cha tatu cha kuliwekea vikwazo taifa hilo vikilenga uchumi. Hata hivyo amesema kuingilia kijeshi sio suluhu ya kutatua mgogoro wa Ukraine.

Msimamo wa Ulaya kuhusu uliokuwa umoja wa Kisovieti

Amesema Ulaya ipo tayari kusimama pamoja na maeneo yalikuwa katika himaya ya kisovieti katika kudhibiti kile kinachoonekana kama uwezekano wa kutokea ukandamiziji wa Urusi. Katika taarifa yake hiyo mbele ya Bunge Merkel amesema iwe Moldova au Georgia watawaonesha umoja wao.

Kama ilivyo kwa Ukraine, Moldova ipo katika shinikizo la Urusi la kutelekeza makubaliano ya ushirikiano na Umoja wa Ulaya. Urusi iliingia vitani na Georgia 2008 kutokana maeneo yanayojitenga ya Abkhazia na Ossetia Kusini.

Aidha akitoa matamshi kuhusu Ukraine yenyewe, ametoa ahadi ya kusaidia kuleta utulivu na kufanikisha mabadiliko ya kisiasa.

Jeshi la Urusi limeendelea kuwepo karibu na mpaka mpaka wa mashariki wa taifa hilo na Ukraine. Kiasi cha wanajeshi 4,000 wa miamvuli, ndege 36 na magari 500 yenye silaha yakipiga doria katika mikoa minne ambapo mitatu kati ya hiyo inapakana na Ukraine.

Mwandishi: Sudi Mnette DPA
Mhariri:Yusuf Saumu