1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel ahutubia Bunge la Israel

Mwakideu, Alex18 Machi 2008

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amepokea mwaliko wa heshima katika bunge la Israel Knesset katika siku yake ya mwisho ya ziara yake nchini humo

https://p.dw.com/p/DQlk
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel aweka shada la maua kwa sehemu ya ukumbusho ya wayahudi waliouwawa na Ujerumani wakati wa vita vya piliPicha: AP

Mapema Kiongozi huyo wa Ujerumani alikutana na Rais wa Israel Shimon Peres, kiongozi wa upinzani Benjamin Netanyahu na waziri wa nchi za nje Tzipi Livni.


Kabla ya kuingia katika bunge la Knesset, Kansela Merkel amepewa fursa ya kulikagua gwaride lililokuwa nje ya bunge hilo.


Baadaye Merkel alikaribishwa bungeni Israel na spika wa bunge hilo Dalia Itzik. Huku akiwa anakanyaga zulia jekundu nyimbo za taifa za nchi hizo mbili zilipigwa kwa heshima yake.


Mapema Kansela Merkel na Rais wa Israel Shimon Peres walipongeza uhusiano bora kati ya nchi hizo mbili; miongo sita baada ya mauaji ya kuwaangamiza wayahudi yaliyotekelezwa na Ujerumani.


Wananchi wa Israel wameikaribisha ziara ya Merkel; Jambo linaloashiria kwamba nchi hizo mbili zinaingia katika uhusiano bora zaidi.


Waziri wa mambo ya nje wa Israel amemwambia Kansela Merkel kwamba nia ya nchi hiyo katika ukanda wa Gaza sio tu kumaliza mashambulio ya roketi kutoka kwa eneo hilo hadi katika maeneo ya kusini mwa Israel bali pia kuzuia uwezo wa kuundwa kwa kundi la kigaidi katika mpaka wa Gaza na Israel.


Waziri huyo ameongezea kwamba Israel itaendelea na vita vyake dhidi ya wanamgambo wanaoishambulia kutoka Gaza na pia haitaacha mazungumzo ya upatanishi yanayoshirikisha serikali ya Rais wa Palestina Mahmoud Abbas.


Mapema alipokutana na Rais wa Israel, Merkel alijadili kuhusu uhusiano wa kichumi kati ya Palestina na Israel akitumai kwamba hatua hiyo italeta amani.


Kiongozi huyo wa Ujerumani ameahidi kusimamia ujenzi wa sehemu ya biashara katika jiji lililoko kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi la Jenin. Ujenzi wa eneo hilo ulikuwa umekwama kwa miaka kadhaa.


Kwa upande wake Rais Peres amesema miradi ya uchumi huenda ikasaidia katika mpango wa amani ya Mashariki ya Kati na pia kuwatia imani wapalestina.


Vile vile ametoa wito kwa ulaya na Marekani kuungana pamoja na kuzuia mpango wa nyuklia wa Iran huku akiongezea kwamba pato la mafuta la Iran linatumiwa kuendeleza ugaidi duniani ukiwemo ule wa Hamas katika ukanda wa Gaza na Hezbollah huko Lebanon.


Merkel ambaye ni mwanademokrasia wa kikristo alitarajiwa kujadili hali ya wakristo nchini Israel pamoja viongozi wa makanisa wa Ujerumani walioko mjini Jerusalem.


Kilele cha ziara yake nchini Israel ambayo inajumlisha maadhimisho ya miaka sitini ya nchi hiyo ni hotuba aliyotoa katika bunge la Israel Knesset leo jioni kwa lugha ya kijerumani.


Merkel ataingia katika vitabu vya historia kama mmoja wa viongozi wachache wa serikali za nje waliohutubia bunge la Israel.


Hata hivyo wabunge watano walitangaza awali kwamba watasusia hotuba yake katika bunge hilo lenye wanasheria 120.


Mmoja wao ni Shelly Yachimovich mwanachama wa muungano wa chama cha Labour ambaye amesema hotuba hiyo itakayotolewa kwa lugha ya kijerumani itazua hisia kali kwa manusura wa maangamizi ya wayahudi yaliyotekelezwa na Ujerumani wakati wa vita vya dunia vya pili.


Yachimovich ambaye ni binti ya mmoja wa manusura wa mauaji hayo amesema Ujerumani ni marafiki wa Israel lakini kuna umuhimu wa kutilia maanani hisia za watu hao.


Wabunge wawili kutoka chama cha upinzani chenye siasa kali cha Likud pamoja na wengine wawili kutoka chama cha kidini cha National Union wameunga mkono matamko ya Yachimovich.


Watatu kati yao wamesema watasusia kabisa hotuba hiyo huku mmoja Arieh Eldad wa National Union akiahidi kuondoka bungeni mwanzoni mwa hotuba hiyo kama ishara ya kupinga utumizi wa lugha ya kijerumani katika bunge la Knesset.


Mwanachama mwenzake Yitzhal Levy ameambia vyombo vya habari kwamba licha ya Ujerumani kuonesha uhusiano mzuri na Israel Wayahudi wangali wanakumbuka yaliyojiri wakati wa vita vya dunia vya pili.


Hata hivyo mbunge mwengine mwenye miaka 73 ambaye ni nusura wa vita hivyo amesema mpango huo wa kususia hotuba ya Merkel ni njia ya kujitafutia umaarufu kwani yeye mwenyewe haoni ubaya wowote wa Kiongozi huyo wa Ujerumani kuhutubia kwa lugha anayoilewa zaidi.


Mwenzake kutoka chama cha Labour ambaye ni mwanaye nusura wa Holocaust Ophir Pines ameshutumu mpango huo akiutaja kama njia ya kuzua uhasama.


Israel na Ujerumani zilirejesha uhusiano wake mwaka wa 1965 baada ya miaka kadhaa ya mazungumzo ya upatanishi. Kwa sasa Israel imeithamini Ujerumani kama nchi yenye uhusiano mzuri zaidi nayo katika bara ulaya.


Hapo jana nchi hizo mbili ziliongeza zaidi uhusiano wake kwa kutia sahihi mkataba wa kushirikiana katika maswala ya kijeshi, tamaduni, siasa na uchumi.


Mkataba huo ulitiwa sahihi katika kikao cha kwanza kabisa kilichoshuhudia mawaziri kutoka nchi hizo mbili wakihudhuria wakiwemo Merkel na waziri mkuu Ehud Olmert.