1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel aendelea na ziara yake Abu Dhabi

Josephat Nyiro Charo25 Mei 2010

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametiliana saini mikataba ya kibiashara na Abu Dhabi, kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya nchi nne za eneo la Ghuba, iliyoanza hapo jana

https://p.dw.com/p/NW3R
Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiwasili Abu Dhabi, Falme za Kiarabu, akilakiwa na waziri wa biashara, Sultan bin Saeed MansouriPicha: picture-alliance/dpa

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel ametiliana saini mikataba ya kibiashara na Abu Dhabi, kituo chake cha kwanza cha ziara yake ya nchi nne za eneo la Ghuba, iliyoanza hapo jana. Bi Merkel ameahidi kwamba Ujerumani iko tayari kufadhili miradi ya nishati inayoweza kutumiwa tena na tena katika Falme za Kiarabu. Josephat Charo na maelezo zaidi.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel amesema nchi za Ghuba zinaunga mkono juhudi za Ulaya kuimarisha sarafu ya euro. Kiongozi huyo ameyasema hayo hii leo huko Abu Dhabi baada ya kukutana na viongozi wa Falme za Kiarabu.

Alipoulizwa iwapo mfumo wa kuwa na sarafu moja barani Ulaya unaweza kuwa mfano kwa mataifa ya Ghuba kuunda sarafu yao, kansela Merkel amesema ndio inawezekana na kuongeza kwamba swala hilo amelipa kipaumbela katika mazungumzo yake. Katika siku za hivi karibuni sarafu ya euro imekabiliwa na msukosuko kutokana na mzozo wa deni la Ugiriki huku wawekezaji wakiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu uimara wa sarafu hiyo.

Kansela Merkel amesema Ujerumani inahitaji kuongeza shughuli zake za kibiashara katika Falme za Kiarabu ili iweze kushindana na mataifa mengine, hususan ya Asia.

Wakati huo huo, kansela Merkel amesema nchi za Ghuba zina wasiwasi kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, kama vile nchi za magharibi. Amesema viongozi wa Falme za Kiarabu wanataka kuona Iran ambayo haijaribu kutengeneza silaha zanyuklia.

Kansela Merkel aliwasili jana Abu Dhabi na kusaini bila kuchelewa mikataba kadhaa ukiwemo mkataba wa ushirikiano katika sekta ya nishati. Bi Merkel alikutana na mwanamfalme wa Abu Dhabi, Sheikh Mohammed bin Zayed al Nahayan. Sheikh Mohammed, amesisitiza kwamba jumuiya ya falme za kiarabu iko tayari kuendeleza ushirikiano wake wa kimkakati na Ujerumani.

Miongoni mwa mada kuu zilizotawala mazungumzo baina ya kansela Merkel na Sheikh Mohammed ni mchakato wa kutafuta amani ya Mashariki ya Kati pamoja na masuala mengine ya kimataifa na ya kanda hiyo.

Kansela Merkel amenukuliwa akimuhakikishia mwanamfalme Sheikh Mohammed kwamba Ujerumani iko tayari kutoa misaada kwa ajili ya miradi ya nishati inayoweza kutumika tena na tena katika famle za kiarabu. Ni kutokana na msingi huo ambapo kansela Merkel alikutana jana na waziri wa elimu ya juu na utafiti wa kisayansi, Sheikh Nahayan bin Mubarak al-Nahayan.

Baada ya mazungumzo hayo viongozi hao walitiliana saini mikataba kadhaa, ukiwemo mkataba wa kuinunua kampuni ya vifaa vya umeme ya Siemens ya Abu Dhabi kwa gharama ya dola bilioni 203. Pia walisaini makubaliano ya ushirikiano katika kutafuta na kuendeleza vituo vya mafuta na gesi. Mkataba mwingine uliosainiwa kati ya Ujerumani na famle za kiarabu unaziwezesha kampuni za Ujerumani kufanyia matengenezo vituo vya kutengenzea gesi asili.

Kansela Merkel amepangiwa kukutana na rais wa Abu Dhabi, Sheikh Khalifa bin Zayed al-Nahayan, hii leo.

Anatarajiwa pia kuutembelea mji wa Masdar, mradi wa Abu Dhabi wa thamani ya dola bilioni 22, mji utakaokuwa huru kutokana na gesi ya carbon dioxide ambao umepangiwa kuwa makaazi kwa watu 55,000 ifikapo mwaka 2015.

Ziara ya kansela Merkel katika eneo la Ghuba inafanyika wakati masoko ya fedha yakikabiliwa na msukosuko kutokana na mzozo wa deni la Ugiriki. Kansela Merkel anatarajiwa leo, kwenda Saudi Arabia ambako atakutana na mfamle Abdullah mjini Jeddah.

Mwandishi: Josephat Charo/ AFP/DPA

Mhariri: Mtullya Abdu