Melinda Gates asema Afrika ni bara la matumaini | Magazetini | DW | 14.04.2012
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Magazetini

Melinda Gates asema Afrika ni bara la matumaini

Magazeti ya Ujerumani wiki hii yameandika juu ya uamuzi wa wanajeshi waasi wa kuyarejesha mamlaka kwa raia nchini Mali na juu ya mapigano baina ya nchi mbili za Sudan na mvutano wa kisiasa nchini Misri.

Mhisani mkubwa Melinda Gates(Mke wa Mwasisi wa kampuni ya Microsoft,Bill Gates)

Mhisani mkubwa Melinda Gates(Mke wa Mwasisi wa kampuni ya Microsoft,Bill Gates)

Gazeti la"die tageszeitung" limechapisha taarifa juu ya matukio ya nchini Mali. Gazeti hilo linasema kwamba hatua muhimu imechukuliwa, katika juhudi za kuutatua mgogoro wa kisiasa nchini humo. Gazeti la"die tageszeitung" limeandika kwamba kikundi cha wanajeshi waliotwaa mamlaka nchini kimeamua kuyarejesha mamlaka hayo kwa raia.

Wanajeshi hao waliiangusha serikali halali tarehe 22 mwezi wa machi. Baada ya kukubaliana na ujumbe wa jumuiya ya uchumi ya nchi za Afrika Magharibi Ecowas wanajeshi hao wameyarudisha mamlaka kwa raia. Na kwa upande wake jumuiya hiyo ya uchumi imeviondoa vikwazo vilivyowekwa dhidi ya Mali.

Gazeti la"die tageszitung"pia limearifu kwamba Spika wa bunge la Mali Dioncounda Troure sasa amepewa jukumu la kuunda serikali ya mpito hadi utakapofanyika uchaguzi mnamo kipindi cha siku 40.

Gazeti la "Frankfurter Allgemeine" limechapisha taarifa juu ya mapigano makali yalitoyotokea baina ya Sudan na Sudan ya Kusini kwenye eneo la mafuta la Heglig .Gazeti hilo limeripoti kwamba msemaji wa serikali ya Sudan mjini Khartoum aliliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC kwamba majeshi ya Sudan ya Kusini na makundi ya waasi yamekiteka kisima cha mafuta cha Heglig.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limetilia maanani katika taarifa yake kwamba uhusiano baina ya nchi mbili za Sudan ni wa mvutano mkubwa. Migogoro baina ya nchi hizo inatokana pia na kasoro zilizopo katika ufafanuzi wa mipaka baina yao.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" wiki hii limeyatupia macho matukio ya nchini Misri. Gazeti hilo limeandika katika makala yake kwamba mvutano wa kisiasa umezidi kuwa mkubwa baina ya wanaitikadi kali wa kiisalamu na wanasiasa wanaofuata sera ya kutenganisha dini na siasa. Limearifu kwamba Mahakama ya mjini Kairo imesimamisha kazi ya tume ya katiba iliyoundwa kutokana na wajumbe walioteuliwa na Bunge linalodhibitiwa na vyama vya kidini.Tume hiyo ingelikuwa na jukumu la kuidurusu na kuifanyia marekebisho katiba ya Misri iliyokuwa inatumika wakati wa utawala wa Rais Hosni Mubarak.

Gazeti la "Süddeutsche Zeitung" pia limewapasha habari wasomaji wake juu ya mgogoro mwingine nchini Misri unaotokana na uamuzi wa Omar Suleiman wa kugombea Urais. Suleiman alikuwa Mkuu wa idara ya ujasusi wakati wa utawala wa Mubarak. Gazeti la "Südeutsche" limesema kwamba uamuzi wa Omar Suleiman wa kuingia katika kinyang'anyiro cha kugombea urais unathibitisha kuwapo mvutano baina ya wawakilishi wa vyama vya kidini na wanasiasa wanaofuata sera ya kutenganisha dini na siasa.

Gazeti la"Der Tagesspiegel"wiki hii limechapisha makala juu ya Aliko Dangote, mwananchi wa Nigeria ambae ni tajiri kuliko mtu mwengine yeyote barani Afrika. Gezeti hilo linatupasha kuwa anaetaka utajiri na mamlaka makubwa nchini Nigeria siyo lazima aingie katika biashara ya mafuta. Gazeti la "Der Tagesspiegel" linasema zipo njia nyingine ambazo mtu anaweza kuzitumia. Mfano umetolewa na Aliko Dangote,tajiri mkubwa kabisa barani Afrika.

Dangote anakadiriwa kuwa na utajiri wa dola Bilioni 12. Alianza mnamo miaka ya 1970 kwa kuagiza sukari,mchele na saruji. Na sasa tajiri huyo mwenye umri wa miaka 55 anakudusia kuiandikisha kampuni yake ya saruji,thamani ya dola bilioni 10 kwenye soko la hisa la London.

Gazeti la"Die Welt" limefanya mahojiano na Melinda Gates mke wa mwasisi wa kampuni ya Microsoft Bill Gates. Melinda na muwewe Bill wanalitembelea bara la Afrika mara kwa mara. Aliulizwa, ni jambo gani linalopotoshwa juu ya bara la Afrika.? Melinda Gates alijibwa kwa kusema kuwa watu wanasema bara hilo halina matumaini.! Amesema madai hayo ni upuuzi na yanamkasirisha sana. Ameeleza kuwa kila anaporudi kutoka Afrika anajawa matumaini juu ya bara hilo!

Gazeti la "die Welt" limeripoti kuwa Melinda Gates alikuwapo mjini Berlin kuzindua mradi wa maendeleo ya familia thamani ya dola milioni 10 kwa ajili ya watu wa Afrika magharibi.

Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen

Mhariri: Abdul-Rahman