1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ya Ugiriki imetekwa nyara na maharamia wa Kisomali

Kalyango Siraj19 Novemba 2008

Ghuba la Aden limeongezeka kuwa kitisho kwa safari za meli baada ya maharamia kuiteka meli ya tatu katika ghuba la hilo.

https://p.dw.com/p/Fxtt
Meli moja kati ya kadhaa zilizotekwa nyara na maharamia wa Kisomali katika Ghuba ya AdenPicha: picture-alliance/dpa

Maharamia wa Kisomali wameteka meli nyingine ya tatu katika mfulululizo wa hujuma zao dhidi ya meli za kibiashara katika ghuba la Aden.Hii imefuatia taarifa zingine kuwa wanamaji wa India wameizamisha meli moja ya maharamia nje ya mwambao wa Somalia.

Ghuba la Aden limeongezeka kuwa kitisho kwa safari za meli baada ya maharamia kuiteka meli ya tatu katika ghuba la hilo.Afisa wa shughuli za usafiri baharini amesema kuwa meli ya Ugiriki imetekwa nyara na maharamia wa kisomali.Na hii inajumulisha meli tatu kuwa mikononi mwa maharamia hao tangu kuiteka ile ya mafuta ya Saudi Arabia mwishoni mwa juma.

Afisa wa shirika la Afrika Mashariki linalowasaidia wasafiri majini,Andrew Mwangura,amenukuliwa na shirika la habari la Ujerumani la DPA akisema kuwa amepokea taarifa za kutekwa meli ya kigiriki ikiwa na mabaharia 25.Hata hivyo hakujapatikana taarifa zaidi kuihusu meli hiyo kama vile inaitwaje ama ilikuwa imebeba nini na ilikuwa inaelekea wapi.

Nae mkuu wa kituo cha kimataifa kinachoshughulikia taarifa za uharamia,Noel Choong, akihijiwa na shirika la habari la DPA hakuweza kuthibitisha taarifa za kutekwa nyara kwa meli ya Kigiriki,ila yeye amesema kuwa taarifa alizonazo ni za kutekwa nyara meli mbili ya mizigo ya Hong Kong pamoja na nyingine ya uvuvi ya Kiribati.

Meli ya Hong Kong ilikiwa na mabaharia 25 na kukodishwa na shirika la meli la Iran. Ilikuwa na shehena ya ngano iliokuwa inaipelewa Iran. Tena ile ya uvuvi ya Kibati ilikodishwa na kampuni moja ya Thailand na ilikuwa na mabaharia 12.

Meli zote zinaaminiwa kupelekwa katika mwambao wa Somalia.

Maharamia wameongeza harakati zao tangu waiteke meli ya mafuta ya Saudi Arabia siku ya jumamosi.Kufuatia tukio hilo majeshi ya ushirika wa NATO yamekuwa yakichunguza mienendo ya meli hiyo.Giovanni Gumiero ni kamanda wa jeshi la NATO ambae anakibarua cha ulinzi wa meli katika eneo hilo.Ameeleza kuwa eneo hilo limekuwa sugu kwa visa vya uharamia ambavyo vimeongezeka mara dufu tangu mwaka jana.

Meli zaidi ya kumi ziko mikononi mwa maharamia wa kisomali katika mwambao wa Somalia. Kuhusu meli ya mafuta ya Saudi Arabia, jeshi la wanamaji wa Marekani linasema limeiona ikiwa imetia nanga katika bandari mmoja ya Somalia ya Harardhere.Kampuni inayomiliki meli hiyo imesema kuwa inasubiri kuanza mazungumzo ya kulipa fidia.

Bandari ya Harardhere inapatikana umbali wa kilomita 400 hivi kutoka eneo la Eyl ambalo ndilo ngome ya maharamia hao.Kawaida maharamia hao huzielekeza meli walizoteka katika bandari hiyo na hivyo kuziweka manuari za kijeshi katika hali ya tahadhari wakati wakiwashikilia mabaharia wa meli hizo.

Na hayo yakiarifiwa meli ya wanamaji wa India inasema imekabiliana na maharamia wa kisomali na kufanikiwa kuzamisha meli ya maharamia hayo na mataboti zingine zikatoroka.

Umoja wa Ulaya umetoa ruhusa kutumwa meli za kijeshi, kati ya tano na saba kutumwa katika ghuba la Aden ili kushika doria.Inasemekana meli hizo zitawasili huko mapema mwezi Disemba.