1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Meli ' Maryam' kuelekeea Gaza

22 Julai 2010

Meli moja ya misaada iliyowabeba wanaharakati wa kike kutoka Lebanon, ipo katika bandari ya Tripoli, nchini Lebanon ikijitayarisha kuelekea Gaza ikiwa imesheheni misaada ya kiutu kwa ajili ya Wapalestina.

https://p.dw.com/p/ORhl
Meli za misaada, zinazoelekea Gaza.Picha: AP

Meli hiyo kwa jina Maryam inalenga kuvunja vizuizi vya Israel huko Gaza, na imewabeba wafanyakazi 50 wa kutoa misaada, wakiwemo watawa kutoka Marekani.

'' Sote tumevutiwa na mradi huu- kwa sababu tumeunganishwa na ile hisia ya kumaliza udhalimu mkubwa na ukiukaji wa haki za kibinadamu dhidi ya wanawake, na watoto huko Gaza, alisema Samar hajj mmoja walioandaa meli hiyo ya Maryam.

Hamas Polizei Polizistinnen Gaza Gazastreifen Palästinenser
Hamas walichukua uongozi Gaza mwaka wa 2007.Picha: AP

Israel imekuwa ikilizingira kijeshi eneo la Gaza na kuliekeea vikwazo tangu kundi la Kipalestina Hamas liliposhinda uchaguzi katika eneo hilo mwaka wa 2006. Ni wakati huo pia ndio Hamas walipomteka nyara mwanajeshi wa Israel Gilat Shalit ambaye wanamzuilia hadi leo. Israel imevikaza vikwazo hivyo kwa ushirikiano na Misri- na imelitia katika hali ya matatito eneo la Gaza katika mahitaji yote muhimu ya kiutu.

Mei 31 mwaka huu, Israel iliuvamia msafara wa meli uliokuwa umewabeba wanaharakati kutoka Uturuki waliotaka kuvunja vizuizi hivyo vya Israel. Matokeo ilikuwa kuuawa kwa wanaharakati tisa. Baada ya shambulio hilo lililoshtumiwa kote ulimwenguni, Samar Hajj aliyeandaa meli hii ya Maryam, alikutana na wanawake wengine na kufanya maandamano mjini Beirut.

Tulisikitishwa na picha tulizokuwa tunaziona katika televisheni, alisema Hajj.

Israel eskortiert Hilfslieferungen für Gaza NO FLASH
Meli Maryam itaanza safari siki kadhaa zijaazo.Picha: AP

Baadaye wanawake hao wakawasiliana na Yasser Kashlak- Raia mmoja wa Syria mwenye asili ya Palestina ambaye anaongoza vuguvugu la kuwapa uhuru Wapalestina. Kashlak alikuwa amefadhili meli nyingi ambazo zimejaribu kuingia Gaza kwa nguvu, ikiwemo msafara wa meli kutoka Uturuki.

Walipokuwa katika mikutano ya kupanga hatua za kuchukuliwa, mwanamke mmoja alitamka jina Mary....na ndipo Samar na wenzake wakapata jina la meli ya Maryam.

Meli hiyo inayopanga kuanza safari yake kuelekea Gaza katika siku kadhaa zijazo, itasimama katika bandari kadhaa za nchi kabla ya kufika Israel- kwa sababu ya uhasama uliopo kati ya Lebanon na Israel. Mwezi uliopita Cyprus ilizipiga marufuku meli zote zinazoelekea Gaza kutia nanga katika bandari yake.

Samar Hajj anasema tayari amepokea maombi kutoka kwa wanawake 500 wanaotaka kushiriki katika safari hiyo ya Gaza, lakini akasisitiza Maryam itawabeba wanawake 50 pekee yake.  Idadi kubwa ya wanawake hao watakuwa ni wa Lebanon, na wengine itakuwa ni Waarabu, wengine kutoka nchi za Ulaya pamoja na Marekani.

Meli hiyo itakuwa inasafirisha dawa za kukabiliana na saratani, pamoja na bidhaa nyengine muhimu zinazohitajiwa na wanawake na watoto. Samar Hajj ameongeza kwamba meli yao haitobeba silaha zozote.

Wanawake wote watakaokuwa katika meli hiyo wataitwa kwa jina Maryam. Na utawatofautisha tu kwa kuwaita Maryam wa kwanza, wa pili, wa tatu na kadhalika.

Mwandishi: Munira Muhammad/ IPS

Mhariri: Josephat Charo.