1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Medwedew,rais mpya wa Urusi

Rabitz, Cornelia (DW Russisch)3 Machi 2008

Eti kweli Putin atamuachia mwanafunzi wake kisiasa ashike hatamu za uongozi?

https://p.dw.com/p/DHFD
Mtangulizi na mrithi wake,Putin na MedwedewPicha: AP

Kipenzi cha Kremlin,Dimitri Medwedew ameshinda uchaguzi wa rais ulioitishwa jumapili iliyopita nchini Urusi.Ushindi wa mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 42 ulikuwa hakika tangu December mwaka jana pale  Vladimir  Putin alipoanza kumpigania.Upande wa upinzani unautaja uchaguzi huo kua ni kiini macho.Wassimamizi wa uchaguzi wanazungumzia juu ya mambo yasiyo ya kawaida.


Matokeo ya uchaguzi huo hayajamshangaza yeyote.Yalikua yakijulikana hata kabla ya uchaguzi kufanyika.Rais mpya wa Urusi anaitwa Dmitri Medwedew.Na hatutashangaa pia tutakapoarifiwa baadae kwamba Vladimir Putin amechaguliwa kua waziri mkuu.


Mtu hawezi kusema uchaguzi umefanyika kwa njia za kidemokrasi kwasababu hakujakua na chaguo lolote jengine la maana.Wananchi wa Urusi wametakiwa tuu wakamchague mtu ambae mwenyewe Putin ndie aliyemteuwa ili aridhi nafasi yake.Wametekeleza matarajio hayo.Wamecheza mchezo waliotakiwa kucheza wakijiwekea matumaini ya kuona hali ya mambo inasalia kama ilivyo.


Wengi nchini humo wanaamini  Putin amewaletea neema na utulivu.Wanataka hali iendelee hivyo hivyo chini ya uongozi wa Medwedew.Na walioko Kremlin nao wanaweza kuonyesha wameheshimu sheria na katiba.


Walimwengu sasa wanamkodolewa macho Dim tri Medwedew mwenye umri wa miaka 42.Sera gani za kisiasa anategemea kuzitilia mkazo?Atalenga kweli,kama wengi wanavyoashiria,sera zake upande wa magharibi na  kuacha milango wazi?Pengine atajikwamua toka  kucha za Putin?


Hakuna ajuaye na watu wakiingiwa na hofu halitakua kosa pia.Hakujakua na ishara yoyote inayoonyesha anaweza kujikwamua.Medwedew,ambae mlezi wake wa kisiasa ni Putin,hata katika kampeni za uchaguzi hakuonyesha dalili zozote za mwenye kutaka kuleta magezi.Ni kweli kabisa kwamba anatokana na kizazi chengine na kwamba kinyume na mtangulizi wake,hakuinukia  na kupanda daraja toka idara za upelelezi.


Ataongoza taifa ambalo  Putin ameweka mhuri wake kwa muda wa miaka minane na kulibadilisha pia.Taasisi za kidemokrasia na kisheria zimedhoofishwa,mashirika ya kijamii yamepwaya na sera za kisiasa na kiuchumi zinaongozwa na wakuu wa idara za upelelezi.

Neema za kiuchumi zinazotajwa zimeletwa na Putin zimesababishwa na biashara ya mafuta na gesi inaosafirishwa nchi za nje-waachache wamezidi kutajirika na wengi wamezidi kua fukara.Kiongozi mpya wa Urusi kwa hivyo ana kazi kubwa ya kufanya na anaweza kuitumia fursa aliyoipata kuhimiza usawa na maendeleo nchini Urusi na kujitahidi kupalilia uhusiano mzuri pamoja na Marekani na Ulaya.


Medwedew atakua akifanya kazi kwa ushirikiano pamoja na waziri mkuu-ambae jina lake ni Vladimir Putin.Kwa mtazamo wa Urusi ,hali hiyo haijawahi kushuhudiwa.Ndo kusema Putin ataridhia  kweli kumuona Medwedew akimiliki madaraka makubwa zaidi?


Yeyote yule aliyefuatilizia kwa makini wakati wa kampeni za uchaguzi ,jinsi Putin na sio mridhi wake,alivyokua akibuni mikakati ya siku za mbele,basi hatakosa kutilia shaka hoja hizo.


Kimoja ni hakika,Urusi,kutokana na historia yake,daima imekua ikipata shida kujiambatanisha na mageuzi  makubwa ya kidemokrasi.Na pengine sio maadili yote ya magharibi yanafaa au yanabidi kuigizwa na dola hilo kubwa jirani la ulaya.


Si wakati wa kufanya pupa hivi sasa, kinachotakiwa ni subira.Watu wanabidi wawaombee wananchi wa Urusi,matarajio yao yaliyowafanya wateremke vituoni kumchagua rais mpya ,yatekelezwe na wajipatie maisha bora kwa siku za mbele.