1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mechi za AFCON zaendelea licha ya kitisho cha Ebola

5 Septemba 2014

Mlipuko wa ugonjwa hatari wa Ebola, ulaghai na udanganyifu, mchezaji kupigwa na kuuawa na mashabiki wake..ni kama soka la Afrika haliwezi kujiondolea sifa mbaya ya kukumbwa na matukio ya vurugu.

https://p.dw.com/p/1D7qU
Sport Fußball Africa Cup of Nations 2013 Finale Nigeria Burkina Faso
Picha: Getty Images

Miezi miwili tu baada ya bara la Afrika kuwa na kampeni ya fedheha ya Kombe la Dunia nchini Brazil, iliyogubikwa na wachezaji kufanya vitisho vya migomo kuhusiana na migogoro ya kutolipwa hela, duru ya mwisho ya mechi za kufuzu katika Kinyang'anyiro cha Kombe la Mataifa ya Afrika litakaloandaliwa hapo mwakani imeanza hapo jana na inaendelea leo huku kukiwa na matatizo chungu nzima.

Mlipuko wa virusi vya Ebola katika eneo la Afrika Magharibi umezusha hofu miongoni mwa wale wanaohitajika kusafiri au kuandaa timu kutoka mataifa yaliyoathirika. Hali hiyo imelazimisha angalau timu mbili kucheza ugenini mbali kabisa na nchi zinakotoka.

Erick Mwanza
Meneja wa Mawasiliano wa Shirikisho la Kandanda Afrika - CAF, Erick MwanzaPicha: CAF

Timu mbili tayari zimepigwa marufuku kushiriki dimba hilo kwa udanganyifu na kuwatumia wachezaji wasiostahiki kucheza na nyingine mbili zikajiondoa zenyewe baada ya kushindwa kucheza mechi za duru za awali.

Kifo cha mchezaji wa Cameroon Albert Ebosse katika mchuano wa ligi nchini Algeria mwezi uliopita baada ya kugongwa na kifaa kichwani kilichorushwa na mashabiki wake ni dalili nyingine ya ukosefu wa usalama katika viwanja vya Afrika ambako wachezaji nyota wa kandanda wamekuwa wakicheza soka lao chini ya usimamizi mbaya. Mechi za mwisho za kufuzu zinazishirikisha timu 28 zilizopangwa kwenye makundi saba na kushindania nafasi 15 pamoja na wenyeji Morocco katika dimba hilo litakaloandaliwa Januari na Februari hapo mwakani.

Mabingwa watetezi Nigeria watafungua dimba leo katika Kundi A dhidi ya Kongo Brazaville, ambayo ilipewa kibai cha kusonga mbele baada ya Rwanda kufurushwa kwa kumtumia mchezaji mwenye uraia wa nchi mbili.

Algeria itaanza shughuli ugenini dhidi ya Ethiopia katika kundi B. Katika kundi D, Cote d'Ivoire na Cameroon zinaanza maisha bila ya Didier Drogba na Samuel Eto'o ambao walitundika njumu zao. Cameroon wanasafiri kumenyana na Kong wakati Cote d'Ivoire wakikabana koo na Sierra Leone. Sierra Leone italazimika kuwatumia wachezaji wanaocheza ligi za kigeni pekee.

CAF iliamuru kuwa hakuna mechi zozote zitakazoandaliwa nchini Sierra Leone wala Guinea hadi katikati ya Septemba. Ghana itacheza dhidi ya Uganda katika mechi ya Kundi E bila wachezaji wake watatu, Michael Essien aliyestaafu na Kevin Prince Boateng na Sulley Muntari waliotimuliwa kikosini kutokana na utovu wa nidhamu.

Mwandishi:Bruce Amani/AFP/DPA/reueters
Mhariri:Josephat Charo