Mechi ya Bundesliga ya ″goli hewa″ haitarudiwa | Michezo | DW | 28.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Michezo

Mechi ya Bundesliga ya "goli hewa" haitarudiwa

Mahakama ya michezo ya Shirikisho la Soka Ujerumani DFB imetoa uamuzi kuwa mechi kati ya Hoffenheim na Bayer Leverkusen iliyozingirwa na bao lenye utata haitarudiwa.

Mpira uliopigwa kwa kichwa na Stefan Kiessling Leverkusen uliingia langoni kupitia nje ya wavu

Mpira uliopigwa kwa kichwa na Stefan Kiessling Leverkusen uliingia langoni kupitia nje ya wavu

Mahakama hiyo imesema refa wa mechi hiyo Felix Brych hakukiuka taratibu za mchezo wa soka nchini Ujerumani kufuatia maamuzi yake ya kuidhinisha bao la mchezaji Stefan Kiessling lililofungwa katika dakika ya 72 baada ya mpira aliopiga kwa njia ya kichwa kuingia langoni kupitia nje ya wavu katika tundu na hivyo kuipa ushindi Leverkusen dhidi ya Hoffenheim ya mabao mawili kwa moja.

Borussia Dortmund walilipiza kisasi kichapo cha mwaka jana kwa kuwapiku Schalke 04

Borussia Dortmund walilipiza kisasi kichapo cha mwaka jana kwa kuwapiku Schalke

Katika mechi zilizochezwa mwishoni mwa wiki, hakuna mengi yaliyobadilika sana kileleni mwa msururu wa ligi, baada ya Bayern Munich, Borussia Dortmund na Bayer Leverkusen kushinda mechi zao. Hata hivyo hapo jana Hamburg ilienedelea kupepea kwa kusajili ushindi wa mabao matatu kwa sifuri dhidi ya Freiburg chini ya kocha mpya Mholanzi Bert van Marwjik. Hamburg ambao sasa wametoka sare mara mbili na kushinda mara mbili ili kusonga katika nafasi ya 12 chini ya kocha van Marwjik, walisaidiwa sana na mlinda lango wa Freiburg Oliver Baumman, aliyefanya makosa na kuwazawaidia magoli yote matatu.

Katika mechi nyingine, ya jana, Borussia Moenchengladbach walijikwamua kutokana na kichapo cha wiki iliyopita mikononi mwa Hertha Berlin na kuwakalifisha Eintracht Frankfurt mabao manne kwa moja na kusonga katika nafasi ya nne kwenye ligi, baada ya ushindi wao wa tano katika mechi zao tano za nyumbani msimu huu.

Viongozi Bayern Munich walikuwa na kibaria kikali dhidi ya Hertha Berlin

Viongozi Bayern Munich walikuwa na kibaria kikali dhidi ya Hertha Berlin

Jumamosi, Borussia Dortmund waliwazidi nguvu watani wao wa jadi Schalke, kwa kuwarambisha magoli matatu kwa moja, wakati Bayern Munich wakitokwa jasho na kuponyoka na ushindi wa mabao matatu kwa mawili dhidi ya Hertha Berlin. Bayer Leverkusen pia ilitoka nyuma na kuipiku Augsburg mabao mawili kwa moja ili kubakia katika nafasi ya tatu kwenye Bundesliga, ikiwa na pointi sawa na Dortmund, moja nyuma ya viongozi Bayern.

Mainz iliwashinda washika mkia Eintracht Braunschweig 2-0, wakati nao Hannover wakiwa na siku ngumu, walipofunzwa soka kwa kufungwa mabao manne kwa moja nyumbani na Hoffenheim, mechi iliyojaa sarakasi chungu nzima, na hata Hannover kumaliza mchezo ikiwa na wachezaji tisa uwanjani.

Mchezaji Mame Biram Diouf alionyeshwa kadi ya njano kwa kudai penalty katika dakika ya 10, na kisha Msenegal huyo akatimuliwa uwanjani baada ya kupiga mbizi katika eneo la hatari. Picha za video hata hivyo zilionyesha kuwa ulikuwa uamuzi wa kujadiliwa. Naye Marcelo akaonyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili kwa kulalamikia kwa hasira bao lililofungwa la Hoffenheim. Wolfsburg iliishinda Werder Bremen magoli matatu kwa sifuri.

Mwandishi. Bruce Amani/AFP/Reuters

Mhariri: Yusuf Saumu