Mchakato wa marekebisho ya katiba Kenya waanza | Matukio ya Afrika | DW | 29.05.2019
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mchakato wa marekebisho ya katiba Kenya waanza

Mchakato wa kuchagiza kura ya maoni umeanza rasmi. Tume ya Uchaguzi nchini Kenya IEBC imeanza shughuli ya kuhakiki saini zilizowasilishwa na chama cha upinzani cha Thirdway Alliance.

Ili hatua hiyo kupita, sharti saini milioni moja zipate ridhaa ya tume ya uchaguzi mkuu. Kauli za kutaka kuifanyia katiba mageuzi kupitia kura ya maoni zimezua gumzo nje na ndani ya serikali kuu kabla ya uchaguzi mkuu wa 2022. Shughuli ya kuhakiki saini milioni 1.4 zilizowasilishwa na chama cha upinzani cha Thirdway Alliance ilianza rasmi kwenye ukumbi wa Chui wa taasisi ya kuandaa mitaala ya KICD hapa jijini Nairobi.Chama cha Thirdway Alliance kiliwasilisha rasimu ya mswada wa mageuzi ya katiba 2019 maarufu mpango wa Punguza Mzigo pamoja na saini milioni 1.4 kwa tume ya uchaguzi ya IEBC. Ili mchakato uingie hatua ya pili sharti saini milioni moja zipate ridhaa ya tume ya uchaguzi.Ekuru Aukot ni kiongozi wa chama cha Thirdway Alliance na anaeleza.

Kwa upande wake tume ya uchaguzi ya IEBC inatazamiwa kuwasilisha mswada huo wa mageuzi kwa mabunge yote 47 ya kaunti ikiwa saini zitapata ridhaa.Kulingana na utaratibu, ikiwa mabunge ya kaunti yasiyopungua 24 yataupitisha mswada huo katika muda wa miezi 3, jukumu litaliangukia bunge la taifa na baraza la senate kuridhia au kuubwaga.Mswada huo utaweza kupata ridhaa ya rais pale utakapoungwa mkono na wengi katika bunge la taifa na baraza la senate. Endapo bunge la taifa halitaupitisha, kura ya maoni itafanyika kuwapa wakenya nafasi ya kuipaaza sauti yao.

Porträt - Dr. Ekuru Aukot

Ekuru Aukot anataka marekebisho ya katiba

Kulingana na mswada wa mpango wa Punguza Mzigo,mabunge ya kaunti yatavuna pakubwa na kutengewa fedha zitakazoongezeka kutokea 15% hadi 35%.Kadhalika mswada unapania kuipunguza idadi ya wabunge kutokea 416 hadi 147 nao muda wa rais kuhudumu kubadilishwa kuwa muhula mmoja pekee wa miaka 7.Hata hivyo viongozi ndani ya serikali kuu wana mtazamo tofauti.Mapema wiki hii Spika wa bunge la taifa Justin Muturi aliweka bayana kuwa kura ya maoni si jambo la kufanyiwa dhihaka.

Mapendekezo mengine nayo pia yamewasilishwa bungeni.Mbunge wa Tiaty William Kamket alipendekeza kuundwa kwa nafasi ya waziri mkuu mwenye mamlaka na manaibu wake wawili.Kwa upande wake naibu wa rais William Ruto alisisitiza kuwa ataunga mkono mswada kama huo ikiwa utakuwa na manufaa kwa mwananchi wa kawaida.

Jee kisheria, kipi kinachowezekana kufanyiwa mageuzi kufanikisha kura ya maoni? Hilo ndilo suali nlilomuuliza Zawadi Kingi ambaye ni wakili jijini Nairobi.

Mpango wa Punguza mzigo unadhamiria pia kuzikita juhudi za maendeleo kwenye wadi za kaunti ili kuifutilia mbali hazina ya maendeleo ya maeneo bunge-NG-CDF.