Mbuga ya Virunga yazindua mpango wa maendeleo | Masuala ya Jamii | DW | 09.10.2013
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Masuala ya Jamii

Mbuga ya Virunga yazindua mpango wa maendeleo

Baada ya takribani miaka 20 ya vita mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Mbuga ya Taifa ya Virunga imezindua mpango wa maendeleo wa miaka 10, unaolenga kuufufua uchumi na kufungua maelfu ya ajira kwa wenyeji.

Mbuga ya Taifa ya Virunga mashariki mwa Kongo

Mbuga ya Taifa ya Virunga mashariki mwa Kongo

Mpango huo ni sehemu ya juhudi za kurejesha amani katika eneo hilo. Mpango huo ujulikanao kama ''Virunga Alliance'', au ''Ushirikiano wa Virunga'', utaweka miradi ya kuongeza upatikanaji wa nishati endelevu kando ya gridi ya taifa, na ya kuboresha sekta ya kilimo.

Mamlaka ya mbuga hiyo imeunda ushirika na wahisani ambao watakuwa tayari kuwekeza kiasi cha dola za kimarekani milioni mia na hamsini (US$ 150 Mil.). Wakfu wa Howard G Buffet ambao umeongoza njia kwa kutoa msaada wa kiufundi na kifedha katika kuandaa mpango huo, umeahidi kutoa fedha zaidi karibu dola milioni 20, ambazo zitatumiwa kujenga mtambo utakaotumia maji ya mto Rutshuru kuzalisha umeme kiasi cha megawati 12.6, ifikapo mwaka 2016. Umeme huo ukipatikana, utasaidia kuinua sekta ya kilimo na ufugaji, na kuongeza kipato cha wakazi wa eneo lililo karibu, ambao ni masikini.

Mchango kwa amani na uchumi

Mauzo ya umeme yatatumiwa kuitunzia Mbuga ya Taifa ya Virunga kwa miaka kati ya 75 na 100 ijayo. Ndani ya mbuga hiyo wanaishi wanyama adimu kama sokwe wa milimani, na mimea ambayo haipatikani mahali pengine.

Mfanyakazi wa mbuga ya Virunga akimhudumia sokwe adimu wa milimani

Mfanyakazi wa mbuga ya Virunga akimhudumia sokwe adimu wa milimani

Mkurugenzi wa Mbuga ya Taifa ya Virunga Cosma Wilungula amesema mbuga hiyo inaweza kutoa mchango mkubwa katika kuunusuru uchumi wa eneo hilo na kurejesha amani katika mkoa mzima.

''Msaada wa wakfu wa Howard G Buffet na wa Umoja wa Ulaya, umeonyesha kuwa jumuiya ya kimataifa inaunga mkono juhudi na uwezo wetu kwa manufaa ya mustakabali wa eneo hili'', ameongeza Wilungula.

Katika nyayo za mradi wa awali

Mpango huu mpya umejengwa juu ya mfano wa mradi mwingine wa awali ambao ulifadhiliwa na Umoja wa Ulaya na wakfu wa Howard G Buffet, ambao umezalisha umeme kiasi ya megawati 0.4 na viwanda viwili vidogo vya kusindika mazao ya kilimo, kwenye kitako cha mlima wa Ruwenzori.

Machafuko ya vita na uasi yanatoa kitisho kwa mbuga ya Virunga

Machafuko ya vita na uasi yanatoa kitisho kwa mbuga ya Virunga

Muasisi na Mkurugenzi Mkuu wa wakfu wa Howard G Buffet na ambaye wakfu huo umechukua majina yake, amesema baada ya kufanya kazi kwa ushirikiano na washirika wenyeji katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, amesema anaamini kwamba kuunda nafasi za kazi katika sekta ambayo inasimamiwa na taasi za kitaifa, ni hatua muhimu katika kurejesha amani ya kudumu.

''Mpango huu unatoa nafasi ya kipekee katika juhudi za kuleta maendeleo kwa watu wa mashariki mwa Kongo, na wakati huo huo ukiihifadhi mbuga ambayo ni mojawapo ya hazina muhimu za taifa hilo'', amesema bwana Buffet.

Mbuga ya Taifa ya Virunga ndio ya kwanza kuanzishwa barani Afrika, mwaka 1925, na tangu mwaka 1979 imewekwa kwenye orodha ya UNESCO ya turathi za dunia. Mbuga hiyo imekuwa ikikabiliwa na kitisho kutokana na hali ya vita mashariki mwa Kongo, na walinzi wake 130 wamepoteza maisha katika vita hivyo.

Mwandishi: Daniel Gakuba/DPAE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman

DW inapendekeza

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com