1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mbeki amtaka rais Gbagbo kumfungulia njia Ouattara kushiriki katika uchaguzi.

Josephat Charo.15 Aprili 2005

Rais Thabo Mbeki wa Afrika Kusini amemtaka kiongozi wa Ivory Coast kutumia mamlaka yake kuhakikisha uchaguzi unakuwa wazi, huru na wa haki kwa wananchi wote nchini humo. Wito huu umetolewa kufuatia mkutano uliofanyika mjini Pretoria, Afrika Kusini juma lililopita.

https://p.dw.com/p/CEG4

Wito alioutoa rais Mbeki, ambaye alikabidhiwa jukumu la kuutanzua mzozo wa Ivory Coast na umoja wa Afrika, ulikuwa ukisuburiwa kwa hamu kubwa kwani swala la kuwaruhusu watu wote kushuriki katika uchaguzi, ndilo shina la vita vya wenyewe kwa wenyewe, ambavyo vimelizorotesha taifa hilo kiuchumi na kutishia amani ya mataifa yanayopakana na nchini hiyo.

Rais Mbeki amemtaka rais Laurent Gbagbo wa Ivory Coast kumfungulia njia kiongozi mkuu wa upinzani, Alassane Ouattara, aweze kugombea wadhifa wa urais katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwezi Oktoba mwaka huu. Kundi la waasi wanaolidhibiti eneo la kazkazini la nchi hiyo linataka sharti hilo muhimu litimizwe.

Rais Gbagbo mara kwa mara amekuwa akihoji kwamba katiba lazima ifanyiwe marekebisho kubadili kipengele kinachomzuia Ouattara kugombea wadhifa wa urais. Anasema swala hili litailazimu nchi hiyo kuwa na kura ya maoni, ambayo inaweza kufanyika tu iwapo waasi watakubali kuwasilisha silaha zao. Rais Mbeki alipewa mamlaka ya kuamua juu ya swala hili katika mkutano wa Pretoria Afrika Kusini.

Waasi kwa upande wao wameukataa msimamo huo na nchi hiyo imegawanyika pande mbili za amani na vita, zinazotenganishwa na ardhi isiyomilikiwa na upande wowote. Msemaji wa rais Gbagbo, Desire Tagro, aliisoma barua iliyoandikwa na Mbeki inayomtaka Gbagbo kutumia mamlaka yake kwa mujibu wa katiba ya nchi hiyo, hususan ibara ya 48, kuidhinisha kisheria uamuzi ulioafikiwa katika mkutano huo wa Pretoria.

Ivory Coast ilitumbukia katika mzozo wa kisiasa mwezi Septemba mwaka wa 2002 wakati waasi walipojaribu kumuondoa mamlakani rais Gbagbo na kuliteka eneo la kazkazini la nchi hiyo. Wanajeshi wa kulinda amani elfu 10 wa kifaransa na wa umoja wa mataifa wanalilinda eneo linalozitenganisha pande mbili zinazozozana.

Ibara ya 48 inasema rais anaweza kuchukua hatua isiyo ya kawaida iwapo taasisi au serikali ya Ivory Coast inakabiliwa na hali ya hatari. Inaongeza kusema kwamba rais Gbagbo anatakiwa kushauriana na spika wa bunge na baraza la maswala ya katiba ya nchi. Barua ya Mbeki inasema usalama wa Ivory Coast ulihatarishwa na upinzani wa waasi.

Hakuna matamshi yoyote yaliyotolewa na ofisi ya rais kuhusiana na uamuzi huo wa Mbeki, lakini Tagro amesema viongozi wa serikali wanauona kama pendekezo tu. Msemaji wa kiongozi wa waasi, Guillaume Soro, alisema wamepokea barua hiyo lakini hawakutoa taarifa yoyote.

Akizungumzia barau hiyo ya rais Mbeki, Tagro alisema baraza la katiba nchini Ivory Coast, linalowajumulisha majaji, linatakiwa kukubali wagombea wanaochaguliwa na vyama vya kisiasa vilivyotia saini mkataba wa amani uliosimamiwa na Ufaransa mwaka wa 2003. Hii itamaanisha Ouattara ataruhusiwa kukiwakilisha chama chake cha RDR katika kinyang´anyiro cha kugombea wadhifa wa urais.

Ouattara anayeungwa mkono na upande wa kazkazini wa nchi hiyo, alizuiliwa na mahakama nchini humo kutoshiriki katika uchaguzi wa mwaka wa 2000 ulioshindwa na rais Gbagbo, eti kwa sababu mzazi wake mmoja anatoka Burkina Faso. Hatua hiyo ya mahakama ilisababisha mapigano barabarani yaliyopelekea kuuwawa kwa watu wengi.

Waangalizi wa kimataifa wanahofu kwamba vijana wanaomuunga mkono Gbagbo, ambao maandamano yao dhindi ya Ufaransa mwezi Novemba mwaka jana yalisababisha raia wa kigeni wasiopungua 8,000 kukimbia kutoka nchini humo, huenda wakazusha ghasia barabarani, iwapo Mbeki ataamua Ouattara aruhusiwe kugombea wadhifa wa urais.