1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazunguzo ya nyuklia ya Iran yarefushwa

Admin.WagnerD25 Novemba 2014

Matarajio ya kumalizika mgogoro wa muda mrefu kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yamesogezwa hadi mwakani baada ya pande mbili kushindwa kuafikiana kufikia muda wa mwisho uliowekwa tarehe 24.11.2014

https://p.dw.com/p/1Dsdk
Atomgespräche in Wien Außenminister 24.11.2014
Picha: picture-alliance/dpa/Roland Schlager

Mawaziri wa masuala ya kigeni kutoka Uingereza, China, Ufaransa, Urusi, Marekani na Ujerumani walisema siku ya Jumatatu kuwa hatua kadhaa zilizopigwa kuhusu makubaliano, na kwamba mapendekezo mapya yaliyotolewa katika siku kadhaa zilizopita yanahalalisha kuwapo na mjadala zaidi.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani John Kerry alisema bado kuna tofauti kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran, lakini akaongeza kuwa kwa kuzingatia walikotoka, na hasa katika siku chache zilizopita, huu siyo wakati wa kukata tamaa.

"Tunaamini makubaliano mapana yanayoshughulikia wasiwasi wa ulimwengu yanawezekana, yanatakiwa, na kwa nukta hii tumejenga uwelewa mkubwa wa namna makubaliano hayo yatakavyoonekana lakini bado kuna baadhi ya masuala muhimu tunayotofautiana, alisema waziri Kerry.

Mawaziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani na Iran - John Kerry na Mohammad Javad Zarif wakiwa na Catherine Ashton.
Mawaziri wa Mambo ya kigeni wa Marekani na Iran - John Kerry na Mohammad Javad Zarif wakiwa na Catherine Ashton.Picha: picture-alliance/AP Photo/Joe Klamar

Tofauti bado zipo

Bado kuna mapengo kuhusu kiasi gani hasa Iran itapunguza shughuli za urutubishaji wa madini yake ya Urani ambayo inaweza kutumika katika mitambo ya kuzalisha umeme na pia kutengeneza silaha za nyuklia, na ni kwa haraka gani vikwazo dhidi ya Iran vinaweza kuondolewa.

Pande zote mbili sasa zinalenga kueleza waliokubaliana ifikapo mwezi Machi, ambapo makubaliano ya mwisho yanatarajiwa kusainiwa ifikapo katikati mwa mwaka ujao. Makubaliano hayo yanatarajiwa kuwa kizuwio cha mpango wa nyuklia wa kiraia wa Iran, na kuhakikisha kuwa hautumiki kutengeneza silaha za atomiki. Matokeo yake ni kwa mataifa hayo sita kuiondolea Iran vikwazo vyote vya kiuchumi.

Zarif, Ashton waahidi kuharakisha mchakato

Waziri wa masuala ya kigeni wa Iran Mohammad Javad Zarif na Catherine Ashton, kiongozi wa majadiliano kwa upande wa mataifa sita, walisisitiza kuwa walitaka kukamilisha majadiliano hayo haraka iwezekanavyo, pengine kabla ya muda mpya wa mwisho.

Kazi kuhusu makubaliano hayo ilianza mwaka uliyopita, muda mfupi baada ya kuchaguliwa kwa Hassan Rouhani, aliemrithi Mahmoud Ahmadinajad mwenye msimamo mkali kama rais wa Iran.

Waandamanaji wakipinga mpango wa nyuklia wa Iran mjini Vienna.
Waandamanaji wakipinga mpango wa nyuklia wa Iran mjini Vienna.Picha: Reuters/H.-P. Bader

Rais Rouhani na rais wa Marekani Barack Obama wanakabiliwa na shinikizo nyumbani kutoka wanasiasa wahafidhina, ambao wanatilia mashaka uanzishaji tena uhusiano baina ya mataifa hayo, ambao ulikatizwa baada ya mapinduzi ya Kiislamu ya mwaka 1979.

Rais Rouhani aliiambia Televisheni ya taifa kuwa hawajafikia makubaliano, lakini walikuwa njiani kuelekea upande huo, na kuongeza kuwa "makubaliano yatafikiwa, kama siyo leo, basi kesho."

Kwa upande wake, waziri John Kerry aliwasihi Wapinzani wa chama cha Republican wanaoyadhibiti mabaraza yote ya bunge la Marekani kuwa na subira wakati wanaendelea na majadiliano na kuacha kuiandama Iran kwa kwa wito wa vikwazo.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/dpae, rtre.
Mhariri: Mohamed Abdul-Rahman.