1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Rais Tshisekedi na wapinzani yakwama

Saleh Mwanamilongo
19 Januari 2021

Moise Katumbi na Jeanpierre Bemba wamesema mazungumzo yamekwama baina yao na rais Felix Tshisekedi kuhusu kuundwa kwa muungano mpya wa kisiasa nchini Congo.

https://p.dw.com/p/3o8A4
DRC Afrika Treffen  Felix Tshisekedi  , Moise Katumbi und Jean Pierre Bemba
Picha: presidential press service of the DRC

Mbunge Muhindo Nzangi msemaji wa chama cha ''Ensemble pour la Republique'' cha Moise Katumbi,ametangaza kujiondoa kwa chama hicho kwenye muungano mpya wa ''Union Sacree'' ulioundwa na rais Felix Tshisekedi na chama hicho kimesema kitaendelea kubaki katika upinzani.

''Ujumbe tulio nao leo ni kwamba mazingira yaliopo hivi sasa hayaturuhusu kuendelea kubaki ndani ya muungano wa Union sacrée.  Ujumbe wa wazi uliotumwa na wenzetu walioko na rais Tshisekedi ni kwamba tuliwasaidia kumuondoa spika wa bunge kutoka chama cha  FCC cha Joseph Kabila,lakini wataendelea kushirikiana na wabunge kutoka chama hicho.''

Chama cha Katumbi kimeelezea kwamba rais Tshisekedi anadhamiria kuteuwa waziri mkuu mpya ambaye ni kutoka miongoni mwa wabunge waliokihama chama cha FCC cha Kabila. Na vilevile anatarajia kuunga mkono spika mpya wa bunge kutoka vuguvugu hilo la FCC.

Demokratische Republik Kongo I Staatspräsident Félix Tshisekedi in Kinshasa
Moise Katumbi, Jean-Pierre BEMBA sambamba na rais Félix Tshisekedi Picha: Giscard Kusema/Präsidialamt Kongo

Duru kutoka ikulu ya rais Tshisekedi zinasema kwamba vyama vya Katumbi na Bemba viliomba kupewa nyazifa za waziri mkuu na spika wa bunge. Na kwa hiyo wanataka kujiuza kwa mnada.

Hata hivyo, Msemaji wa chama cha UDPS cha rais Tshisekedi amesema kwamba mazungumzo yataendelea baina ya rais na viongozi hao wawili wa upinzani, ilikumaliza tofauti zao.

Mbunge Leon Mubikayi,kiongozi wa wabunge wa chama cha UDPS bungeni amesema wako tayari kukiachia chama cha Moise Katumbi wadhifa wa waziri mkuu.

Wiki iliopita Tshisekedi ,Katumbi na Bemba walikutana mjini Kinshasa ilikujadili uwezekano wa kuundwa kwa serikali ya mseto baada ya kuvunjika ile ya muungano baina ya Tshisekedi na Joseph Kabila.

Toka rais Tshisekedi kutangaza kuvunjika kwa muungano wake na Kabila mwezi Desemba  uliopita, hadi sasa Kabila hajatoa kauli yoyote. Na zaidi ya wabunge mia moja na hamsini wametangaza kukihama chama cha Kabila na kujiunga na rais Tshisekedi.

Kufuatia uchaguzi wa 2018,chama cha Kabila kilinyakuwa uwingi wa viti bungeni,lakini baadhi ya wabunge sasa wametangaza kukihama chama hicho na kumuunga mkono rais Felix Tshisekedi.