1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya nyuklia na Iran kuanza tena Novemba 29

Sylvia Mwehozi
5 Novemba 2021

Mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran yataanza tena baadae mwezi huu huku Rais wa Marekani Joe Biden akitafuta uwiano baina ya vitisho na motisha vya kuirejesha Iran katika kuafikiana na mkataba wa nyuklia wa 2015.

https://p.dw.com/p/42cSY
Iran |  Felix Plasencia -  Staatsbesuch in Teheran - Ebrahim Raisi
Picha: Iranian Presidency/AA/picture alliance

Iran imekubali kurejea katika meza ya mazungumzo yatakayofanyika Novemba 29 na mataifa yaliyo na nguvu duniani ili kuyaokoa makubaliano ambayo ilikubali kupunguza shughuli za nyuklia wakati huo ikipunguziwa vikwazo vya kiuchumi.

Mambo mengi yamebadilika tangu mazungumzo yalipovunjika mwezi Juni, haswa juu ya uchaguzi wa Iran ambao ulimuweka madarakani rais mwenye misimamo mikali Ebrahim Raisi.

Katika kipindi hicho cha mapumziko, Iran imeendelea na shughuli zake za nyuklia na kusababisha mataifa ya Magharibi yaliyounga mkono mkataba wa 2015 kuonya kwamba makubaliano hayo yanaweza yasiwe na maana kutokana na maendeleo ya Tehran.

Biden aliingia katika mazungumzo yasiyo ya moja kwa moja mjini Vienna kwa matumaini ya kuyafufua haraka makubaliano hayo yaliyokwama wakati wa utawala wa Donald Trump ambaye aliindoa Marekani katika mkataba huo. Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price alinukuliwa akisema kuwa Washington inaweza kufikia haraka makubaliano ya kufufua mkataba wa nyuklia na Iran ikiwa Tehran ina dhamira ya kweli.

"Tunaamini bado inawezekana kufikia haraka na kutekeleza maelewano juu ya kurejea kwa pande zote katika kufuata JCPOA kwa kumaliza idadi ndogo ya masuala ambayo yalisalia mwishoni mwa Juni wakati duru ya sita ilipomalizika. Tunaamini kwamba ikiwa Wairani wako makini, tunaweza kufanya hivyo kwa muda mfupi."

Iran | Videostill | Anlage zu Uran-Anreicherung in Natanz
Sehemu ya mitambo ya kurutubisha Urani ya IranPicha: IRIB/AP Photo/picture alliance

Moja ya kipengele chenye kuleta msuguano kinahusu Iran inayotaka kuondolewa kwa vikwazo vyote wakati utawala wa Biden ukisema hatua pekee zilizoko ni zile zilizowekwa na Trump juu ya mpango wa nyuklia wakati Marekani ikijiondoa katika mkataba huo. Lakini jukumu hilo sio jepesi kwa sababu utawala wa Trump katika miezi yake ya mwisho uliiwekea Iran vikwazo vingi.

Rais wa Iran, Ebrahim Raisi ameyaonya mataifa ya Magharibi Alhamis kwamba hatokubaliana na "masharti magumu" katika mazungumzo ya baadae mwezi huu baada ya mkwamo wa miezi mitano.

Iran inataka uhakikisho kwamba Marekani itatekeleza wajibu wake na Biden alionekana kugusia ahadi hiyo wakati wa taarifa ya pamoja pembezoni mwa mkutano wa nchi zilizoendelea kiviwanda ulimwengu za G20 huko mjini Roma. Taarifa hiyo ilitolewa kwa pamoja na viongozi wa Uingereza, Ufaransa na Ujerumani, mataifa ambayo sambamba na Urusi na China yamesalia kuwa sehemu ya mkataba huo ambao zamani ulijulikana kama mpango wa pamoja wa utekelezaji JCPOA.

Viongozi wa nchi hizo tatu za Ulaya walisema kuwa "wanakaribisha dhamira ya Rais Biden inayodhihirisha wazi kuirejesha Marekani katika kuafikiana na JCPOA ili mradi tu Iran nayo itafanya hivyo". Hata hivyo, mataifa ya Magharibi yameendelea kuhoji ikiwa Rais wa Iran Ebrahim Raisi na kiongozi mkuu wa nchi hiyo Ali Khamenei kama wanayo dhamira ya kweli ya kulinda mkataba huo.