Mazungumzo ya Merkel na Putin mjini Sochi | Matukio ya Kisiasa | DW | 22.01.2007
 1. Inhalt
 2. Navigation
 3. Weitere Inhalte
 4. Metanavigation
 5. Suche
 6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya Merkel na Putin mjini Sochi

Mbali na nishati, wagusia pia suala la hatima ya Kosovo na mgogoro wa Mashariki ya kati.

Putin na Merkel katika mkutano na waandishi habari baada ya mazungumzo yao.

Putin na Merkel katika mkutano na waandishi habari baada ya mazungumzo yao.

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel na Rais Vladimir Putin wa Urusi wanataka mgogoro wa nishati liwe jambo la kuepukwa mnamo siku za usoni. Hayo yametokana na mazungumzo ya viongozi hao wawili hapo jana katika mji wa Urusi wa Sochi, ambapo pia waliafikiana kuhusu suala la Mashariki ya kati, huku Rais Putin akiunga mkono mkutano wa pande nne zinazohusika na suala hilo, ambao unapangwa kufanyika mjini Washington, tarehe 2 mwezi ujao wa Februari.

Viongozi hao wawili Rais Vladimir Putin na mwenyeji wake Kansela Angela Merkel walikua na mazungumzo na waandishi habari baada ya mkutano wao, huku Rais Putin akiuondolea wasi wasi Umoja wa ulaya , kwamba haina budi kuitegemea Urusi kama mshirika wa kuamini katika usambazaji wa nishati mnamo siku zijazo na atoa pendekezo la kuwa tayari kuweka akiba ya gesi ya Urusi nchini Ujerumani.

Kutokana na kuzuiliwa kwa muda wa siku tatu usafirishaji wa nishati mapema mwezi huu, ambapo Urusi inamtwika lawama jirani yake Belaruss, hivi sasa inajaribu kupunguza kutegemea njia ya kupitia nchi ya tatu na badala yake inazingatia ujenzi wa njia mpya hadi nchi za umoja wa Ulaya, ambao hupata 30 asili mia ya mafuta yake kutoka Urusi.Mvutano huo uliikasirisha Ujerumani na mataifa mengine ya Umoja wa Ulaya, kwa sababu Urusi ilishindwa kuzionya na mapema .

Akigusia upande huo Kansela Merkel alielezea matumaini na umuhimu wa kuwa na mawasiliano panapozuka hali kama hiyo akisema“Kwa upande wangu nilieleza wazi kwamba tunakubaliana kuwa mawasiliano katika hali ngumu kama ile yanapaswa kuimarishwa, ili kuepusha migogoro, na pia tunataka ushirikiano wa kutegemewa wa muda mrefu.”

Bibi Merkel pia aligusia juu ya suala la haki za binaadamu nchini Urusi na kumuuliaza mwenyeji wake, iwapo kuna maendeleo yaliopatikana katika kuchunguza kisa cha kuuwawa kwa mwandishi habari wa kirusi Anna Politkovskaya Oktoba mwaka jana. Putin alijibu kwamba maafisa wahusika wachunguza kikamilifu mauaji hayo, lakini hadi sasa hakuna kipya.

Aidha Merkel na Putin walizungumzia pia masuala ya kimataifa na miongoni mwayo ni hatima ya jimbo la Kosovo, chini ya mtazamo wa uchaguzi wa bunge nchini Serbia hapo jana na hali ya Mashariki ya kati.

Katika suala la Kosovo, palidhihirika tafauti ya maoni kati ya viongozi hao wawili, huku Rais Putin akisema hatima ya jimbo hilo la Serbia lazima iamuliwe bila shinikizo kutoka nje. Urusi daima imekua mtetezi wa Serbia. Matamshi ya kiongozi huyo wa Urusi aliyoyasisitiza katika mkutano wao na waandishi habari, yamekuja katika wakati ambao mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa kuhusu Kosovo,Martti Ahtisaari, akitarajiwa kupendekeza baadae wiki hii, aina fulani ya uhuru kwa jimbo hilo.

Kuhusiana na Mashariki ya kati, walikubaliana juu ya kuitishwa mapema mwezi ujao mkutano wa pande nne zinazohusika na mgogoro kati ya Israel na Wapalestina, ambazo ni Marekani, Urusi, Umoja wa mataifa na Umoja wa Ulaya ikiwemo Ujerumani, ambapo itakua ni mara ya kwanza pande hizo zinakutana baada ya kipindi kirefu.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Marekani Condoleeza Rice alitoa mualiko kawa Ujerumani kama mwenyekiti wa sasa wa Umoja wa Ulaya, wakati wa ziara yake mjini Berlin wiki iliopita.

Kansela Merkel alisisitiza kwamba Rais Putin anaiunga mkono hatua hiyo akisema :“Kuna makubaliano kamili juu ya haja ya kukutana kwa pande zinazohusika na Mashariki ya kati, na kama sasa zitakutana, basi watu wanaweza kukaa pamoja na kuzingatia njia za kutafuta suluhisho la mzozo kati ya Israel na Wapalestina chini ya mpango wa ramani ya njia ya kuelekea amani, na iwapo sulusho la mgogoro huo litapatikana, basi linakua muhimu katika kuipatia ufumbuzi migogoro mengine katika eneo hilo.”

Licha ya kwamba Kansela Merkel hana uhusiano wa karibu na Rais Putin kama alivyokua mtangulizi wake Gerhard Schroeder hata hivyo taarifa ya Ikulu ya Urusi-Kremlin, kuhusiana na mazungumzo kati ya Viongozi hao wawili ilisema yalikua ya kirafiki. Bibi Merkel alitangaza kwamba mkutano ujao wa mashauriano kati ya serikali za Ujerumani na Russia utafanyika baadae mwaka huu mjini Wiesbaden.

 • Tarehe 22.01.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHL2
 • Tarehe 22.01.2007
 • Mwandishi Mohammed Abdul-Rahman
 • Chapisha Chapisha ukurasa huu
 • Kiungo https://p.dw.com/p/CHL2
Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com