1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya Taliban na Marekani yamalizika

13 Machi 2019

Mazungumzo kati ya kundi la wanamgambo wa Taliban na Marekani yamemalizika Jumanne usiku mjini Doha, Qatar. Mazungumzo hayo yanalenga kumaliza miaka 17 ya vita vya Marekani nchini Afghanistan.

https://p.dw.com/p/3EvIf
Afghanistan Zabul - U.S. Soldat
Picha: picture-alliance/dpa/ISAF

Mazungumzo hayo yaliyochukua takribani wiki mbili yamepelekea miswada miwili ya makubaliano kati ya kikundi cha wanamgambo wa Talibani na serikali ya Marekani juu ya muda wa kuelekea kutoka kwa vikosi vya Marekani na hatua madhubuti za kupambana na ugaidi.

Mwanadiplomasia wa Marekani, Zalmay Khalilzadi, ameandika kwenye ukurasa wa Twitter kuwa " Mazingira ya kuleta amani yamefanywa kuwa bora". Ni wazi kwamba pande zote mbili zinataka kumaliza vita licha ya misukosuko kuelekea makubaliano hayo.

Afghanistan Taliban-Kämpfer in Farah
Wanamgambo wa Taliban Picha: picture-alliance/AP Photo

Kwa upande mwingine, Taliban imetoa tamko lao wakisema hatua zimepigwa katika mazungumzo hayo, ila walitilia mkazo kwamba hakuna makubaliano yaliyofikiwa kuhusu kusitisha mapigano.

Kadhalika hakuna makubaliano yoyote ya kulitaka kundi hilo la wanamgambo kuzungumza na serikali ya Afghanistan.

Kwa sasa pande zote mbili zinafurahia hatua zilizopigwa katika mazungumzo hayo na zinajiandaa kwa mazungumzo na kujiandaa kwa mkutano ujao, ambao hadi sasa tarehe haijapangwa.

Mazungumzo hayakuwa rahisi

Ofisa wa Taliban ambaye alikuwepo kwenye mazungumzo hayo amelimbia Shirika  la  Habari  la Associate Press kwa makubaliano ya kutotajwa jina lake kwamba suala tete kati ya pande mbili ni juu ya siku majeshi ya Marekani yatakapoondoka Afghanistan.

Taliban wanataka majeshi hayo yaondoke kati ya miezi mitatu hadi minne ijayo, wakati Marekani inadai itahitaji kuanzia miezi 18 hadi miaka miwili.

Afghanistan Luftwaffenstützpunkt Bagram nahe der Hauptstadt Kabul
Picha: picture-alliance/dpa/H. Amid

Suala jingine tata katika mazungumzo hayo ni madai kutoka kwa Marekani yanayotaka Taliban kutokuwa mwenyeji wa wanamgambo ambao wanafanya mashambulizi kwenye nchi yao. Taliban imesema itakubaliana na masharti hayo lakini imekataa sharti la kuainisha ni makundi gani wanayapaswa kujitenga nayo..

Mrithi wa Osama bin Laden ndani ya Al-Qaida, Ayman al Zawahri, anasadikiwa kuwa amejificha Afghanistan. Pia baadhi ya wanamgambo kutoka nchi za kiarabu mfano Yemen na Saudi Arabia wanasadikiwa kuwa wanaishi Afghanistan.

Taliban ambao wamekataa kuzungumza na serikali ya Afghanistan kwa madai kwamba wao ni vibaraka wa Marekani wamekua wakitaka kufanya mazungumzo kwa muda mrefu moja kwa moja na Marekani. Marekani imekua ikiliepuka suala hilo lakini sasa mazungumzo hayo yamefanikiwa kuanza.

 

Mwandishi: Harrison Mwilima/APE/AFPE

Mhariri: Sekioni Kitojo