Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yarefushwa | Matukio ya Kisiasa | DW | 17.11.2017
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages

Matukio ya Kisiasa

Mazungumzo ya kuunda serikali ya muungano yarefushwa

Juhudi za Kansela wa Ujerumani Angela Merkel kutafuta uwezekano wa kuunda serikali ya mseto ya vyama vinne zinaweza kuchukua juma zima baada ya vyama hivyo kupitisha muda wa mwisho wa kufikia makubaliano.

Deutschland Fortsetzung der Sondierungsgespräche (picture-alliance/dpa/S. Stein)

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel

Wawakilishi wa vyama ndugu vya kihafidhina vya Kansela Merkel Christian Democratic Union  CDU na Christian Social Union CSU, chama cha Free democratic Party FDP na kile cha walinzi wa mazingira die Grüne waliwaambia waandishi habari  leo saa kumi alfajiri kwamba wanapumzika  baada ya masaa 15 ya majadiliano ya kukatisha tamaa, na wanatarajia kurejea katika vikao vyao baadaye leo mchana.

"Bado tunaamini kwamba tunapaswa kulifanyia kazi hili kwa nguvu zetu zote, lakini kwa upande mwengine ni wazi kwamba ni ngumu," alisema Peter Tauber, Katibu mkuu wa chama cha Kansela Merkel cha CDU.

Wolfgang Kubicki, Naibu kiongozi wa chama cha FDP aliwaambia waandishi habari kuwa ameghadhabishwa  na kukatishwa tamaa baada ya wiki nne za majadiliano yaliyoshindwa kufikia makubaliano ya pamoja.

Deutschland Fortsetzung der Sondierungsgespräche (picture alliance/dpa/K. Nietfeld)

Kansela wa Ujerumani Angela Merkel akiingia katika mazungumzo ya kuthatmini uwezekano wa kuunda serikali ya muungano

Amesema iwapo hali itaendelea kama ilivyo kwa sasa majadiliano hayatafika kokote, ameongeza kuwa inasikitisha kukaa pamoja katika majadiliano lakini baadaye unatambua mnarejea pale pale mlipoanzia bila ya mafanikio.

Kwa upande wake Kiongozi wa CSU Horst Seehofer amesema masuala ya uhamiaji  pamoja na mambo mengine ndiyo yanayokwamisha majadiliano hayo.

"Ni muhimu sana kwetu kwamba Uhamiaji hautaongezeka, idadi tuliyonayo kwa sasa pamoja na kuunganishwa kwa familia ni kubwa mno na ndio maana hatuwezi kufikia suluhu itakayopelekea ongezeko la wahamiaji," alisema Seehofer.

Iwapo makubaliano hayatafikiwa basi uchaguzi mpya huenda ukaitishwa. 

Masuala ambayo bado ni changamoto kubwa katika meza ya mazungumzo ni suala la hifadhi ya wakimbizi uhamiaji na kuungana kwa familia, ulinzi wa mazingira, fedha, usalama wa ndani, pamoja na Umoja wa Ulaya na sera ya sarafu katika kanda ya euro. Hata hivyo Michael Kellner, afisaa mkuu katika chama cha walinzi wa mazingira cha kijani amesema bado kuna kazi kubwa ya kufanywa hakuna kilichokubaliwa na hakuna pia kilichoamuliwa.

Berlin Wahllokal zur Bundestagswahl (Getty Images/M. Hitij)

Raia wa Ujerumani akionekana kupiga kura yake katika uchaguzi uliyopita wa tarehe 24 September 2017

Muakilishi mwengine kutoka chama cha kijani amesema kuna hatua zilizopigwa juu ya kupunguza kwa kiasi kikubwa matumizi ya nishati yanayotokana na makaa ya mawe lakini chama ndugu cha kihafidhina cha Bavaria CSU kimekataa kukubaliana juu ya suala la wahamiaji wanaotaka hifadhi waliyotaka kuleta familia zao haraka iwezekanavyo nchini Ujerumani.

Aidha Merkel alitaka majadiliano haya ya kutathimini uwezekano wa kuundwa serikali ya mseto kukamilika siku ya alhamisi lakini hilo halikuwezekana kufuatia changamoto iliyoko ya kufikia makubaliano.

Hata hivyo kushindwa kufikia makubaliano juu ya Muunganao wa Jamaica jina linalotokana na rangi ya vyama hivyo kufanana na bendera ya Jamaica huenda ikasababisha Ujerumani kurejea tena debeni na kuandaa uchaguzi mpya.

Mwandishi:  Amina Abubakar AP/AFP/dpa

Mhariri: Yusuf Saumu

 

Matangazo

Unaweza kusikiliza matangazo yetu hapa

Kusikiliza matangazo ya Idhaa ya Kiswahili ya DW, tafadhali bonyeza alama ya spika ya masikioni hapo chini, na kuwasiliana nasi, tafadhali tuandikie moja kwa moja kupitia: kiswahili@dw.com