1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mazungumzo ya kuunda baraza la mpito yaendelea Sudan

Oumilkheir Hamidou
20 Mei 2019

Viongozi wa kijeshi na wakuu wa vuguvugu la maandamano ya umma nchini Sudan watarejea katika meza ya majadiliano kukamilisha muundo wa baraza tawala la mpito baada ya majadiliano hayo kushindwa kuleta tija hapo awali

https://p.dw.com/p/3IljV
Sudan Khartum Proteste gegen Militär-Regierung
Picha: AFP/M. El-Shahed

Kwa mujibu wa msemaji wa baraza la kijeshi la mpito, Jenerali Shamseddine Kabbashi ,mazungumzo hayo yataendeleo "kukiwa na matumaini makubwa ya "kufikia makubaliano". "Hatuna pupa ya kufikia ushindi muhimu" lilisema kupitia mtandao wa Twitter shirika la wasomi wa Sudan - waanzilishi wa vuguvugu la malalamiko. "Matokeo yoyote yatakayopatikana, yatamaanisha hatua moja mbele" amehakikisha  msemaji wa shirika hilo na kuongeza mazungumzo ya leo usiku yanahusiana na "madaraka ya utawala wa mpito."

Viongozi wa vuguvugu la malalamiko wanataka kwa kila hali raia aongoze taasisi hiyo muhimu ya mpito, baada ya wito wa jumuia ya kimataifa kutaka majadiliano yamalizike kwa kuundwa "kipindi cha mpito kitakachopongozwa na raia."

"Mshika bendera wa vuguvugu hilo - Muungano kwaajili ya uhuru na mageuzi walisema jana mazungumzo yangejikita katika suala la kugawana viti vya baraza la mpito kati ya wanajeshi na raia pamoja pia na kumteuwa atakaeliongoza baraza hilo.

Msemaji wa baraza la kijeshi la mpito jenerali Shamseddine Kabbashi
Msemaji wa baraza la kijeshi la mpito jenerali Shamseddine KabbashiPicha: Getty Images/M. El-Shahed

Wafuasi wa itikadi kali wadai sharia ya kiislam itumike

Wanajeshi na wanaharakati wanaopigania mageuzi walikubaliana kuhusu mada kadhaa kabla ya kusitisha mazungumzo yao-ikiwa ni pamoja na kipindi cha mpito cha miaka mitatu, kuundwa bunge la watu 300 na ambalo thuluthi mbili ni wawakilishi wa Muungano kwaajili ya Uhuru na Mageuzi.

Majadiliano yalisitishwa jumatano iliyopita na baraza la kijeshi linaloongozwa na jenerali Abdel Fattah al-Burhane aliyetwaa madaraka baada ya kupinduliwa na baadaye kukamatwa rais Omar al Bashir, Aprili 11 iliyopita. Wanajeshi walidai vizuwizi viondolewe na kusisitiza mwanajeshi ndie anaebidi kuongoza baraza la mpito.

 Kabla ya mazungumzo  kuanza , na kwa mara ya kwanza tangu Omar al Bashir alipopinduluiwa mamia ya wafuasi wa itikadi kali waliandamana jumamosi iliyopita mbele ya kasri la rais. Wanapinga aina yoyote ya utawala wa kiraia ambao hautaitumia sharia ya dini ya kiislam kuwa ndio muongozo wa sheria nchini Sudan.

Muungano kwaajili ya uhuru na mageuzi haujasema chochote bado kuhusu madai hayo.

Sheria ya Kiislamu inatumika nchini Sudan tangu mapindizu yaliyomleta madarakani Omar al Bashir aliyeungwa mkono na wafuasi wa itikadi kali mwaka 1989.

 

Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef