Mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini yaanza Addis Ababa | Matukio ya Afrika | DW | 07.01.2014
  1. Inhalt
  2. Navigation
  3. Weitere Inhalte
  4. Metanavigation
  5. Suche
  6. Choose from 30 Languages
Matangazo

Matukio ya Afrika

Mazungumzo ya kutafuta amani Sudan Kusini yaanza Addis Ababa

Wawakilishi wa serikali na waasi wa Sudan Kusini wameanza mazungumzo ya ana kwa ana nchini Ethiopia kutafuta amani katika taifa hilo changa ambalo limekumbwa na mzozo unaotishia kulitumbukiza katika vita

Mazungumzo hayo ya Addis Ababa yanaangazia pakubwa kusitishwa kwa mapigano ambayo yamedumu kwa wiki tatu sasa na ambayo tayari yamesababisha vifo vya zaidi ya watu elfu moja na kuwaacha wengine zaidi ya laki mbili bila makaazi.

Mjumbe mmoja wa serikali, Mabior Garang, ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wameanza mazungumzo yatakayokomesha uhasama kati ya pande zinazohasimiana.

Mwanadiplomasia mmoja kutoka Ethiopia amesema Jumuiya ya Ushirikiano ya nchi za Mashariki na Pembe ya Afrika, IGAD, inayosimamia mazungumzo hayo imewatuma wajumbe kwenda Juba kumshinikiza Rais Salva Kiir kuwaachia wafungwa wa kisiasa, suala ambalo upande wa waasi unataka litayafanya mazungumzo hayo yawe ya tija.

Rais wa Sudan Omar al Bashir(Kushoto) na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir mjini Juba

Rais wa Sudan Omar al Bashir(Kushoto) na Rais wa Sudan Kusini Salva Kiir mjini Juba

Wakati huo huo, askofu mkuu nchini Sudan ya Kusini, Daniel Deng Bul, ambaye ni miongoni mwa viongozi wakuu wa kidini nchini humo, amewaambia wajumbe wa pande zote mbili wanaofanya mazungumzo kuwa hatma ya taifa hilo changa liko mikononi mwao.

Hatma ya Sudan mikononi mwa wajumbe Addis

Bul amesema nchi hiyo inahitaji amani na ametoa wito kwa wajumbe wanaokutana Addis Ababa kuwa wajaribu kila wawezalo kusitisha vita kwani ni mzozo usiokuwa na manufaa yoyote huku watu wakizidi kupoteza maisha.

Licha ya kuanza kwa mazungumzo na wito huo wa kusitisha mapigano, pande zote mbili zinaendelea kuimarisha mapambano kote nchini humo, ikiwa ni chini ya miaka mitatu tu tangu nchi hiyo kusherehekea kwa mbwembwe uhuru walioupigania kwa hali na mali kutoka Khartoum.

Maelfu bado kambini

Hali katika mji mkuu wa Sudan ya Kusini, Juba, inaonekana kuwa kawaida hasa ikizingatiwa kuwa mji huo huwa na wanajeshi wanaoshika doria wakiwa katika magari, lakini kiasi ya watu laki tatu bado wana hofu kubwa mno kuondoka kutoka kambi za wanajeshi wa kulinda amani wa Umoja wa Mataifa na kurejea makwao.

Usiku milio ya risasi husikika na hali ya taharuki imetanda katika mji wa Juba. Maduka yamefungwa huku maelfu ya wafanyibiashara na wakaazi wakitoroka makwao na wengine wakivuka mipaka na kuingia nchi jirani za Uganda na Kenya.

Raia wa Sudan Kusini walioko katika kambi za wakimbizi mjini Bor

Raia wa Sudan Kusini walioko katika kambi za wakimbizi mjini Bor

Maafisa wa Umoja wa Mataifa wanasema wanaamini maelfu ya watu wameuawa na pande zote mbili zinashutumiwa kwa kuhusika na mauaji hayo na kwamba kambi za wanajeshi wa umoja huo zimefurika maelfu ya raia wanaotafuta hifadhi na usalama.

Hapo jana, Rais wa Sudan Omar al Bashir alifanya mazungumzo na mwenzake Kiir mjini Juba na kukubaliana kutuma kikosi cha pamoja cha jeshi ili kulinda maeneo yaliyo na mafuta huku China ambayo ni mwekezaji mkubwa zaidi katika sekta ya mafuta nchini humo ikitoa wito wa mapigano kusitishwa mara moja.

Mapigano yaliyozuka tangu tarehe 15 mwezi Desemba ambayo yanaonekana kuwa ya kikabila ni kati ya majeshi ya serikali ya Rais Salva Kiir na waasi watiifu wa aliyekuwa makamu wa rais Riek Machar aliyesimamishwa kazi na Kiir mnamo mwezi Julai mwaka jana.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/afp

Mhariri: Mohammed Khelef

DW inapendekeza